Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haitosita kujenga Miradi ya maendeleo inayowanufaisha wananchi wake Nchini.
 
Mhe. Hemed ameyasema hayo alipofanya Ziara Katika Jimbo la Pangawe na Jimbo la Fuoni Wilaya ya Dimani kichama ikiwa ni  muendelezo wa ziara zake za kukiimarisha Chama Cha Mapinduzi katika Majimbo yote ya Uchaguzi ya Zanzibar.
 
Amesema Serikali ya awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeshafikia asilimia kubwa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020- 2025 ndani ya Miaka miwili. Hivyo, ni wajibu wa Viongozi wa ngazi zote wa Chama Cha Mapinduzi kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali yao.
 
Amesema ni wajibu wa kila mwananchi kuunga Mkono juhudi zinazochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi ili mema mengi yaweze kutekelezwa kwa wakati.
 
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Tanzania inapiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na dhamira njema ya Viongozi wake wenye chachu ya mabadiliko kwa wananchi wao.
 
Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed ameweka Jiwe la Msingi la ujenzi wa Tawi la CCM Pangawe Bondeni  na kueleza kukemea tabia ya baadhi ya Viongozi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi wanaopanga safu za Uongozi wa Uchaguzi wa Dola wa mwaka 2025 na kusema kuwa CCM haitamvumilia mtu yeyote atakayejaribu kufanya kitendo hicho.
 
Ameeleza kuwa kufanya hivyo ni kukiuka taratibu na Kanuni za Chama na kuwavunja moyo viongozi waliopewa dhamana ya Uongozi na Chama Cha Mapinduzi.  Ameendelea kukemea tabia hiyo na kuonya kwa kila atakayekiuka kanuni na taratibu za Chama taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwani kipindi hiki inapaswa kitumike katika kuimarisha Chama.
 
Nae Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Jimbo la Pangawe Ndugu Dadi Juma Dadi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi wa Jimbo la Fuoni Ndugu Muharami Mwinyi Kombo wameeleza kuwa wanaendelea na ujenzi wa Majengo ya Kisasa ya Chama ikiwemo Matawi ili kuwawekea mazingira mazuri wanachama na viongozi wa CCM katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
 
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Magharibi B ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Fuoni Kipungani Khamis Hassan Haji amemshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi kwa kuelekeza miradi mingi ya Maendeleo katika Manispaa ya Magharibi B hasa ujenzi wa Soko la Mwanakwerekwe na Soko la Jumbi.
 
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top