Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuwahudumia Wananchi wake katika kuwapatia huduma muhimu na za msingi za Kijamii ikielewa fika kwamba inatekeleza Sera na ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi { CCM } ya mwaka 2010.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo hapo katika Kijiji cha Mvuleni Kidoti Wilaya ya Kaskazini “A “ wakati akikabidhi vifaa mbali mbali vya ujenzi kwa ajili ya kuufanyia matengenezo makubwa Msikiti Mkuu wa Ijumaa wa Kijiji hicho.


Balozi Seif alikabidhi vifaa hivyo ambavyo ni pamoja na Mabati,Miti na Papi za kuezekea, mbao,matofali, mawe, mchanga pamoja na saruji ikiwa ni awamu ya kwanza ya matengenezo hayo akianza kutekeleza ahadi aliyoitoa Tarehe 20 mwezi uliopita alipofanya ziara fupi kukagua maendeleo na changamoto zinazowakabili wananchi wa Kijiji hicho.

Vifaa hivyo vya ujenzi vimegharimu jumla ya shilingi za Kitanzania Milioni kumi na mbili na laki sita { 12,600,000/- }.

Balozi Seif alisema Serikali inaelewa dhiki na matatizo ya Kiuchumi na Kijamii yanayowapata wananchi katika maeneo mbali mbali nchini. Hivyo katika kukabiliana na matatizo hayo Serikali itaendelea kuhudumia kadri hali itakavyoruhusu.

Alifahamisha kwamba Serikali ina jukumu la kutoa huduma hizo ikielewa kwamba wananchi ndio washirika wakubwa wanaochangia na kulipa kodi ambapo vifaa vilivyotolewa ni miongoni mwa kodi zao wenyewe.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwatanabahisha wananchi hao kuendelea na harakati zao za kujitafutia maisha na kuweka kando propaganda wanazopelekewa na wana siasa waroho zenye muelekeo wa kuviza maendeleo yao.

Msimamizi wa matengenezo ya Msikiti huo wa Ijumaa wa Kijiji cha Mvuleni Bwana Khamis Yussuf Kombo kwa niaba ya waumini na wananchi wa kijiji hicho alimpongeza Balozi Seif kwa msimamo wake anaouchukuwa wa kusimamia harakati za kijamii hapa Nchini.

Bwana Khamis alimueleza Balozi Seif kwamba tathmini ya hivi sasa ya ujenzi wa msikiti huo hadi kukamilika kwake inatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi Milioni 25,880,000/-

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alipata fursa ya kutembelea mradi wa ujenzi wa tangi kubwa la kuhifadhia maji safi na salama liliopo katika Kijiji cha Mwanguo Bwereo.

Tangi hilo lenye uwezo wa kuhifadhi maji zaidi ya Lita milioni tatu na laki sita linatarajiwa kupokea maji kutoka katika visima sita vilivyochimbwa na mamlaka ya maji Zanzibar { zawa } katika Kijiji cha Kiashange.

Afisa wa Maji Wilaya ya Kaskazini “A “ Ndugu Dude Kidongo Amour alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Tangi hilo litakapomalizika litakuwa na uwezo wa kusambaza huduma ya maji katika Vijiji mbali mbali vilivyomo ndani ya Wilaya hiyo.

Nd. Dude alisema kazi ya usambazaji huo inatarajiwa kuanza mara baada ya wahandisi wanaosimamia mradi huo kutoka Nchini Jamuhuri ya Watu wa China kukamilisha na kukabidhi rasmi mradi huo kwa mamlaka ya maji { ZAWA } mwezi ujao.

Ujenzi wa tangi hilo na lile liliopo kiashange umegharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika { ADB }.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top