Taasisi ya Kimataifa inayojihusisha na Miundo mbinu ya Elimu, Madini, mafuta na Gesi, nishati na mawasiliano ya Planet Core kutoka Nchini India imejitolea kutaka kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha Sekta hizo.
Mwenyekiti wa Timu ya Uongozi wa Taasisi hiyo Bwana Deepak Balaji alieleza hayo wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi nyumbani kwake Mazizini nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Bwana Deepak ambae yeye na ujumbe wake yupo Tanzania kwa siku nane kuangalia fursa zilizopo ambazo Taasisi yake inaweza kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji alisema Planet Core imeshaamua kuwa mshirika na Zanzibar kwa lengo la kuimarisha uchumi na kustawisha maisha ya Wananchi wa kawaida.
Mwenyekiti huyo wa Timu ya Uongozi wa Planet Core alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Taasisi hiyo tayari imeshawekeza na kuwa mshirika mkubwa wa Elimu katika Mataifa 16 Duniani baadhi yake zikiwemo Nchi za Bara la Afrika Tanzania Bara ikiwa miongoni mwake.
“ Uwekezaji wetu umelenga katika miradi ya Mafuta, Gesi na Elimu kwa hivi sasa miradi ambayo inatekelezwa kwa ufanisi kwenye Mataifa mbali mbali Ulimwenguni “. Alieleza Bw. Deepak.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo wa Timu ya Uongozi wa Planet Core alifafanua kwamba Taasisi hiyo imefanikiwa kuwa na miradi na wataalamu wazuri wa Sekta za Maji, Nishati, Madini pamoja na Biashara za Kimataifa.
Bwana Deepak alisema kwamba miradi hiyo huanzishwa na Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Mataifa washirika kulingana na mahitaji halisi ya Mataifa hayo kwenye sekta hizo.
“ Tumeshakuwa na vituo vyetu vya huduma za miradi hiyo katika nchi za Marekani, Uingereza, India yenyewe, Mashariki ya Kati pamoja na baadhi ya Mataifa ya Bara la Afrika “. Alisema Bw. Deepak.
Alifahamisha zaidi kwamba miradi ya Elimu imepata mafanikio makubwa kwa vile mafunzoya walimu yameimarishwa kwa kutumia Teknolojia ya kisasa ya Mtandao wa Kompyuta.
Bwana Deepak Balaji alieleza kuwa uimarishaji huo wa elimu umekwenda sambamba na kuvijengea uwezo zaidi vituo vya amali ili visaidie kuzalisha ajira hasa kwa vijana wanaomaliza masomo yao.
Akiiushukuru Taasisi hiyo ya Planet Core ya Nchini India kwa uwamuzi wake wa kutoa msukumo wa kitaalamu katika mataifa machanga Duniani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uamuzi wa Taasisi hiyo unapaswa kuungwa mkono na mataifa washirika katika kustawisha jamii zao.
Balozi Seif alisifu miradi inayosimamiwa na Planet Core ambayo inaonyesha wazi kuzingatia hali ya mazingira ya sayansi na teknolojia yaliyopo hivi sasa ulimwenguni kote.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri Uongozi wa Planet Core kutayarisha mpango mkakati wa miradi ya elimu na Viwanda vidogo vidogo ambayo inaweza kuwekezwa hapa Zanzibar.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia taasisi husika zinazosimamia sekta hizo hapa Nchini itakuwa tayari kutoa ushirikiano wa kina kwa Taasisi hiyo ili kuona miradi hiyo inaanzishwa na kuleta faida hapa Nchini.
Akigusia suala la Mafuta na Gesi Balozi Seif aliueleza ujumbe huo kwamba Suala hilo hivi sasa liko katika mambo ya muungano jambo ambalo Zanzibar pekee haiwezi ikalitolea maamuzi.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Tanzania hivi sasa inaendelea na mchakato wa majadiliano ya Katiba Mpya hali ambayo suala la Mafuta kama Zanzibar ilivyopendekeza kutolewa katika Mambo ya Muungano hatma yake itajuilikana mara baada ya kukamilika kwa mchakato huo wa Katibva.
Alieleza kwamba Zanzibar inatarajia kuelekeza nguvu zake za kiuchumi hapo baadaye katika Sekta ya Mafuta na Gesi baada ya kukamilika taratibu zote za kisheria pamoja na utafiti utaobainisha uwepo wa rasilmali hiyo.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment