Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itasimamia kikamilifu katika kuona Kituo cha Afya cha Kijiji cha Vikunguni Wawi chake chake Pemba kinaanza kutoa huduma zake ifikapo Januari mwaka ujao wa 2015 ili kuwaondoshea usumbufu wa huduma za afya wananchi wa kijiji hicho.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo wakati alipokitembelea kituo hicho kilichopo pembezoni mwa skuli ya msingi ya Vikunguni ndani ya Jimbo la Wawi Mkoa wa Kusini Pemba.

Alisema kitendo cha wananchi hao hasa akina mama na watoto kufuatia huduma za afya katika kituo cha afya Gombani kinastahiki kupatiwa dawa kwa lengo la kuwapa nafasi wananchi hao waendelee na harakati zao za kimaisha.

Balozi Seif alieleza kuwa Serikali kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya chake chake, Wizara ya Afya, Mwakilishi wa Jimbo la Wawi pamoja na baadhi ya wafadhili watakaojitokeza watafanya juhudi za pamoja kukimaliza kituo hicho kinachotarajiwa kuwa cha daraja la kwanza.

“ Juhudi mlizozichukuwa katika ujenzi wa Kituo chenu mnastahidi kusaidia kwa nguvu zote na nitajaribu kumshauri Mwakilishi wenu wa Jimbo fedha atakazozipata za kuendeleza Jimbo azielekeze katika kituo hichi “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza wananchi hao kwa uamuzi wao wa kujenga kituo cha afya unaokwenda sambamba na sera ya Serikali ya ya kuwa na huduma za afya isiyopungua umbali wa kila kilomita tano.

Nao Wananchi wa Kijiji cha Vikunguni walimueleza Balozi Seif kwamba kutokana na usumbufu wanaoupata wa huduma za afya walilazimika kujenga kituo hicho ili waondokkane na tatizo hilo.

Walisema ujenzi wa kituo hicho ulioanza mapema mwaka 2002 bado unahitaji mchango wa kumalizia kwa hatua za plasta,sarujidari, pamoja na vifaa muhimu vya huduma za afya.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top