Na,Jumbe Ismailly-Itigi 
HALMASHAURI ya wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida imetumia zaidi ya shilingi milioni 99 kuwalipa mishahara maafisa watendaji wa vijiji walioajiriwa katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2015/2016 ambao mpaka sasa bado hawajapangiwa vituo vya kazi.

Kiasi hicho cha fedha kimetumika kuwalipa watendaji hao mishahara ya ngazi ya TGS B ya shilingi 435,000/= kila mwezi kwa maafisa watendaji wa vijiji 38 walioajairiwa mwezi juni,mwaka huu na kutakiwa kupangiwa vituo vya kazi na kuanza kufanyakazi kuanzia julai,mwaka huu.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili na kuthibitishwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Huduma za jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Bwana Ally Minja umebaini kuwa juni,mwaka huu Halmashauri ya Manyoni iliajiri maafisa watendaji wa vijiji 38 licha ya kutopangiwa vituo vya kazi,lakini wameendelea kulipwa mishahara yao kwa ngazi ya TGS B ya shilingi 435,000/= kwa kila mmoja.

Hata hivyo Bwana Minja ambaye kwa sasa ni mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi aliweka bayana kwamba katika mkutano wake wa kwanza wa uzinduzi wa Halmashauri hiyo,baraza hilo lilipendekeza maafisa watendaji wa vijiji hao 38 wapangiwe vituo vya kazi ili waweze kupunguza kero zinazowakabili wananchi hivi sasa kwa kutokuwa na watumishi wa kada hiyo.

Akitoa wito huo kwenye mkutano wa kwanza wa uzinduzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo uliofanyika kwenye ukumbi wa Social mjini Itigi,Bi Minja alifafanua kwamba kabla Halmashauri ya wilaya ya Manyoni haijatenganishwa na Itigi kulitangazwa ajira za watendaji wa vijiji na waliajiriwa maafisa watendaji wa vijiji 38 ambao mpaka sasa bado hawajapangiwa vituo vya kazi,bila kujali kwamba mahitaaji yao ni makubwa sana kwa wananchi.

“Waheshimiwa madiwani tunao watumishi walioajiriwa wakati tukiwa bado Halmashauri moja,tunao watendaji wa vijiji wapatao 38,baadhi ya watendaji taratibu za kiutumishi ziko vizuri na mishahara wanakula,lakini hawana vituo vya kazi mpaka leo”alisisitiza Minja.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo wa kwanza wa Halmashauri hiyo, watendaji hao walipangiwa maeneo ya kazi halafu wakarudi kujificha,hivyo kutokana na hali hiyo alitumia fursa hiyo kumwagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi kuhakikisha anakaa na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni ili wakubaline kila mmoja achukue watumishi wake,ili waje haraka kuanza kazi kwenye vituo vyao.

“Kuna baadhi ya kata hapa unakuta kata nzima ukiondoa kaimu afisa mtendaji wa kijiji,watendaji wote ni wakuchukua mitaani tu na leo tunakuja kuwakabidhi dhamana kubwa hatuwezi kwenda hivyo”alisisitiza mwenyekiti huyo huku akionyesha kukerwa na mkurugenzi wa Manyoni kutowapangia vituo watendaji hao.

Kwa hali hiyo alimwagiza mkurugenzi mtendaji huyo kulishsughulikia suala hilo mapema ili watendaji hao wa vijiji waweze kuripoti Halmashauri ya Itigi na kupangiwa vituo vya kazi haraka iwezdekanavyo.

“Hivyo mkurugenzi tunakuagiza ulishughulikie suala hili mapema ili watendaji waweze kuripoti Itigi na kupanagiwa vituo vya kazi haraka iwezekaanavyo,kaeni pamoja mpange watendaji na wala usikubali kuambiwa kuwa watendaji watapanga wao peke yao haiwezekani na ninyi mshiriki katika kikao hicho”alifafanua Minja.

Hata hivyo Minja libainiha kwamba kwa kuwa mfumo umekaa vizuri haoni sababu yeyote ya kuwachelewesha watendaji hao kuwapangia vituo na kwambaa iwapo Halmashauri ya Manyoni bado kuna kitu wanasubiri,basi hawana budi kuwapatia watendaji 19 wa Itigi ili waweze kupangiwa vituo.

Alipotakiwa kuzungumzia kwa njia ya simu sababu za kutowapangia maafisa watendaji wa vijiji hao vituo huku akiendelea kuwalipa mishahara bila kufanyakazi,mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Supeet Roine Mseya,simu yake haikuwa kipatikana.

0 comments:

 
Top