Na,Jumbe Ismailly-Manyoni 
MAKAZI ya walemavu na wasiojiweza ya Sukamahela,wilayani Manyoni,Mkoani Singida yalianzishwa mwaka 1974 katika Kijiji cha Sukamahela,kata na tarafa ya Kilimatinde chini ya Idara ya Ustawi wa jamii kwa dhamana ya serikali.

Makazi hayo yaliyoanzishwa mwaka 1974 yalikuwa na walemavu 148 wakiwemo wanaume 57,wanawake 51,watoto wa kike 21 na watoto wa kiume 19,na kwa sasa makazi hayo yana jumla ya walemavu 62 wakiwemo wanaume 25,wanawake 24,watoto wa kiume 2 na watoto wa kike 11.

Eneo la makazi ya watu wenye ulemavu Sukamahela lina ukubwa wa hekta 80 ambalo linatumika kwa makazi na kilimo kwa walemavu na watumishi wanaohudumia makazi haya.

Tatizo la ombaomba katika wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida linaonekana kuwa sugu kutokana na viongozi wa ngazi zote kushindwa kutoa ushawishi kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili waweze kuachana na tabia hiyo.

Sababu za ombaomba hao kuendelea kuwepo katika wilaya hiyo ni pamoja na ugumu wa maisha,uzee,ulemavu,kutopenda kufanyakazi na starehe zisizokuwa za lazima.

Tabia hiyo ya watu kuwa ombaomba imejengeka miongoni mwa jamii kutokana na sababu moja au nyingine ikiwemo tabia ya mazoea iliyopo kwa baadhi ya watu hao kwa kuona kuwa wana haki ya kuomba na kusaidiwa wanachohitaji.

Mkuu wa wilaya ya Manyoni,Mkoani Singida,Bi Fatma Hassani Toufiq katika makala hii anaweka mikakati ya kuwaondoa watu wanaoomba kandokando ya barabara kuu ya Dodoma manyoni kwa kufanya operesheni kabambe ya kuhakikisha wanawaondoa watu hao wanaoiabisha serikali ya wilaya hiyo na taifa kwa ujumla,licha ya kuwa na ndugu,jamaa na marafiki wenye uwezo kabisa wa kuwasaidia.

“Haya ndugu mwandishi wa habari ni kweli kwamba hilo tatizo lipo kwenye eneo hilo la Kijiji cha Sukamahela pale pamoja na sehemu kidogo ya Kijiji cha Mbwasa,lakini tatizo kubwa ni kwamba wale ombaomba ni kweli wapo na mimi nimefuatilia sana nikaambiwa wapo kwa muda mrefu sana”alifafanua mkuu wa wilaya huyo.

Anasema inasemakana kwamba kati ya mwaka 1999 na 2006 imeshafanyika operesheni kubwa sana wakati alipokuwa mkuu wa wilaya hiyo,marehemu Ernesti Masima na hali hiyo ilipungua kwa wakati huo.

Lakini anasema kadri muda ulivyokuwa ukienda na walipoona hakuna hatua zozote zile zinazochukuliwa,hivi sasa wanazidi kuongezeka siku hadi siku.Anasema na yeye akiwa kama mkuu wa wilaya hiyo tatizo hilo ameshalibaini.

Anafafanua pia kwamba pamoja na kwamba katika Kijiji cha Sukamahela kuna kituo cha watu wasiojiweza cha Sukamahela,lakini wanaokaa pale kweli ni wale watu wasiojiweza na wenye ulemavu mbali mbali.

“Hawa ambao wapo barabarani wengi wao wanatoka katika vijiji vya jirani ambavyo ni pamoja na Kijiji cha Mbwasa na Sukamahela na kwa taarifa ambazo mimi nimezipata baada ya kufuatilia nimeambiwa kwamba kuna wengine ambao wana familia zao”alizizitiza Toufiq.

Kwa hiyo anasema na wengine ni watu ambao wana nafasi zao,ni watu ambao wana watoto wao na kwa fununu zilizopo ni kwamba kuna baadhi yao huwa wanasema kabisa siku za jumapili wanakwenda kwanza kwenye ibada halafu baada ya hapo ndipo wanakwenda barabarani kuomba.

Anasema inawezekana hiyo ndiyo huluka yao watanisamehe sana wenyeji wa maeneo ya kanda ya kati,mikoa ya Dodoma na Singida na inafahamika kabisa idadi kubwa ya ombaomba inatoka katika maeneo hayo.

Lakini anasema kwamba hali hiyo imekuwa ikijitokeza kutokana na hali ya watu kutopenda kujituma kufanyakazi.

Anafafanua mkuu huyo wa wilaya kwamba kwanza kama wilaya wanajiandaa kufanya operesheni ya kuwaondoa kwa sababu pale wanapokaa na kuombaomba ni aibu kubwa kwa wilaya,ni aibu kwa taifa na kwa serikali kwa ujumla kwamba inaonekana wale watu pale hawana watu wa kuwaangalia.

Sambamba na hilo lakini anasema na hilo eti wao wanategemea kwamba serikali ndiyo iwahudumie,nadhani watu wanashindwa kuelewa serikali kwamba eti kila kitu kwamba mtu hata chakula chake,au mtu kijana kumlea mzazi wake ni kazi ya serikali.

“Lakini sambamba na hilo eti wao wanategemea kwamba serikali ndiyo iwahudumie,nadhani watu wanashindwa kuelewa serikali kwamba eti kila kitu kwamba mtu hata chakula chake au mtu kijana kumlea mzazi wake,yaani mimi mzazi wangu serikali inisaidie kumlea kwa sababu mtu akishakuwa mzee siinamaana kwamba vijana wao wanatakiwa wawalee “?alihoji Bi Toufiq.

Kwa hiyo nachoweza kusema ni kwamba serikali ya wilaya tumejiandaa tumefanya utaratibu wa kuhakikisha kunafanyika tena operesheni nyingine ili kuhakikisha kwamba wale watu kwa kweli lile ni chukizo pale.

“Kwa sababu hapa katikati kama unavyofahamu tulikuwa bado tuna zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa lakini naamini kabisa kwamba kabla ya machi 20,mwaka huu zoezi hili litakuwa limeashaanza na ni lazima twende tukabaini zile kaya zote za wale ombaomba wanaokaa pale barabarani kwa ajili ya kuombaomba”anafafanua zaidi

Anasema kati ya ombaomba hao wanaokaa barabarani wapo wa aina nyingi ambao wengine ni wazee,wengine ni watu wenye nguvu zao,lakini nachoweza kusema labda ni hulka na wengine wamezoea hiyo tabia ya kuomba ili waweze kuunganishwa na familia zao ili waweze kuwahudumia.

Fredrick E.Mboya ni afisa Mfawidhi Makazi ya Sukamahela kwa upande wake anaelezea shughuli zinazofanywa na kituo hicho,mafanikio pamoja na changamoto zinazokikabili na kuwasibu wazee wanaoishi katika kambi hiyo.

Makazi ya walemavu na wasiojiweza cha Sukamahela,wilayani Manyoni,Mkoani Singida yalianzishwa mwaka 1974 katika Kijiji cha Sukamahela,kata na tarafa ya Kilimatinde chini ya Idara ya Ustawi wa jamii kwa dhamana ya serikali.

Makazi hayo yaliyoanzishwa mwaka 1974 yalikuwa na walemavu 148 wakiwemo wanaume 57,wanawake 51,watoto wa kike 21 na watoto wa kiume 19,na kwa sasa makazi hayo yana jumla ya walemavu 62 wakiwemo wanaume 25,wanawake 24,watoto wa kiume 2 na watoto wa kike 11.

Eneo la makazi ya watu wenye ulemavu Sukamahela lina ukubwa wa hekta 80 ambalo linatumika kwa makazi na kilimo kwa walemavu na watumishi wanaohudumia makazi haya.

Makazi haya yana huduma za nyumba,zahanati,kituo cha kulea watoto wadogo mchana(DCC),watoto walemavu wanaosoma shule ya msingi,huduma ya maji na watumishi.

Anasema kituo hicho kina nyumba 54 ambazo kati ya hizo,52 ndizo wanazoishi watu wenye ulemavu pamoja na watumishi wanaohudumia makazi hayo.Nyumba moja inatumika kama darasa la kulelea watoto wadogo na nyumba iliyobakia inatumika kama ofisi ya watumishi wa kituo.

Anasema afisa huyo kuwa katika kituo hicho kuna zahanati ya Kijiji cha Sukamahela inayohudumia watu wenye ulemavu pamoja na wananchi walio karibu na makazi haya.Huduma zinazotolewa na zahanati hii ni huduma ya mama na mtoto,huduma ya wagonjwa wa nje (OPD) na huduma ya uzazi.

Aidha Mboya anafafanua kwamba kuna kituo cha kulelea watoto mchana ili kuwapunguzia mzigo wazazi ili waweze kufanya shughuli za kiuchumi.Kituo hiki ni mali ya serikali,kituo hiki kina mtumishi mmoja anayetoa huduma katika kituo hiki.

Anasema kituo hiki kinahitaji kuongezewa mtumishi kwani inakuwa vigumu kuendelea na huduma pindi mtumishi aliyepo anapokuwa na matatizo na kwamba idadi ya watoto waliopo kituoni ni wanaume 12 na wanawake 18 na hivyo kukifanya kituo hiki kuwa na jumla ya watoto 30.

Hata hivyo afisa huyo mfawidhi wa makazi ya walemavu Sukamahela anasema kuna watoto sita wa kike wenye ulemavu wanaosoma katika shule ya msingi.

Kuhusu huduma za maji safi na salama kituoni hapa,anasema makazi ya watu wenye ulemavu cha Sukamahela yanapata maji safi na salama kutoka katika kisima (Wind mill) kilichochimbwa na wamisionari wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu ambao wana makazi yao jirani na kituo hiki.

Aidha anasema huduma hii ya maji safi na salama haikidhi mahitaji ya makazi haya na ongezeko la watu na mahitaji.

Akizungumzia ikama ya watumishi katika kituo hicho,Mboya anasema kwamba makazi hayo yana jumla ya watumishi sita,ambao kati yao watumishi watatu ni wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni na watumishi watatu ni wa idara ya Ustawi wa jamii.

Anasema kwamba kutokana na idadi hiyo ya watumishi hivyo kuna upungufu wa watumishi wa idara yaa Ustawi wa jamii 11.

“Kuna upungufu wa watumishi wa idara ya Ustawi wa jamii kama ilivyoonyeshwa kwenye jedwali hapa chini ambako kwa kada ya Afisa Ustawi wa jamii mahitaji ni mmoja na waliopo ni mmoja,muhudumu wa afya mahitaji ni wanne na waliopo ni mmoja,wapishi mahitaji ni watatu hakuna hata mmoja,mlinzi mahitaji ni watatu hakuna hata mmoja na Walezi wa watoto mahitaji ni watatu waliopo ni mmoja”alifafanua Mboya.

Akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika kituo hicho,afisa huyo anasema tangu kituo hicho kianze kimekuwa na mafanikio mbali mbali.Ameyataja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na ukarabati wa nyumba 20 kati ya 54 sawa na asilimia 37 ya zilizopo katika makazi haya,nyumba 31 na matundu ya vyoo zinatakiwa kufanyiwa ukarabati mkubwa.

Mafanikio mengine kwa mujibu wa Mboya ni ujenzi wa matundu ya vyoo mapya saba umekamilika na vimeanza kutumika na kuwepo kwa kituo cha kulelea watoto wadogo.

Kuhusu matatizo anasema kwamba kituo hicho kinakabiliwa na ukosefu wa usafiri kwa ajili ya huduma ya Makazi,hasa kwa walemavu wanapougua na kupewa rufaa ya kwenda Hospitali ya wilaya na ukosefu wa nyumba za watumishi wa makazi ya watu wenye ulemavu.

Matatizo mengine ameyataja kuwa ni ukosefu wa ofisi na samani zake kwa sasa watumishi wanatumia nyumba moja kama ofisi,ukosefu wa stoo ya kuhifadhia chakula,ukumbi wa chakula hutumika kama stoo ya chakula,kituo cha kulelea watoto kinatumia nyumba moja kama darasa kwani hakuna darasa na makazi hayana wigo hivyo kusababisha watu kupita kila mahali hivyo kuhatarisha usalama wa makazi na mali zao.

Anasema matatizo mengine ni makazi hayana huduma ya nishati ya umeme,hivyo wanaomba kuunganishiwa huduma hiyo ya nishati ya umeme kutoka njia ya umeme iendayo Kintinku,upungufu wa maji safi na salama pamoja na upungufu wa watumishi hasa kitengo cha wapishi,wahudumu wa afya na walinzi kwa hali hiyo wanaomba kuwepo na ajira kwa kupatiwa wapishi watatu,wahudumu wa afya watatu na walezi wa watoto wawili.

Kuhusu ufumbuzi wa matatizo hayo Mboya anasema kwa sasa wagonjwa wanaopata rufaa wanapatiwa usafiri na Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,kwa sasa watumishi wametengewa baadhi ya nyumba za watu wenye ulemavu kwa ajili ya makazi yao,nyumba moja imetengwa kwa ajili ya ofisi,kwa sasa ukumbi wa chakula unatumika kama stoo ya kuhifadhia chakula na nyumba moja inatumika kama darasa la kulelea watoto.

“Walemavu wa Makazi ya Sukamahela,tarafa ya Kilimatinde,wilayani Manyoni wanatoa shukrani za dhati kwa watu mbali mbali waliowasaidia wakiwemo Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania,Mh,Dk.Jakaya Mrisho Kikwete,Mbunge wa jimbo la Manyoni mashariki,Mh.Kapteni John Chiligati,Shirika la Damu Azizi ya Yesu,Masister wa Mt.URUSULA,Vikundi mbalimbali vya mashirika ya dini,Chama cha Umoja wa Makanisa(CCT),Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,Shirika la mafao ya uzeeni(NSSF),Kamati ya Bunge ya huduma za jamii na serikali ya Ireland na kikundi cha vijana (TAMACAEFO) kwa misaada yao ya hali na mali”alisisitiza Mboya.

Kwa upande wake Kaimu Afisa Ustawi wa jamii Mkoa wa Singida,Bi Fatuma Malenga anasema kituo hiccho kilichoanzishwa mwaka 1994 kinategemea huduma zake kutoka sehemu mbali mbali ikiwemo serikali kuu chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii(idara ya Ustawi wa jamii).

Bi Malenga anazitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na chakula,makazi yaliyojengwa na wizara ya Afya na Ustawi wa jamii,watumishi wameajiriwa na wizara,na hupatiwa huduma zingine muhimu.

Anasema Makazi haya yanategemea pia huduma zake kutoka katika Halmashauri na kwamba huduma zinazotolewa na Halmashauri ni pamoja na huduma za afya kwa kuwapangia wataalamu wa afya kuhudumia wazee na kwamba jumla ya watumishi watatu ni wa Halmashauri ya wilaya ya Manyoni.

Huduma zingine kwa mujibu wa kaimu afisa huyo zinatoka kwa wamissionari wa Shirika la Damu Takatifu ya Yesu ambazo ni huduma za maji safi na salama kwa kuchimba kisima,chakula pale ambapo chakula kutoka serikali kuu kinapochelewa,pia wamejenga kituo cha afya pamoja na nyumba ya wahudumu wa afya na jiko.

Anasema makazi hayo yana uwezo wa kupokea watu 102 kwa kuwa kuna nyumba 51 na kila nyumba watu wawili,na kwa sasa kuna wahudumu 62 na watoto wa kike 11.

Anafafanua kwamba upatikanaji wa chakula umekuwa mgumu kwa kuwa fedha za chakula hazitolewi kwa wakati na hata wazabuni wamekuwa wakiidai Wizara kwa muda mrefu,hali ambayo inawakatisha tamaa.

Anasema kutokana na hali hiyo wakati mwingine wanapoweka oder kwa wazabuni wanakataa kwa kuwa wanadai au wanajua malipo yao yatachukua muda mrefu.Na ikitokea hali hiyo wadau wa wakazi (Shirika la Damu Takatifu ya Yesu) wamekuwa wakisaidia kuwapatia chakula wahudumiwa hao.

Bi Malenga anasema huduma za afya bado haziridhishi kutokana na upungufu wa wahudumu pamoja na upatikanaji hafifu wa dawa maalumu kwa wazee hao.

Anafafanua kwamba wazee wanahitaji wahudumu wa afya ili kuwafuatilia maendeleo yao kwa mfano kama wako kwenye dose ni wajibu wao kuhakikisha wanakunywa dawa kwa wakati muafaka.

Katika upatikanaji wa huduma ya afya anasema kwamba kuna watu binaafsi kutoka Dar-es-Salaam ambao waliandaa Bima ya Afya kwa wahudumiwa wote na huwalipia gharama za matibabu kwa kipindi cha mwaka mzima.

Anasema hali ya majengo siyo rafiki kwa kuwa baadhi ya majengo yamechakaa na yanaweza kuwadhuru,pia hali ya usafi wa majengo hayo hayaridhishi kutokana na upungufu wa watumishi,hususani wa wazee.

Vile vile anasema huduma ya malazi ya wazee hao siyo rafiki kwa mfano mwaka jana,wizara ilipeleka vitanda aina ya double deckers,hali ambayo kwa wazee ni vigumu wao kupanda juu kwenye vitanda hivyo vya double decker.

Kuhusu ushiriki wa watoa huduma afisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia walemavu wa Mkoa wa Singida anasema huduma na watoa fedha na vifaa ni hafifu kwa mfano Wizara kuamua kununua vifaa kama vile vitanda vya aina ya double decker bila kuwashirikisha au hata kumshirikisha Mkuu wa makazi na hivyo ameshauri kuwa wizara ishirikishe uongozi wa makao kabla ya kununua vifaa vya aina yeyote ile.

Hata hivyo Malenga anatoa wito kwa serikali ya Kijiji kuwa iwe na mpango wa kutoa huduma kwa wahudumiwa kwa mfano usafi wanaweza kutenga siku moja kwa wiki kwa ajili ya usafi wa mazingira,nyumba za wahudumiwa kama vile kuwafulia,kuwakata nywele,kuwakata kucha,usafi wa vyomba na kadhalika.

Vile vile anasema serikali ya Kijiji iweke mkakati wa ulinzi na usalama wa wahudumiwa na mali zao pamoja na mali za makazi.

Kwa upande wa kamati ya maendeleo ya kata (WDC),Bi Malenga anasema kamati hiyo iweke masuala ya kuwahudumia wazee na walemavu katika mipango ya kila mwaka na hasa juu ya utoaji wa elimu kwa wananhci ili waweze kutoa misaada kwa wahudumiwa mmoja mmoja au kwa ujumla wao.

Kwa Halmashauri ya wilaya kaimu afisa huyo anasema inatakiwa kutoa msaada wa haraka pale unapohitajika kwa mfano usafiri kupeleka wahudumiwa wanaopewa rufaa kwenda Hospitali ya wilaya na mahitaji mengine.

Anasema Wizara ya afya haina budi kutenga bajeti ya kutosha na fedha zitolewe kwa wakati,iweze kuajiri mtumishi zaidi kulingana na mahitaji kama vile wapishi,wahudumu wa afya na walinzi.

Anasema wizara iyapatie gari makazi hayo ili kurahisisha usafiri,ijenge stoo ya chakula kwa sasa bwalo la chakula hutumika kama stoo,inunue samani za ofisi kwa kuwa kuna upungufu wa kabati,meza pamoja na viti.

Anasema sambamba na ujenzi wa ofisi kwani kwa sasa nyumba moja ya wahudumiwa ndiyo inatumika kama ofisi ya Mfawidhi wa makazi.

Wakizungumzia sababu za kuwa ombaomba katika eneo hilo,baadhi ya wazee wanaojihusisha na tabia hiyo,Bi Asha Makambara mkazi wa Kijiji cha Sukamahela aliyewahi kuishi kwenye kambi la wazee wenye ulemavu mwaka 2013 kwa mwezi mmoja tu na kuondoka anasema kilichomfanya kuondoka kwenye kambi hiyo ni tabia ya vitendo vya kishirikina (wanalogana sana) vilivyosababisha wengi wao kupoteza maisha.

Anasema hata kama viongozi watafika kwenye kambi hiyo na kudai waonyeshwe eneo la makaburi waliyozikwa walemavu wataamini kabisa kuyaona matuta yaliyofukiwa watu hao ambao vifo vyao vilitokana na ushirikina.

“Kambini mimi nimekaa huku kwenye hingili huku Kijijini,huku Ustawi wanamaliza sana bwana,watatuchawia bwana watu wanakufa ovyo hapo kambini kwa hiyo tunaogopa kwenda huko”anasema

Hata hivyo anasema anapokuwa barabarani hapo na kuendelea na zoezi lake la ombaomba huwa anafanikiwa kupata kati ya shilingi 200 na 500 pamoja na vitu kama vile unga,mikate,sabuni,sukari na mchele.

Naye Emiria Matonya,mkazi wa Kijiji cha Sukamahela anasema amelazimika kujiingiza katika shughuli hiyo ya ombaomba baada ya kubaini kwamba serikali imekuwa ikimtenga kwa misaada mbali mbali kama vile kutoorodheshwa katika daftari la kunusuru kaya maskini kupitia mpango wa TASAF.

Wakati mwingine anasema licha ya kukaa kwa siku nzima kandokando ya barabara akiombaomba amekuwa akijikuta akiambulia patupu hata shilingi moja na siku zingine amekuwa akishinda na njaa tu.

Kwa upande wake Donald Chinoje wa Kijiji cha Sukamahela anasema licha ya serikali kuwazuia kuombaomba barabarani hapo lakini amekuwa akifanya shughuli hiyo kwa njia za ujanjaujanja tu kwa sababu ya shida zinazowakabili na hasa kwa yeye huitumia siku ya mapumziko kama jumapili baada ya kutoka kanisani ndipo anakuja kuendelea na ombaomba.

Naye Mbunge wa jimbo la Manyoni Mashariki,Kapteni Mstaafu John Chiligati anasema tatizo la huduma duni katika Makazi ya walemavu wa Sukamahela inatokana na utaratibu mbovu uliowekwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii.

Anasema mwakilishi huyo wa wananchi kwamba utaratibu uliowekwa na Wizara wa kuyahudumia Makazi hayo ya walemavu kutegemea kutoka Mkoani badala ya eneo lililopo karibu na makazi hayo,ndiyo chanzo kikuu cha walemavu hao kukabiliwa na mateso hayo yanayojitokeza kwa sasa.

Akifafanua zaidi Chiligati anasema kutokana na adha wanayoipata walemavu hao,katika ziara yao waliyofanya kutembelea makazi hayo miaka miwili iliyopita,kamati ya kudumu ya Huduma za jamii ya Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa ushauri ambao ungeweza kusaidia kupunguza na kama siyo kuondokana kabisa na tatizo lililopo kwa sasa.

Mwakilishi huyo wa wana Manyoni mashariki anasema kamati hiyo ilishauri kwamba Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iangalie uwezekano wa kusogeza huduma zake kwenye ngazi ya Halmashauri ya wilaya ya Manyoni,badala ya kusubiri kutoka Mkoa kupeleka huduma hizo katika Makazi ya wazee wanaoishi Sukamahela.

0784 596 786

0 comments:

 
Top