Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewataka  Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kusimamia Misingi ya Chama hicho kwa kujenga umoja, mshikamano, heshima na nidhamu pamoja na  kuhakikisha CCM inaendelea kushika Dola kila unapofika Muda wa Uchaguzi.
 
Mhe. Hemed ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameyasema hayo wakati akizungumza na  wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi katika ziara yake ya kukagua uhai wa Chama katika Jimbo la Kiembesamaki na Jimbo la Dimani Wilaya ya Dimani Kichama.
 
Amesema Tanzania inajengwa kwa kusimamia misingi ya umoja, mshikamano iliyoasisiwa na waanzilishi wa TANU Marehemu Mwalimu Julias Kambarage Nyerere na muanzilishi wa ASP Marehemu Sheikh Abeid Amani Karume ambayo inaendelezwa na Mwenyekiti wa CCM Taifa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
 
Mhe. Hemed amewataka Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi Nchini kuhakikisha wanachama wote wanasajiliwa katika Mfumo wa kadi za Elektroniki ili kukiendeleza Chama.
 
Amesema Dhamira ya Chama Cha Mapinduzi ni kuhakikisha wanachama wote wanasajiliwa katika Mfumo huo ambao utakuwa na taafira zote za msingi za mwanachama .
 
Aidha Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa amewakumbusha wanachama kulipa ada za uanachama ili kukiendeleza Chama hicho.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaendelea kusimamia hali za watendaji wake katika ngazi zote hasa Mashina ambapo amewapongeza Mabalozi wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kukisimamia Chama.
 
Mhe. Hemed amewataka Wabunge, Wawakilishi na Madiwani kufanya ziara katika maeneo yao ili kujua shida za Wananchi na kusimamia dhamana na jukumu lao la kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2020 - 2025.
 
Aidha amewataka Viongozi hao kusimamia jukumu lao la msingi waliopewa na Chama Cha Mapinduzi la kuwatumikia na kuzishirikisha Kamati za Siasa katika mipango ya maamuzi ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi.
 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali inaendelea na ujenzi wa Miradi mbali mbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Skuli Chukwani, Ujenzi wa Barabara pamoja ujenzi wa Miundombinu ya maji hatua ambayo itasaidia kumaliza changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi na kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
 
Kwa upande wake Katibu Siasa, Itikadi na Uenezi Zanzibar Khamis Mbeto Khamis amemshukuru Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa kwa ziara yake hiyo ambayo inaonesha wazi utayari wa Viongozi wakuu wa CCM katika kukiimarisha Chama.
 
Nao Viongozi wa Mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi Ngazi ya Majimbo, Wilaya, Mkoa na Taifa wameeleza kuwa ni wajibu wa Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali zote mbili zinazoongozwa na CCM na kuwataka vijana kuwa mstari wa mbele kueleza mema hayo na kuacha kusikiliza maneno yasio na ukweli.
 
Katika Ziara hiyo Mjumbe huyo wa Kamati ya Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amepokea Taarifa ya utekelezaji wa Jimbo la Kiembesamaki na Jimbo la Dimani, amekagua Ujenzi wa Tawi la CCM Michungwani, ujenzi wa Ofisi za CCM Jimbo la Dimani.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top