Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuwaenzi wanazuoni waliowarithisha Elimu ili kuthamini jitihada zao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajji Dkt Hussein Ali Mwinyi ametoa kauli hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla katika hafla ya ufunguzi wa Majengo mapya ya Madrasatu Nour Ukutani Mkunazini Wilaya ya Mjini Unguja.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo na kuyatumia vyema kwa kuwapa watoto mafunzo ya Qur-an na masomo ya Dini ni katika kuenzi jitihada za muasisi wa Madrasa hiyo Almarhuum Sheikh Abdallah Bin Abubakar Bin Abdallah Baakathir.
Amesema ni vyema kwa walimu wa Madrasa hiyo kuzidi kuitunza mirathi hiyo na kuiendeleza zaidi kielimu ili Madrasa hiyo ibaki katika hadhi yake kama ilivyo na kufikia malengo ya muasisi wa madrasa hio.
Aidha Rais Dkt Mwinyi amesema kazi za kujenga Madrasa ni Sadaka inayoendelea inayomfaa Muumini hapa hapa Duniani na baada ya kufa hivyo amewataka waumini kutoa kwa Nia ya kutaraji malipo kutoka kwa Allah subhana wataala.
Sambamba na hayo Rais Dkt Mwinyi amewaasa wazazi na walezi kuthamini juhudi za walimu wa Madrasa kwa kufanya juhudi za Makusudi katika kutoa michango ya Mwezi iliyowekwa na Madrasa ili kuwatia moyo waweze kuendelea kuwatunza watoto ili kuwa na Tabia njema na kuwa na fani mbali mbali za Dini kwa ufanisi uliotukuka zaidi.
Pamoja na mambo mengine Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ametumia fursa hiyo kuipongeza Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuendelea kufanya ukaguzi na usajili wa Madrasa pamoja na Walimu ili kuwa na walimu wenye ujuzi na weledi katika kutoa elimu bora kwa watoto.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema ni vyema kwa wafadhili wa majengo ya Madrasa na Misikiti kuzingatia miundombinu ya watu wenye mahitaji Maalum ili nao kuweza kufanya Ibada pamoja na kupata taaluma kwa mazingira rafiki kwao.
Aidha amesema amesema Ofisi Ya Mufti Mkuu wa Zanzibar itaendelea kusimamia Maadili katika Madrasa ili kusimamia misingi ya Dini ya Kiislamu katika kuongoza Madrasa hizo.
Nae Mudir wa Madrasatu Nour Ukutani Zanzibar Sheikh Abdulrahman Bin Shareef Habshy ameeleza kuwa ujenzi wa Majengo hayo inaakisi muendelezo wa utoaji wa Elimu bora ya Dini kwa vijana wa Zanzibar ili waweze kusoma katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kupata taaluma sahihi inayohitajika.
Aidha amesema Madrasa za Qur-an zinajukumu kubwa la kulea na kukuza watoto kuwa na malezi mazuri yatakayowasaidia kuja kuwa na jamii bora hapo baaadae.
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment