Na Jumbe Ismailly-Igunga

Wakati serikali ya awamu ya tano ikiendelea kuziba mianya ya upotevu wa fedha za umma pamoja na wananchi nchini,Meneja wa Mamlaka ya maji safi na maji taka(IGUWASA) wilayani Igunga,Mkoani Tabora,Raphael Merumba anakabiliwa na tuhuma za kununua chombo cha kwenye tenki la maji katika chujio la maji ambalo ni kichakavu,lililoko Bulenya,wilayani hapa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa majina yao gazetini,baadhi ya watumishi wa idara hiyo walisema kwamba kulikuwa kumejitokeza kuharibika baadhi ya miundombinu katika matenki ya maji yanayosafirisha maji kutoka bwawa la Bulenya hadi mjini Igunga.

Watumishi hao hata hivyo walidai kuwa chombo kilichoharibika kinacchofahamika kwa jina la foot valve ambahco husafirisha maji bila kupitisha uchafu na kwamba baada ya kuharibika,ndipo meneja huyo wakati akiwa Mkoani Mwanza kwa shughuli zake binafsi,aliamua kwenda kununua kifaa hicho katika maduka ya wafanyabiashara kwa bei ya shilingi 950,000/= bila kufuata taratibu za manunuzi.

Hata hivyo wananchi hao walibainisha kuwa baada ya kuifikisha foot valve hiyo na walipoifunga ilishindikana huku ikionekana ilishatumika na kwa sasa imepulizwa rangi,hali ambayo mafundi hao walilazimika kuanza kuitengeneza foot valve ile iliyokuwa ya zamani na kufanikisha kurejesha upatikanaji wa maji katika mji wa Igunga.

“Sisi kama watumishi ametushangaza sana meneja huyo kwani fedha hizo alizolipwa kwa foot valve aliyonunua itakuwa ameiibia serikali kwa kuwa haikufanya kazi na haifai kwani imepuliziwa rangi tu na ndio maana hakutushirikisha ili kujua kwamba inatakiwa foot valve nyingine” walisisitiza.

Hata hivyo watumishi hao walibainisha kuwa unahitajika uchunguzi wa kina kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kujua kama kuna ukweli wowote ule wa kama taratibu za manunuzi zilifuatwa kwa mujibu wa sheria.

Kufuatia tuhuma hiyo,gazeti hili lilimtafuta Meneja,Raphael Merumba ili aweze kuzungumzia juu ya tuhuma anayolalamikiwa,ambaye alikiri foot valve aliyonunua haikuweza kutumika kama ilivyokusudiwa.

“Ni kweli foot valve hiyo niliinunua mimi kwa thamani ya shilingi 950,000/=lakini nilipoifikisha kwa mafundi walipoifunga iligoma kwa kuwa matundu yalikuwa mapana na hivi sasa tayari tumeipeleka kwa fundi ili kuweza kuifanyia tena matengenezo” alifafanua Merumba.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya maji wilaya ya Igunga,Costa Olomi alidai kwamba yeye binafsi alipata taarifa kuwa foot valve imeharibika na hivyo mafundi walifanya mawasiliano ili kuagiza kutoka bohari ya vifaa Dar es salaam kwa bei ya shilingi laki tano.

Aidha Olomi alifafanua pia kuwa kilichomshangaza ni kusikia kuwa meneja wa mamlaka ya maji (IGUWASA) alinunua foot valve hiyo kutoka Mkoni Mwanza kwa thamani ya shilingi 9,50,000/= na kwamba walipojaribu kuifunga iligoma.

0 comments:

 
Top