Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla  alisema Wataalamu wa Lugha ya Kiswahili wana jukumu adhimu la kuhakikisha kwamba Lugha hiyo pamoja na lahaja zake zote inalindwa, inaendelezwa na kukuzwa ili izidi kuzungumzwa na kutumika katika mambo mengi zaidi kwenye ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.

Alisema Lugha ya Kiswahili lazima iwe na misamiati ya kutosha  katika Nyanja ya kiufundi, teknolojia ya Habari na mawasiliano, sanaa, sheria, michezo,dini na Nyanja zote za kiuchumi kwa lengo la kuwa na nguvu kubwa itakayojitosheleza ili kuepuka kuwa fukara kwa kutegemea misamiati ya Lugha nyengine.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo akimuwakilisha Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi katika hafla ya ufunguzi wa Kongamano ya Nne la Kiswahili la Kimataifa la Siku Mbili lililoandaliwa katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Alisema kumekuwa na Utamaduni wa kukivuruga Kiswahili bila ya aibu hasa kwa Wanajamii walio wengi ambao hufuata mkumbo jambo ambalo huleta athari isiyopendeza katika matamshi ya Lugha yenyewe inayo lahaja za kupendeza katika uzungumzaji wake.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alibainisha kwamba Wanahabari na Wasomi ndio wanaotegemewa katika kuiendeleza Lugha ya Kiswahili. Hivyo ni vyema kuwa makini katika matumizi yake hasa wakati wanapotoa Taarifa mbali mbali kwa wana Jamii.

“ Mnahitaji mjue jinsi ya kuteua maneno na pale mnapokosa uhakika wa uteuzi wa maneno muwafaka basi ulizeni kwa wanaojua. Eleweni kwamba nyinyi ndio mnaosikika kwa haraka zaidi na kuigwa na wanajamii”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Alisema amevutiwa na juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Baraza la Kiswahili Zanzibar { BAKIZA} kwa kushirikiana na Taasisi tofauti za Serikali na hata za kiraia katika kuandaa Kongamano hilo kila Mwaka linalowajumuisha Wataalamu waliobobea katika Lugha ya Kiswahili waliopo Zanzibar, Ukanda wa Afrika Mashariki na Nchi nyengine za Mabara ya Amerika na Asia.

Alieleza kwamba umuhimu wa Kongamano la Kiswahili la Kimataifa  unazidi kuonekana kila Mwaka kutokana na mafanikio yanayopatikana ambayo yamesaidia kuwezesha kwa sasa Lugha ya Kiswahili kuwa miongoni mwa Lugha kubwa Kimataifa yenye kutumika katika shughuli mbali mbali.

Alifahamisha kwamba zipo Takwimu na baadhi ya Vitabu vilivyoandikwa vikionyesha  Kiswahilki kimekuwa Lugha ya Saba kati ya Lugha zenye kuzungunzwa na Mataifa mbali mbali kukiwa na idadi ya wanaozungumza na kukifahamu inayokisiwa kufikia Watu takriban Milioni 160 Idadi inayoongezeka kwa haraka kadri ya miaka inavyosonga mbele.

Alisema tafsiri ya Takwimu hizo ni kwamba juhudi hizo za pamoja za kukikuza na kukitangaza Kiswahili zinaendelea kutoa matunda mazuri hasa kwa vile tayari kimesharidhiwa kuwa Lugha inayozungumzwa ndani ya Mikutano ya Viongozi wa Umoja wa Afrika {AU} na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika {SADC}.

Mheshimiwa Hemed  alitanabahisha kwamba Historia inafunza kuwa ili Lugha yoyote iendelee kuwepo, ikue, isambae na iwe inatumika katika Nyanja tofauti, lazima iwepo mipango na jitihada maalum za kufikia huko  kwa vile ni chombo cha  mawasiliano miongoni mwa Wanaadamu.

“ Tunajifunza kwamba kulikuwa na Lugha nyingi sana tofauti, lakini kati ya Lugha hizo nyengine zimekufa kutokana na kushindwa kwenda sambamba na mabadiliko kadhaa yanayojitokeza katika mifumo ya maisha ya Wanaadamu”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

Alibainisha kwamba Utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni {Unesco} kuhusu Lugha zilizo hatarini kutoweka, unaonyesha kwamba baina ya Mwaka 1950 hadi 2010, jumla ya lugha ndogo ndogo 230 zimetoweka katika kipindi cha Miaka 60 iliyopita.

Mheshimiwa Hemed Suleiman  alieleza hadi Mwaka 2,000 ilikadiriwa kwamba zipo jumla ya Lugha elfu 7,000 zinazozungumzwa Duniani kote lakini kuna uwezekano mkubwa wa kwamba kati ya Lugha hizo asilimia 50% hadi 90% huenda zikawa zimeshakufa ifikapo Mwaka 2050.

Alisema kwa kutambua umuhimu wa Lugha ya Kiswahili kupitia Hotuba aliyoitoa Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi  wakati akilifunguwa Baraza la Wawakilishi Zanzibar aliahidi kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane itafanya jitihada kubwa za kuendeleza na kuitunza Lugha ya Kiswahili.

Mh. Hemed alieleza katika kutekeleza ahadi yake mkazo utawekwa katika kufanya Utafiti kwenye maeneo ya Fasihi na Isimu pamoja na Tamaduni za Asili akielezea kutokuwa na shaka kwamba Wataalamu wa Lugha hiyo watatoa rai na michango inayohitajika ili kuweza kufikia azma iliyokusudiwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuelezea kuvutiwa na kufarajika kwa Ujumbe wa Kongamano hilo la Mwaka huu unaoeleza “Tuchangamkieni Fursa za Soko la Kiswahili Duniani”.

Alisema Ujumbe huo unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kukuza ajira ili kupunguza tatizo la ajira linalowakabili  Vijana na Wananchi wa Rika mbali mbali Nchini. Hivyo Ujumbe huo usiishie vitabuni bali utekelezaji wake lazima uwe wa vitendo.

Alifahamisha kwamba Mwaka ujao anaweza kupata faraja na furaha kubwa pale Uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {BAKIZA} utapokuja kutoa Takwimu za ajira ndani na nje ya Nchi zilizopatikana kupitia Wataalamu waliopata Elimu ya Lugha ya Kiswahili Vyuoni.

Mh. Hemed alisema si jambo la kuridhisha hata kidogo kuona kwamba  fursa za ajira zipo na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar {SUZA} kinafundisha masomo ya Kiswahili hadi ngazi ya Uzamivu, lakini bado idadi ya Wataalamu wanaopata ajira nje ya Nchi katika fani zinazohusiana na Kiswahili haieleweki.

“ Nitapenda kusikia au kuona ni Watu wangapi kutoka Zanzibar wameajiriwa nje ya Nchi katika ufundishaji, Utangazaji, utunzi, Ukalimali, Uhariri na Uchapishaji”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Aliupongeza Uongozi wa Baraza la Kiswahili Zanzibar {Bakiza} kwa kuandika Kitabu kinachomuelezea Dr. Shein na Maendeleo ya Kiswahili Zanzibar 2010 -2020 kwa Heshima ya Kumuenzi Kiongozi huyo wa Awamu ya Saba ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliyeweka uzio katika kuiimarisha Luha ya Kiswahili.

Ameuhimiza Uongozi huo wa Bakiza kuongeza kasi katika kuhifadhi na kutangaza kazi zao mbali mbali katika mfumo wa Kisasa wa Mawasiliano ikiwemo mitandao ya Kijamii kwa vile Vijana wengi wanapenda kupata Taarifa kupitia Mitandao kuliko zile njia za asili za machapisho.

Alisema nukuu walizokusanya na Kazi nyengine za Riwaya, tamthilia na mashairi, tenzi kutoka kwa waandishi mbali mbali zikiwemo nukuu muhimu za Viongozi wa Kitaifa walioko madarakani na walioondoka ziwe zinapatikana katika Tovuti yao kwa vile eneo hilo bado halijafanyiwa Kazi vizuri.

Akitoa Salamu fupi ya Kongamano hilo Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Zanzibar Dr. Mohamed Seif  Khatib alisema moja kati ya kitu dhimu kwenye mjumuiko huo ni pale washiriki wa Kongamano hilo kutengewa muda mahsusi wa kutembelea maeneo ya Kihistoria hapa Nchini.

Dr. Mohamed alisema Maeneo hayo maalum yameguswa na Watunzi kwenye Vitabu walivyovitunga ambapo kwa Mwaka Huu Mtunzi Marehemu Mohamed Said Mohamed maarufu Bwana MSA aliligusa eneo la Kazole kwenye panga maalum litakalotembelewa na Washiriki hao.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi kulifungua Kongamano hilo, Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mheshimiwa Tabia Maulid Mwita alisema kuendelea kufanyika pamoja na usiriki wa Wadau wa Kiswahili ni moja ya Heshima kubwa inayoipata Zanzibar.

Tabia alisema dhamira ya Kongamano hilo inadhihirisha wazi ile kasi ya Serikali katika kueneleza nguvu zak kwenye Uchumi ndani ya muelekeo wa Uchumi wa Buluu ambao machapisha ya Lugha ya Kiswahili katika Vidhaa zinazoingia kwenye soko la Utalii yataendelea kupata nafasi.

Waziri wa Habari, Vinaja, Utamaduni na Michezo alieleza kwamba Wizara hiyo imejipanga kuandaa Programu ya mashindano ta Mashairi kwa Wanafunzi wa Skuli za Sekondari kwenye Kongamano la Tano litakalosimamiwa na Bakiza hapo Mwakani yatakayosaidia kuzalisha Wasomi zaidi wa Kiswahili.

Katika ufunguzi huo wa Kongamano la Kiswahili la Kimataifa ya Nne Mgeni Rasmi alipata wasaa wa kuzindua Kitabu Maalum pamoja Bango la Nukuu za Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awmu ya Saba Dr. Ali Mohamed Shein.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top