Picha na DW
SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imeahidi kuwapatia wakulima pembejeo na huduma nyengine za kilimo, ili kuwaondoshea changamoto kuelekea mapinduzi ya kijani kwa uchumi endelevu.
Aidha, Rais Dk. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuzitengeneza barabara zote zilizomo kwenye viwanja vya Maonesho ya Nane Nane Kizimbani, kwa kiwango cha lami ili kuyaongezea hadhi Maonesho ya mwakani.
Alisema, Serikali inawajibu wa kuhakikisha ardhi ndogo ya kilimo ilioyopo inatumika kwa ufanisi ili izalishe na kuongeza tija.
Akizungumzia hali halisi ya uzalishaji kilimo nchini, Rais Dk. Mwinyi alieleza Serikali imeweka jitihada mbalimbali kufanikisha sekta hiyo na kueleza kuwa na matokeo yenye tija. Alieleza ongezeko la uzalishaji wa mboga mboga na matunda nchini kutoka tani 64,820 mwaka 2021 hadi tani 66,304 mwaka 2022, muhogo umeongezeka kutoka tani 181,668 mwaka 2021 hadi tani 202,519 mwaka 2022.
Alisema, hizo ni dalili nzuri za mafanikio katika sekta ya Kilimo na Ufugaji kwa Zanzibar.
Alieleza lengo la Serikali kufanya Maonesho ya Kilimo ni kuhimiza kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa mbinu bora za kilimo ikiwemo matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji maji na zana za kisasa kwa madhumuni ya kuongeza uzalishaji kwa mazao ya chakula na biashara ili kupata tija zaidi na kuwapa faida kubwa wakulima na Taifa kwa jumla na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo ili kuendeleza sekta ya kilimo pamoja na kuhamasisha uwekezaji wa sekta binafsi
Akizungumza kwenye maonesho hayo, Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis alisema, wizara inajitahidi kutekeleza kwa vitendo maelekezo ya Serikali katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 145 ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 – 2025.
Uzinduzi wa Maonesho ya Nane Nane kwa mwaka 2023 ulikwenda sambamba uzinduzi wa Mkakati wa kilimo chini ya kaulimbiu isemayo “Vijana na wanawake ni msingi imara wa mifumo endelevu ya chakula”
IDARA YA MAWASILIANO, IKULU-ZANZIBAR
0 comments:
Post a Comment