Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefungua milango kwa kuruhusu kila mwananchi na hasa Vijana kujituma kwa kutumia kipaji alichonacho katika kufanya kazi itakayomsaidia kuendesha maisha yake ya kila siku.

Alisema vipaji walivyonavyo baadhi ya watu kama kazi za amali pamoja na kilimo na ufugaji vinaweza kuondosha vikwazo vya wananchi hao katika kuelekea kwenye matumaini mema.

Balozi Seif alisema hayo wakati akizindua utoaji wa mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi Kisiwani Pemba huko Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ambapo shughuli kama hiyo tayari ameshaifanya kwa vikundi cha wajasiri amali wa kisiwa cha Unguja.

Vikundi 13 vya wajasiri amali hao kutoka Wilaya zote Nne za Pemba wamekabidhiwa hundi za mikopo ya fedha zenye thamani ya shilingi milioni 30,000,000/- kati ya Milioni 70,000,000/- zilizoidhinishwa na mfuko huo wa uwezeshaji wananchi Kiuchumi.

Balozi Seif alisema Serikali iliamua kuimarisha mfuko huo ukilenga Vijana, akina mama na makundi maalum ya jamii kwa kuwapatia mitaji itakayowawezesha kujiajiri ili kupunguza utegemezi.

Alifahamisha kwamba mkopo wa fedha zilizotolewa ni maalum kwa kusaidia wananchi wa kipato cha chini ambao hawana njia madhubuti za kuendesha maisha yao.

“Kila Kijana ana haki ya kuipata huduma hii. Hivyo vijana wetu tunawafungulia milango na cha msingi ni kufuata taratibu zilizowekwa na Wizara husika katika kukopa na kurejesha “. Alieleza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba wale waliosaidia kuchangia mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi waendelee na juhudi hizo ambazo ni jambo jema kwa vile huduma za mikopo hiyo itakuwa imekurubishwa kwa walengwa.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Bibi Asha Abdulla alisema uanzishwaji wa mfuko huo utawaongezea mtaji wajasiri amali ambao hushindwa kuchukuwa mikopo katika taasisi za kibenki kutokana na ukubwa wa riba.

Alisema juhudi zitaendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara inayosimamia Uwezeshaji katika kuujengea nguvu zaidi mfuko huo ili uzidi kuwahudumia wajasiri amali kwa kipindi kirefu kijacho.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi wa utoaji mikopo ya mfuko wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Wanawake na Watoto Mh. Zaiban Omar Mohamed alisema maombi 433 kutoka vikundi 40 tayari yameshapokelewa na mia 109 kati ya hayo yameshapitishwa.

Waziri Zainab alisema vikundi vinavyohitaji kukopeshwa lazima viwe na shughuli za uzalishaji unaoweza kuhimili ulipaji mkopo sambamba na kujiongezea mapato ili viweze kujiendesha kwa muda mrefu.

Vikundi 13 vya Wilaya Nne zilizomo ndani ya Kisiwa cha Pemba vimepatiwa hundi za fedha za mikopo hiyo inayohitaji kurejeshwa kwa muda utakaokubalika kati ya pande hizo mbili.

Vikundi hivyo ni Heri ya moyo mmoja, kulegea si kung’oka, tudumishe amani na juhudi zetu vilivyomo Wilaya ya Micheweni wakati vile vya Wilaya ya Wete ni pamoja na Usilolijua, tupendane na haviliki.

Vyengine ni Maendeleo, Nia safi iwepo, Pemba Sea Cliff vya Wilaya ya Chake chake wakati vile vya Wilaya ya Mkoani ni Muelekeo, Tuishi kwa usalama pamoja na walemavu.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikabidhi vifaa vya ukulima wa mwani vilivyotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohd Shein kwa ajili ya kikundi cha ukulima wa mwani cha Maneno hayasaidii kitu cha Wilaya ya Micheweni.

Dr. Shein alitoa msaada huo wa Kamba na Tai Tai wenye thamani ya shilingi Milioni 3,000,000/- kufuatia ahadi aliyopitowa kwa Kikundi hicho wakati wa ziara yake aliyoifanya katika Mkoa wa Kaskazini Pemba miezi ya hivi karibuni.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top