Na Jumbe Ismailly-Ikungi 
MUUGUZI wa zahanati ya kata ya Dung’unyi,tarafa ya Ikungi,amesema baadhi ya wanaume wa kata hiyo wamekuwa wakiwazuia wake zao kujiunga na huduma za uzazi wa mpango kutokana na kile wanachodai kwamba watajiingiza katika vitendo vya kihuni.

Muuguzi huyo wa zahanati,Evaline Mdee alisema licha ya imani potofu hizo walizonazo wanaume hao,vile vile waumini wa madhehebu ya Romani Catholic hukataza pia waumini wake kujiunga na huduma za uzazi wa mpango.

Kutokana na changamoto hizo,Mdee aliweka wazi kwamba kumechangia pia idadi ya wanawake wanaotumia huduma za mpango huo kuwa wachache mwaka hadi mwaka.

Kwa mujibu wa muuguzi huyo wa zahanati kati ya wanawake wenye umri wa miaka 14 hadi 45 wanaotumia huduma za uzazi wa mpango katika kata hiyo ni 1,672.

Hata hivyo Mdee alifafanua pia kuwa katika kipindi cha mwaka jana wanawake waliofunga kizazi ni 33 kati ya wanawake 548 waliojiunga na mpango huo mwaka 2015.

Akifafanua zaidi muuguzi huyo alisema kwamba kwa mwezi julai,mwaka jana wanawake 14 walifunga kizazi,wakati mwezi sept.ni wanawake 12 na mwezi wa kumi wanawake saba walifunga kizazi.

Muuguzi huyo wa zahanati hata hivyo alitumia fursa hiyo kuwatahadharisha wanawake wajawazito kujenga utamaduni wa kutekeleza ushauri wanaopewa na wataalamu wa afya kila inapobidi kufanya hivyo.

“Ni ukweli usiopingika kuwa bado tuna kazi ngumu sana ya kuendelea kutoa elimu kwa akina mama wajawazito wanapokuwa katika hali hiyo kwani idadi kubwa hupuuzia ushauri wanaopatiwa na wataalamu wa kwenda kusubiri karibu na hospitali kubwa kuanzia mimba ya kwanza hadi ya tano”alisisitiza Mdee.

Wakati huo huo wilaya ya Mkalama inakabiliwa na upungufu wa madawati 6,600 yanayohitajika kutengenezwa haraka iwezekanavyo kwa kupitia taratibu zitakazowekwa na kamati za shule kwa kushirikiana na uongozi wa shule husika.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Iguguno,tarafa ya Kinyangiri kwenye mkutano wa hadhara,mkuu wa wilaya hiyo,Christopher Ngubiagai alisisitiza kuwa kamati za shule pamoja na uongozi wa shule hawana budi kuangalia namna nzuri ya upatikanaji wa madawati hayo yanayohitajika.

Alibainisha Ngubiagai kwamba kumekuwepo tafsiri potofu kwa baadhi ya watu kuwa dhana ya elimu bure inalenga kumtoa kabisa mzazi katika kuchangia chochote,dhana ambayo haina ukweli wowote kwani wenye shule hizo ni wananchi,hivyo hawana budi kushirikiana na mamlaka husika kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa madawati hayo.

“Serikali imetoa miezi sita kwa kila wilaya kuhakikisha upungufu huo wa madawati unakwisha kabisa”alisisitiza mkuu wa wilaya huyo.

0 comments:

 
Top