Na,Jumbe Ismailly-Igunga

BALOZI, katika ya mtaa wa stoo,wilayani Igunga,Mkoani Tabora Nazaeli Mkonge ( 74 ) amekutwa na mwenyekiti wa serikali ya mtaa akikusanya vitambulisho vya kupigia kura na kukamatwa.

Mwenyekiti wa mtaa wa Stoo,Joseph Njile Michaeli akizungumza na waandishi wa Habari mbele ya wananchi waliohudhuria kushuhudia tukio hilo muda mfupi baada ya kukamatwa kwa mjumbe huyo wa nyumba kumi,alisema kuwa mafanikio ya kukamatwa kwa kiongozi huyo wa CCM, yametokana na ushirikiano na wananchi baada ya kuchoshwa kuombwa vitambulisho vya kupigia kura kutoka kwa baadhi ya mabalozi wao.

Hata hivyo alisema Michaeli kuwa tangu zoezi la kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura kwisha katika wilaya ya Igunga,wananchi wameshangazwa kuanza tena kuombwa vitambulisho vyao kwa kuambiwa kwamba vinaenda kufanyiwa uthibitisho wa namba zake zilizoko kwenye vitambulisho hivyo.

Mwenyekiti huyo hata hivyo alibainisha kuwa kutokana na hali hiyo ya malalamiko toka kwa wananchi wake kuwa mengi, alilazimika kufanya msako na ndipo julai,04,mwaka huu saa mbili asubuhi,walifanikiwa kumkamata Nazaeli Mkonge akiwa tayari amekusanya vitambulisho vinne alivyokuwanavyo kwenye mfuko wake.

Aidha alifafanua kuwa baada ya kukamatwa kwa kigogo huyo wa CCM,alikiri kuhusika na zoezi zima la kukusanya vitambulisho kwa wananchi na kudai kwamba yeye alitumwa na kiongozi wake ambaye ni mwenyekiti wa mabalozi kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyetambulika kwa jina la Isaya Sombe,mkazi wa mtaa wa stoo.

Kwa mujibu wa Mkonge kazi kubwa aliyokuwa akifanya yeye ni kuandika namba za vitambulisho na alipomaliza alikuwa akiwarudishia wananchi vitambulisho vyao.

Hata hivyo wananchi waliochukuliwa vitambulisho vyao na balozi huyo ni pamoja na Sulile Jahulula,mwenye namba 10039523270,Joyce Mabula mwenye namba 100397524110, Joyce Kandu mwenye namba 100397525567 na Winga Luhende mwenye namba 100397525400.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti,wananchi hao walisema wao walilazimika kumpa balozi huyo vitambulisho vyao hivyo kwa kuwa aliwaambia vinaenda kuorodheshwa namba zake.

Naye mwenyekiti wa mabalozi,Isaya Sombe alikiri kumtuma balozi wake kuorodhesha namba za vitambulisho hivyo kwa kile alichodai ni agizo la chama cha mapinduzi ( CCM ) wilaya ya Igunga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Igunga,Costa Olomi alikanusha taarifa kwamba Chama kilitoa agizo hilo la kukusanya vitambulisho, bali kiliwaagiza mabalozi wake kuwatembelea wanachama wa chama hicho na kuorodhesha namba za kadi za wanachama ili kujua idadi yao na siyo kukusanya vitambulisho vya kupigia kura.

Hata hivyo balozi huyo alifikishwa katika kituo cha polisi cha wilaya na mwenyekiti wa serikali ya mtaa akiwa na vitambilisho vyake vinne ambapo alihojiwa na jeshi la polisi kwa zaidi ya masaa manne na baadaye alipata dhamana na kuamriwa kurudi kituo cha polisi leo.

Naye Kaimu Kamanda polisi Mkoa wa Tabora,Juma Bwire alisema hajapokea taarifa yeyote kuhusiana na suala hilo na kuahidi kulifuatilia.

0 comments:

 
Top