Viongozi wa Kamati za Misikiti wametakiwa kushikamana ili kusimamia Ibada katika Misikiti wanayoisimamia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla ametoa wito huo wakati akizungumza na waumini wa Masjid Zam Zam uliopo Kibele Maftani Mkoa wa Kusini Unguja katika hafla ya ufunguzi wa Mskiti huo.

Amesema Imani waliyopewa viongozi hao kusimamia misikiti hiyo inahitaji Busara na Hekima ili kufikia lengo la kujengwa kwa Msikiti huo.

Aidha mhe. Hemed amesema ni vyema kwa misikiti kutumika kwa masuala mbali mbali akitolea mfano kusomesha vijana juu ya masuala ya Ibada pamoja na ya kijamii ili kuwajenga watoto katika makuzi mema.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameeleza kuwa jambo la ujenzi wa Misikiti ni katika Sadaka kubwa ya kuendelea ambayo itamfaa muumini baada ya kuondoka duniani.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Hemed amewataka waumini wa Msikti huo kuutumia kukataza matendo maovu ambayo Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Ali Mwinyi imedhamiria kuyamaliza nchini.

Kwa upande wake Naibu Mufti Mkuu wa Zanzibar Shekh Mahmoud Mussa Wadi amesema ni vyema kwa viongozi wa Misikiti kuwaandaa vijana kuja kuwa Maimamu wa kusimamia Misikiti.

Aidha Sheikha Mahmoud amewataka viongozi wa Msikiti huo kuepuka mivutano inayojitokeza baadhi ya Misikiti na kuwataka kufata kigezo chema cha Mtume Muhammad (S.A.W) na kudumisha usafi wa msikiti huo.

Abdulrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top