Waumini wa Dini ya Kiislamu wana wajibu wa kuungana na Wananchi wenzao Nchini katika kuona Taifa linaendelea kupata Maendeleo ya haraka ili ustawi wa maisha yao uimarike katika kipindi kifupi kijacho kama ilivyo azma ya Serikali Kuu ya kuwasogezea huduma muhimu.

Akitoa salamu mara baada ya Ibada ya sala ya Ijumaa katika Msikiti Mkuu wa Kijiji cha Chwaka Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Uchaguzi Mkuu umemalizika na kazi iliopo hivi sasa ni kujenga Nchi  na Wananchi ndio wadau wakuu

Mh. Hemed alisema wakati Serikali Kuu tayari imeshajizatiti kuendeleza  Nchi katika Mfumo wa Umoja wa Kitaifa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984 Wazanzibari wana wajibu wa kuendelea kudumisha Umoja, Ushirikiano na mshikamano ili kufanikisha malengo hayo muhimu.

Alieleza kwamba Kazi ya kuhudumia Wananchi inahitaji ushirikiano mkubwa. Hivyo kupitia ahadi za Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi alizozitoa wakati wa Kampeni ya Uchaguzi zitapatiwa  ufumbuzi unaostahiki kwa mujibu wa mahitaji ya Jamii na maeneo husika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaeleza Waumini hao wa Dini ya Kiislamu wa Chwaka na vitongoji vyake kwamba Serikali Kuu inalewa fika baadhi ya maeneo yanayoendelea kukumbwa na changamoto tofauti ikiwemo huduma za Maji safi, Bara bara, Afya huduma za Elimu ambazo kupitia Ilani ya Uchaguzi zitaendelea kupatiwa ufumbuzi.

Alielezea faraja yake kuona Jamii katika maeneo mbali mbali Nchini meanza kuona na kushuhudia azma ya Serikali yao katika kuwasogezea Maendeleo kwenye sehemu zao. Hivyo amewaomba kupitia maeneo yao ya Ibada waendelee kuliombea Taifa livuke salama katika azma hiyo njema.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Waumini wa Kijiji hicho Mmoja wa Viongozi wa Msikiti Huo Sheikh Makame Khamis alisema Jamii ya Kijiji hicho imepata faraja kutokana na ujio wa Viongozi Wakuu kwenye maeneo yao ikiwa ni ishara njema kwao.

Sheikh Makame alisema wao kama Wananchi wengine wako tayari kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuwasogezea huduma muhimu za Maendeleo ambazo tayari wameanza kujenga matumaini makubwa kutokana na uharaka wa Serikali iliyoanza kuwajibika ndani ya kipindi cha Mwezi Mmoja sasa.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top