Na Jumbe Ismailly-Ikungi
WAKAZI wa kata ya Dung’unyi,wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida wamelazimika kutembea umbali wa kilomita kati ya kumi hadi 18 kufika katika Hospitali ya Misheni ya Makiungu,tarafa ya Mungaa,kituo cha afya cha Ikungi na Hospitali ya Misheni ya Puma,kutokana na zahanati hiyo kutokuwa na mtaalamu wa maabara pamoja na jengo la kufanyiakazi za vipimo kwa zaidi ya miaka kumi na miwili sasa.

Mganga wa zahanati ya kata ya Dung’unyi,Gabrieli Pyuza aliyasema hayo katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hizi aliyetembelea katika zahanati hiyo kutaka kufahamu ni sababu zipi zinazochangia wagonjwa kutopatiwa vipimo katika zahanati hiyo licha ya kuwepo kwa darubini kwa kipindi kirefu sasa.

Aidha mganga huyo mfawidhi alisema baada ya kamati ya maendeleo ya kata hiyo kubaini kero hiyo kwa wagonjwa wanaokwenda kufuata huduma katika zahanati hiyo ilikaa na kuazimia kwamba kila kijiji kifyatue tofali mia sita ili ujenzi wa chumba cha maabara uweze kuanza.

Kwa mujibu wa Pyuza shughuli za kufyatua tofali hizo unatarajiwa kuanza mapema mwezi may,mwaka huu mara tu mvua za masika zitakapopungua kunyesha.

Hata hivyo Pyuza alibainisha kwamba pamoja na ujenzi wa maabara,vile vile wataongeza vyumba viwili vya kupumzishia wagonjwa waliozidiwa na wanaojifungua na ambao watalazimika kukaa kituoni hapo kwa uangalizi wa mama na mtoto kwa muda wa saa 24 kuanzia mama mjamzito alipojifungua.

Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko ya wananchi wa kata ya Dung’unyi,Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Mohamedi Nkya licha ya kukiri darubini hiyo kutofanyakazi kwa zaidi ya miaka kumi,lakini alisema kinachochangia ni ukosefu wa wataalamu wa maabara unaoikabili Halmashauri hiyo.

Aidha Nkya hata hivyo aliweka bayana kwamba ili kukabiliana na tatizo hilo hivi karibuni Halmashauri hiyo imepokea wataalamu watatu wa maabara,ila bado hawajapangiwa vituo vya kazi kutokana na wataalamu hao kusubiri vyeti vyao vitakavyowatambulisha kuwa wana ujuzi wa fani hiyo.

“Ni kweli Halmashauri ya Ikungi haina wataalamu wa maabara kwa muda mrefu sana sasa ila hivi karibuni Halmashauri imepokea wataalamu watatu wa maabara ambao mpaka sasa bado sijawapangia vituo kwani bado wanasubiri vyeti vyao vitakavyowatambulisha kuwa wana sifa za kufanyakazi hiyo”alifafanua mkurugenzi huyo.

Katika hatua nyingine mkuu wa wilaya ya Mkalama, Christopher Ngubiagai ametoa muda wa siku saba kwa afisa mtendaji wa kata ya Iguguno kumpatia majina ya watoto wote waliochaguliwa kuendelea na masomo ya kidato cha kwanza mwaka huu watakaokuwa bado hawajaenda shule.

Mkuu huyo wa wilaya alitoa agizo hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Iguguno,tarafa ya Kinyangiri,wilayani hapa baada ya kupokea taarifa ya afisa mtendaji huyo kuwa mpaka sasa bado kuna wanafunzi 33 ambao bado hawajaripoti shuleni kuanza masomo yao.

Kwa mujibu wa Ngubiagai iwapo serikali imeshaanza kutoa elimu bure haoni ni sababu gani wazazi na walezi wa wanafunzi hao washindwe kuwapeleka watoto wao kuanza shule na kuonya kwamba baada ya muda huo kumalizika hatasita kuanza kutumbua majipu kwa wazazi watakaopuuzia agizo lake hilo.

0 comments:

 
Top