Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameipongeza Taasisi ya Alhikma Foundation kwa kuandaa mashindano ya kuhifadhi Qur-an Afrika.

Mhe. Hemed ametoa pongezi hizo katika hafla ya uzinduzi wa mashindano ya 22  ya Qur-an Tukufu Afrika iliyofanyika katika ukumbi wa Hayatt Regency Hotel Kilimanjaro jijini Dar-es-Salaam.

Amesema ni wazi kwamba Mashindano hayo yanayofanyika kila ifikapo Mwezi Mtukufu wa Ramadhan wakila mwaka yameamsha hisia za wengi ulimwenguni kwa jinsi Waumini wanavyojitokeza kwa wingi kuungana na waandaji wa Mashindano hayo.

Aidha Mhe Hemed amesema kitendo cha kupata hadhira kubwa katika mashindano hayo ni kuonesha wazi namna vijana walivyokihifadhi kitabu Kitukufu cha Qur-an na wanavyohamasika katika kukisoma pamoja na  kukihifadhi kitabu hicho.

"Vijana wetu wameshajishika sana katika kusoma na kuhifadhi Qur-an, kwa hakika mashindano haya ni ya kupigiwa Mfano. Hongereni sana" amesema

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameitaka Taasisi ya Alhikma Foundation na Taasisi nyengine kujikita katika masuala mazima ya kuhifadhi Maadili ya vijana na kubuni njia bora za kuwakuza kimaadili ili kuweza kupata jamii bora yenye Maadili mema hapo baadae.

Amesema ni vyema kwa wazazi na walezi kuwasimamia watoto wao kuhifadhi na kuifuata Qur-an katika Maisha yao  hatua ambayo itasaidia kuweka Maadili mema katika Jamii. G

Hata hivyo Mhe. Hemed ametumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi hiyo kuisaidia Serikali katika kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo Elimu na Afya hatua ambayo Dini ya Uislamu umehimiza masuala hayo.

"Kwa hakika mambo haya ni ya kupigiwa mfano na ni yakuigwa na Taasisi nyengine ili jamii yetu izidi kupata maendeleo endelevu na kuweza kukuza na kuboresha hali za maisha ya jamii inayotuzunguka" Mhe. Hemed

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ametumia fursa hiyo kuwanasihi wafanyabiashara kufanya Tahfifu kwa kadri inavyowezekana ili kuweza kutoa huduma bora kulingana na  hali za maisha kwa wananchi hasa katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Pia amewataka waumini hao kuendelea kulinda Amani na Utulivu uliopo pamoja na kuzidisha mshikamano baina yao ili Taifa llizidi kubaki katika Amani kipindi chote na Serikali kuweza kutekeleza ahadi zake kwa vitendo kwa wananchi wake.

Kwa upande wake Rais wa Alhikma Foundation Sheikh Abdul-Qadir Al-Ahdaly amesema kuandaa kwa Mashindano hayo ni kuonesha ari kwa Taasisi hiyo kuona wanaohifadhi Qur-an nchini wanajipamba na tabia njema zilizomo ndani ya kitabu kitukufu cha Qur-an.

Nae Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Alhikma Foundation Sheikh Nurdin Kishki amesema lengo la kuanzisha Mashindano hayo ya Qur-ani  ni kuirejesha jamii katika kusimamia Kitabu kitukufu cha Qur-ani na kueleza kuwa kwa mwaka huu mashindano hayo yatajumuisha Nchi ishirini na Mbili.

Akitoa Salamu za Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume Katibu Mtendaji Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar ameitaka jamii kujifungamanisha na Qur-an katika Maisha ya kila siku na kukemea tabia ya baadhi ya  madrasa kutumia Qur-an kinyume na Sheria akitolea mfano upiga wa Dufu kwa kutumia baadhi ya aya za Qur-an kuzifanya kuwa ndio nyimbo zao.

Abdullrahim Khamis

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top