Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameagiza Chombo chochote cha Moto iwe cha Binafsi na hata kile cha Serikali kuanzia sasa lazima kilipiwe Bima ili kuheshimu Sheria iliyowekwa na Serikali Kuu.

Alionya kwamba endapo chombo cha Serikali kitapata ajali atakayewajibika kulipa hasara itakayotokea ni Mkuu wa Taasisi inayotumia chombo hicho akiwa Waziri, Katibu Mkuu, Mkurugenzi na Wakuu wa Taasisi za Umma.

Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alitoa agizo hilo hapo afisini kwake Vuga wakati akizungumza na Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania {TIRA} ulioambatana na Wakurugenzi na Mameneja wa Mashirika ya Bima Nchini.

Alisema Sheria tayari imeshalekeza vyombo vyote vya Moto lazima vikatiwe Bima ambapo inasikitisha kuona kwamba Bajeti za vyombo hivyo kwa Taasisi za Umma imekuwa ikitengwa kila Mwaka lakini hakuna mfumo sahihi wa Fedha unaotumiwa kwa ajili ya Kazi hiyo.

Aliwataka Viongozi wa Taasisi zote kuhakikisha wanasimamia vyema upatikanaji wa Mapato ya Serikali kwa kuepuka Rushwa, Ubadhirifu, Uzembe na ukosefu wa uwajibikaji ambao kamwe Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imejitolea kupambana nao kwa hali yoyote ile.

Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba Sekta ya Bima imekuwa na mchango mkubwa wa kuongeza Mapato ya Taifa ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibat imedhamiria kuweka mkazo Zaidi kwenye Sekta hiyo muhimu ya Kifedha.

Akizungumzia Mawakala wababaishaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimtaka Kamishna wa Usimamizi wa Bima Tanzania kufuatilia Taasisi za Bima zinazojihusisha na Mawakala wa  aina hiyo na pale atakapogundua suala hilo lazima achukuwe hatua za Kisheria mara moja.

Alisema Mawakala wababaishaji wanapaswa kuondolewa  mara moja kutokana na dhulma wanayoifanya katika Jamii  kwa vile haikubaliki hasa ikizingatiwa kwamba  inarejesha nyuma  Imani za Wananchi pale wanaohitaji huduma za Bima.

Mheshimiwa Hemed alifahamisha kwamba yapo matukio kwa baadhi ya Wananchi wanayopambana nayo zaidi wakati wa kukata Bima pamoja na pale vyombo vyao vinapopata ajali wakijikuta wanazunguusha na hatimae kukata tamaa ya kukosa haki zao za msingi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania kuimarisha Afisi yake pamoja na kuongeza Wanasheria VisiwaniZanzibar watakaowajibika kuondosha changamoto zinazowakuta Wananchi hasa kwenye kesi za Madai ya Vyombo vinavyopata ajali  ambazo chukuwa muda mrefu.

“ Zipo Kesi za masuala ya Bima hasa ajali zinazoshindwa kupata ufumbuzi kwa kukosa Mwanasheria. Urasimu lazima uondoshwe kwa vile Serikali haipendelei kupata au kusikia malalamiko kutoka kwa Wananchi juu ya suala hilo”. Alisisitiza Mheshimiwa Hemed.

Aliwakumbusha Viongozi hao wa Taasisi zinazosimamia masuala ya Bima Tanzania kuangalia Sheria zenye utata katika uwajibikaji wao wa kila Siku  na baadae kuziwasilisha katika ngazi ya maamuzi za Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho.

Wakitoa ufafanuzi wa baadhi ya majukumu yao baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Bima Nchini walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kazi yao kubwa ni kutafsiri muono wa Viongozi wa Serikali katika uimarishaji wa Uchumi utakaomkomboa moja kwa moja Mwananchi.

Walisema Mikakati madhubuti itawekwa katika kuhakikisha  bidhaa za Kilimo zinapatikana kwa Wakulima sambamba na kuwekwa mkazo hivi karibuni kwenye msukumo wa Sekta ya Uvuvi katika kuunga mkono Uchumi wa Buluu ambao ndio Dira ya Serikali kwa wakati huu.

Baadhi ya Wakuu hao wa Taasisi za Bima walifahamisha kwamba tayari wamejenga matumaini makubwa yanayotoa ishara ya Siku za baadae Sekta ya Bima itachangia asilimia 20% ya Pato la Taifa kutokana na kasi kubwa inayosimamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane.

Mapema Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania Nd. Muusa Juma alisema kwa vile Washirika wa Bima ndio wenye jumuku la kusimamia Mapato sahihi ya Taifa ipo mikakati tofauti inayotekelezwa kwa lengo la kuwafikia Wananchi ambao ndio Wadau wakuu.

Hata hivyo Nd. Mussa alisema safari ya kuelekea kwenye soko sahihi la Bima bado ni ndefu kutokana na uelewa mdogo wa Wananchi walio wengi hasa katika masuala ya kuweka Bima kwenye matukio ya Majanga pamoja na ajali zinazosababishwa na vyombo wanavyotumia.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top