Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wazee na Wazazi Nchini kuendelea kuwekeza katika Sekta ya Elimu ili jitihada hizo ziwe fursa na matunda bora yatakayowajengea njia sahihi Watoto wao katika Maisha yao ya baadae.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza hayo kwenye Mahafali ya Nane ya Wahitimu wa Chuo cha Afya kiliopo Mtaa wa Kwamchina mwanzo { Zanzibar Shool of Healthy} waliotunukiwa Stashahada katika  fani za Uuguzi na Ukunga, Ushauri Nasihi, Afisa Tiba pamoja na Astashahada ya Ushauri Nasihi, hafla iliyofanyika katika Uwanja wa Michezo wa Mao Zedong.

Alisema Wazazi na Wazee umefika wakati lazima wabadilike na kujenga Utamaduni wa kutumia nguvu zao kubwa katika Elimu ya Kizazi chao  badala ya baadhi yao kuendeleza tabia ya kutenga fedha nyingi kwa ajili ya kuwafanyia sherehe kubwa Watoto wao wakati wanapofunga ndoa.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alibainisha wazi kwamba Elimu pekee katika Karne hii ya sayansi na Teknolojia ndio itakayowawezesha Watoto kuingia katika ushindani na Watoto wenzao Ulimwenguni katika mfumo wa kujiamini kwenye soko la Ajira.

Aliwapongeza wahitimu hao kwa kukamilisha mafunzo yao lakini wanalazimika kujipanga upya kwa Kazi iliyo mbele yao juu ya namna watakavyolihudumia Taifa katika misingi ya Uaminifu na Udadilifu kama walivyokula kiapo kwa wale wa Kada ya Uuguzi na Ukunga.

Hata hivyo amewaasa Wahitimu hao kwamba wanaweza kuingia katika hatari ya kuachwa nyuma Kielimu baada ya Miaka michache ijayo endapo hawatakuwa tayari kujielimisha Zaidi ili kwenda sambamba na mabadiliko ya sayansi na Teknolojia.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Chuo cha Elimu ya juu katika Kada ya Afya ya Zanzibar School of  Health kwa kuanzisha mafunzo ya Fani ya Madawa yaliyotanguliwa na yale ya Kukabiliana na Majanga ambayo Wataalamu wake bado ni wachache hapa Nchini.

Aliutaka Uongozi wa Chuo hicho kujipanga vyema katika muelekeo wa Malengo yake ya kuelekea kuwa Chuo Kikuu na akaahidi kwamba Serikali Kuu iko tayari kuunga mkono malengo hayo kwa vile yamejikita kuunga mkono jitihada za Serikali Kuu.

Mheshimiwa Hemed aliuhakikishia Uongozi huo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaruhusu Watendaji wake katika Taasisi mbali mbali za Umma wanaohusiana moja kwa moja na masuala ya Maafa wajiunga na Mafunzo hayo.

Alifahamisha kwamba kwa vile Maafa yanapotokea hayana taarifa lazima Taifa lijipange kwa lengo la kuacha tabia ya kutegemea Wafadhili au Wataalamu wa Kigeni pale yanapotokea.

Akigusia suala la udhalilishaji wa kijinsia unaowakumba Zaidi Wanawake na Watoto wadogo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema umefika wakati Watu lazima waachane na muhali kwa vile hakutapatikana hatia bila ya kuwepo ushahidi.

Alieleza kwamba kwa kuwa maisha ya Watoto hivi sasa yako hatarini upo umuhimu wa kuanzishwa kwa Mahakama Maalum ya watuhumiwa wa Udhalilishaji ambao kwa sasa umekuwa ukihusisha pia baadhi ya Viongozi wenye dhamana kubwa katika Jamii.

“ Inachafua kuona baadhi ya hata Mawakili katika maeneo yetu tofauti wamekuwa na tabia ya kuwatetea Watu wanaohusika na vitendo vya udhalilishaji bila ya aibu wakijisahau kuwa wao ni miongoni mwa Jamii iliyowazunguuka”. Alisema Mh. Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alionya kwamba pale Serikali Kuu itakapogundua  uwepo wa Kiongozi anayejihusisha na tabia hiyo mbaya ya udhalilishaji  haitasita kumuwajibisha mara moja.

Mapema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chuo cha Zanzibar School of Health Bwana Ali Saleh alisema ndoto ya Zanzibar katika uimarishaji wa Elimu inachipua kutokana na Sekta Binafsi kujitokeza katika kulea Maeneo ya Taaluma.

Bwana Ali Saleh alieleza kwamba ipo nafasi kubwa ya ongezeko la Ajira ya Vijana kupitia Sekta Binafsi katika harakati zake za kushirikiana na Serikali katika kupambana na uhaba wa ajira  licha ya kwamba hivi sasa imeelemea zaidi katika masuala ya Utalii.

Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Zanzibar Schoo of Health alifahamisha kuwa Sekta ya Taaluma kwa sababu ina mchango mkubwa wa kusaidiana na Serikali katika kufinyanga Vijana upo umuhimu kwa Serikali Kuu kuangalia upya masuala ya Kodi kwa zile Taasisi Binafsi zilizokwisha jikubalisha kufanyakazi pamoja na Serikali.

Akimkaribisha Mgeni rasmi katika Mahafali hayo ya Nane ya School of Health Waziri wa Eimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar Mh. Simai Mohamed Said alisema kiapo walichokula Wahitimu hao hasa wale wa Fani ya Uuguzi na Ukunga kinapaswa kuwa Dira ya kufanikisha wajibu wao katika kuhudumia Wananchi.

Mheshimiwa Simai ameupongeza Uongoziwa Chuo hicho cha Afya Kwamchina Mwanzo kwa uharaka wake wa kuwafinyanga Vijana unaokwenda sambamba na kasi ya sasa ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane katika kuhudumia Jamii.

Waziri wa Eimu na Mafunzo ya  Amali Zanzibar anayekaimu pia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii aliuthibitishia Uongozi wa Chuo hicho kwamba Serikali itajaribu kuangalia uwezekano wa kutafuta njia itakayopekea kupunguza Kodi kwa Sekta Binafsi za Taaluma.

 Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top