Mbunge wa Bunge Maalum la Katiba Mh. Hamad Rashid Mohamed alisema kauna dhambi kubwa itakayofanywa na wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba linalofikia ukingoni mwake Mjini Dodoma kama kuwakosesha Watanzania rasimu ya Katiba Mpya wanayoisubiri kwa shauku kubwa.

Mh. Hamad Rashid alitoa kauli hiyo nzito wakati akitoa nasaha zake kwa niaba ya Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wa kundi la 201 kutoka Zanzibar kwenye chakula cha jioni kilichoandaliwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi nyumbani kwake Mtaa wa Farahani Mjini Dodoma.

Alisema Wajumbe hao wamebeba dhima kubwa kwa kukubali kwao kula kiapo kilichokwenda sambamba na kutumia kodi za Wananchi zilizotolewa kwa kutakiwa kuwatengenezea Watanzania Katiba mpya na si vyenginevyo.

Mh. Hamad alisema Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba hasa wale waliotoka vyama vya upinzani na taasisi za Kijamii wanapaswa kusimamia vyema ukamilishaji wa rasimu inayopendekezwa na Bunge hilo ili kukata kiu waliyonayo Watanzania kwa kipindi kirefu sasa.

Alisema Vyama vya upinzani zikiwemo taasisi za kijamii na wana harakati ndio waliosimama kidete kudai uwepo wa katiba mpya Nchini Tanzania jambo ambalo lilikuwa zito kukubalika ndani ya Uongozi wa chama tawala cha Mapinduzi { CCM }.

“ Hakuna nji nyengine ye yote ya mkato katika kukipa changamoto chama cha Mapinduzi isipokuwa upande wa upinzani kukubaliana na rasimu iliyoandaliwa na Bunge Maalum la Katiba itakayopelekwa kwa wananachi kwa ajili ya kupigiwa kura “. Alisema Mbunge huyo.

Mh. Hamad Rashid alitahadharisha kwamba Watanzania wamejinyima mambo ya msingi likiwemo suala la kuwapatia elimu watoto wao na kuwamua kodi wanazochangia kuzielekeza katika mchakato wa kupata Katiba mpya.

Aliwanasihi Viongozi wa kisiasa pamoja na jamii kuzikimbia choko choko za kisiasa zinazochangia cheche ya kusambaratisha jamii kama zilivyotokea katika Mataifa mbali mbali Duniani watu wakishuhudia matukio ya vyurugu kupitia vyombo vya Habari.

Alisema Tanzania hadi sasa bado haijafikia hatua za Watoto pamoja na wake wa Wabunge kuteswa, kudhalilishwa hadi kufikia hatua ya kubakwa kutokana na vurugu zinazotokana na siasa na hitilafu za Kidini kama zinavyofanyika katika Mataifa tofauti Ulimwenguni.

“ Tuzikimbie choko choko za kisiasa na kidini zinazowasambaratisha wana jamii kama zilivyowakumba wenzetu Wakorea na Wajerumani ambao historia inaeleza kwamba walikuwa wamoja “. Alisema Mh. Hamad.

Alifahamisha kwamba Tanzania ina fursa kubwa ya Kidemokrasia iliyojengeka tokea kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa ambayo imekuwa ikipatikana ndani ya vyombo vyake vya maamuzi.

Hata hivyo alitanabahisha kwamba yapo makosa na hitilafu ndogo ndogo zitakazoweza kujitokeza kwenye Katiba Mpya endapo itapatikana baada ya kupigiwa kura. Lakini alisema masuala na hitilafu hizo yachukuliwe kuwa ni udhaifu walionao wanaadamu.

Mjumbe huyo wa Bunge Maalum la Katiba aliwaomba Wajumbe wote wa Bunge hilo kuwafariji Viongozi wakuu wa Taifa hili Rais Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar Dr. Ali Moh’d Shein kwa kuwapatia Katiba Mpya ili kutimiza ndoto yao ya kujenga Historia mpya ndani ya Kipindi cha miaka 50 ya Muungano wa Tanzania.

“ Tunapaswa kuwafariji Viongozi wetu Rais Jakaya Kikwete na Rais Sheni kwa kutupa fursa hii ya kihistoria ya kuandika Katiba mpya bila ya kutusimamia wakati wote wa kazi zetu za mchakato. Kwa kweli tunastahiki kuwapatia zawadi hii Wakuu wetu hawa “. Alisisitiza Mhe. Hamad.

Mh. Hamad alisema Viongozi hao wawili wamekuwa mfano wa kuigwa na Mataifa mengine Duniani kwa uvumilivu wao mkubwa uliotoa fursa nzuri kwa wajumbe hao kuendelea na mchakato wao bila ya kuwasimamia kama inavyotokea kwa mataifa mengine wakati wa michakato kama hiyo.

Mapema akiwakaribisha wajumbe hao wa Bunge Maalum la Katiba kupitia Kundi la 201 kutoka Zanzibar Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema rasimu iliyoandikwa na Bunge hilo imeisaidia sana Zanzibar kwa zaidi ya asilimia 90% hali ambayo hata Watanzania Bara wameilalamikia.

Balozi Seif alisema wakati huu ni muhimu na ndio mahali pekee pa kupata maslahi ya Zanzibar ndani ya jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, vyenginevyo Zanzibar itaendelea kulalamika kero za Muungano endapo rasimu itayopendekezwa na Bunge Maalum haitapita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Wajumbe hao wa Bunge Maalum la Katiba kupitia kundi la 201 kwamba Zanzibar ilikuwa na malalamiko mengi kuhusu kero za Muungano masuala ambayo sasa ni muda muwafaka kuyamaliza kupitia mchakato walionao mikononi mwao hivi sasa.

Alisema koti la Tanzania Bara linalodaiwa kuvaliwa ndani ya Mambo yasiyo ya Muungano litaweza kuvuliwa iwapo rasimu hiyo itakipiga kura na kupita kwa theluthi mbili pande zote za Muungano jambo ambalo litatoa fursa kwa Zanzibar kutekeleza mambo yake yenyewe yaliyokuwa nje ya Muungano.

Alisema kukosekana kwa Katiba mpya kwa sababu za Wazanzibari ndugu zao wa upande wa Tanzania Bara hawata waelewa na watawashangaa kwa kupata fursa hii adhimu na ya pekee na badala yake wakaichezea.

“ Katiba ikikosekana kwa sababu zetu sisi Wazanzibari ndugu zetu wa Tanzania Bara hawatatuelewa na watatushangaa sana baada ya kuipata fursa hii adhimu tukaitupa “. Alieleza Balozi Seif.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top