Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alisema kwamba utitiri wa vyuo vikuu bila ya ubora wa elimu inayotolewa ni jambo linalopelekea vyuo hivyo kutoa vijana wasiouzika kiajira katika taasisi mbali mbali za umma na hata zile za binafsi.

Alisema athari hiyo ambayo pia ni hatari kwa hatma yao ya kimaisha hapo baadaye pia inaweza kuwanyima fursa pana nay a uhakika ya kujiunga na vyuo vyengine vya elimu ya juu ndani na nje ya nchi.

Mama Asha Suleiman Iddi alisema hayo wakati wa hafla maalum ya kuagana kwa wana jumuiya ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro wa ZAMUMSA ambao wanatarajiwa kumaliza mafunzo yao mwezi Novemba mwaka huu.

Hafla hiyo ya aina yake iliyoshirikisha pia baadhi ya wahitimu wengine wa vyuo vikuu mbali mbali Nchini Tanzania ilifanyika katika ukumbi wa Zamani wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar uliopo Kikwajuni Mjini Zanzibar.

Mama Asha alisema vyuo vikuu viliopo hapa nchini hivi sasa vinatosha, lakini kinachohitajika zaidi ni kuimarishwa kwa ubora wa elimu inayotolewa kwenye vyuo hivyo.

Aliwataka wasomi wa vyuo vikuu wanaomaliza masomo yao kuweka malengo maalum ya kujiendeleza kimaisha ili kuwa tayari kukabiliana na changamoto watakazokuja pambana nazo katika maisha yao ya baadaye.

Alisema Zanzibar ni ndogo kulingana na wimbi la vijana wanaomaliza elimu ya vyuo vikuu. Hivyo akasema ni vyema wakajiandalia mazingira ya kujiunga katika vikundi vya uzalishaji ndani na nje ya vyuo ili kuwa tayari katika kukabiliana na matatizo ya kimaisha wamalizapo masomo yao.

Mama Asha alifahamisha kwamba jumuiya ya ZAMUMSA inafaa kufanya miradi ya kisomi kwa kutengeneza vitini na kuwauzia wanafunzi wa sekondari na pale inapowezekana hata kutunga vitabu vya sekondari katika masomo mbali mbali.

Katika kuunga mkono jumuiya hiyo ya wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha aliahidi kuipatia mchango wa Kompyuta, Printa na Mashine ya Fotokopi Jumuiya hiyo ili ipate nguvu zaidi za kiutendaji.

Hata hivyo Mama Asha aliwaasa na kuwatahadharisha wanafunzi hao wa elimu ya juu kujiepusha na ushawishi wa wanasiasa kwa kuwatumia kujiingiza katika matendo maovu ya uvunjifu wa amani ya Nchi.

Alisema wasomi mara nyingi ndio wanaotumiwa katika kufanya fujo na kuvuruga amani katika maeneo mbali mbali duniani kupitia mkono wa Viongozi wa kisiasa.

Akigusia suala la wanafunzi wanaoingia vyuo vikuu kulazimishwa kusomea fani wasiyoitaka, mama Asha alisema suala hilo bado linazungumzika bila ya kuleta utata au hofu yoyote ile.

Alitoa wazo kwa wana jumuiya hiyo pamoja na wasomi wengine kukutana na Uongozi wa juu wa Wizara inayoshughulikia Taaluma katika kutafuta njia muwafaka ya kulitatua tatizo hilo kwa njia sahihi isiyo na shaka.

Akisoma risala ya wanajumuiya hiyo ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma Chuo Kikuu cha Kiislamu Mkoani Morogoro { ZAMUMSA } Mwanajumuiya Saleh Haji alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo mwaka 2006 ni kuwaunganisha pamoja wanafunzi wote ili kuwa rahisi kukabiliana na changamoto wanazopambana nazo.

Saleh Haji kwa niaba ya wanajumiya wenzake wameiomba Serikali Kuu kuongeza nguvu za ziada katika uimarishaji wa maabara na Maktaba kwa skuli za Sekondari ili kuzalisha wanafunzi wa sayansi ambao hivi sasa bado idadi yao hailingani na mahitaji halisi ya upatikanaji wa wataalamu wa fani hiyo.

Aidha wanafunzi hao wa ZAMUMSA wameiomba Serikali kufanya juhudi ya kuwadhibiti wasomi wanaomaliza elimu ya juu kwa kuwajengea mazingira mazuri yatakayowapa hamu ya kuitumikia elimu yao hapa nyumbani.

Mapema Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Zanzibar wanaosoma chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro Hamad Ali alisema wanajumiya hao wameamua kujitolea kuitumikia nchi yao licha ya changamoto wanazopambana nazo.

Hamad Ali alisema wanafunzi hao wanahitaji kuitumia taaluma waliyojifunza kwa kuisaidia jamii iliyowazunguuka katika maeneo yao.

Wanafunzi wasiopungua mia 800 kutoka Zanzibar wamejiunga na chuo kikuu cha Kiislamu Morogoro katika fani mbali mbali ikiwa ni zaidi ya asilimia 47% ya wanafunzi wote chuoni hapo.

Idadi hiyo ni kubwa ikilinganishwa na vyuo vyengine vikuu hapa Tanzania inayotokana na mazingira halizi ya chuo hicho yanayolingana na utamaduni na silka za wanafunzi hao.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pilim wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top