Eka Mia 150 za miwa iliyopea zilizotiwa moto na watu wasiojuilikana katika eneo la kusini Magharibi ya Mashamba ya Miwa ya Kiwanda cha Sukari Mahonda zinakadiriwa kuleta hasara ya Dola za Kimarekani Laki 947,475.72 sawa na shilingi za Kitanzania Bilioni 1,832,242,500.00/-.

Moto huo ulioshambulia mashamba hayo jana majira ya saa sita mchana ulizimwa kwa ushirikiano kati ya wapiganaji wa Kikosi cha Zima moto na Uokozi Zanzibar, JKU, Wafanyakazi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda pamoja na Wananchi na kufanikiwa kuudhibiti mnamo majira ya saa Tisa Jioni.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alifika katika eneo hilo la maafa na kujionea hali halisi ya hasara iliyopatikana ambapo Meneja wa Mradi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda Bwana Tushar Mehta alisema eneo hilo la Eka 150 lililotiwa moto pekee lilikuwa na uwezo wa kuzalisha Sukari Tani Mia 750 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.5.

Bwana Tushar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho umesikitishwa na kitendo cha watu waliofanya hujuma hiyo licha ya nia njema ya Kiwanda hicho kuwekeza mradi huo wenye lengo la kuongeza Mapato kwa Serikali sambamba na kuongeza fursa za ajira kwa wakaazi wa maeneo jirani yanayokizunguuka Kiwand hicho.

Hata hivyo Bwana Tushar alimuhakikishia Balozi Seif kwamba Uongozi wa Kiwanda hicho bado umeonyesha nia ya kuongeza uzalishaji wa bidhaa ya sukari kwa kutoa mapendekezo ya kupatiwa mashamba zaidi ya kilimo cha miwa katika Maeneo ya Bumbwi Sudi na Bambi.

Alisema hatua hiyo imekuja kutokana na mabadiliko makubwa ya uendeshaji wa Kiwanda cha Sukari ambapo kwa sasa kimekuwa katika harakati za matengenezo ya kuwekewa mashine kubwa zitakazokuwa na uwezo mkubwa zaidi wa uzalishaji wa Sukari.

Akielezea masikitiko yake kutokana na kitendo cha hujuma ya moto katika shamba hilo la miwa Mahonda Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema huo ni uharibifu mbaya ambao hauitakii mema Nchi hii.

Balozi Seif alisema kitendo hicho cha uhalifu kinachopaswa kulaaniwa vikali na uuma kimeleta sura mbaya na kuisababishia ukosefu wa mapato Serikali Kuu iliyoamua kukaribisha uwekezaji wa Viwanda hapa Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba Uongozi wa Kiwanda cha Sukari Mahonda kutovunjika moyo kutokana na kitendo hicho na kuahidi kwamba Serikali kupitia vyombo vyake vya Dola inaendelea na uchunguzi kumbaini Mtu au kikundi kilichohusika na vitendo hicho na kufikishwa kwenye vyombo vya Sheria.

Hata hivyo Balozi Seif alifahamisha kwamba Serikali Kuu itajitahidi kuendelea kuuelimisha Wananchi juu ya umuhimu wa uwekezaji vitenga uchumi nchini wenye lengo la kuimarisha ustawi wa Jamii.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top