Na: Hassan Hamad (OMKR)

Wakati Chama Cha Wananchi CUF kikiingia katika uchaguzi Mkuu Taifa, Viongozi wakuu wa Chama hicho wamewataka wajumbe watakaokosa nafasi za uongozi kutobabaika, na badala yake waendelee kukijenga chama hicho.

Akizungumza katika hafla maalum ya kuagana na wajumbe wa Baraza Kuu pamoja na watendaji wengine wa ngazi mbali mbali, Katibu Mkuu wa Chama hicho Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amesema kila mwanachama ana wajibu wa msingi wa kukijenga chama bila kujali wadhifa alionao.

“Wasiorudi kwenye baraza kuu na ngazi nyengine yeyote ya uongozi bado wana mchango mkubwa wa kukijenga chama chetu ili kiweze kushika dola mwaka 2015, na jukumu hilo limo ndani ya katiba ya chama chetu”, alisisitiza Maalim Seif katika hafla hiyo iliyofanyika nyumbani kwa Mwenyekiti wa Chama hicho Prof. Ibrahim Lipumba katika eneo la Kunduchi Dar es Salaam.

Amewapongeza wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi kwa mashirikiano waliyokuwa nayo katika kipindi chote cha miezi 64, hali ambayo amesema imeleta mafanikio makubwa ndani ya chama hicho.

Maalim Seif amesema ndani ya kipindi hicho Chama pia kilikabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo hata hivyo kwa kutumia busara na hekima za viongozi waliweza kuzitatua.

Amewasisitiza wajumbe watakaochaguwa kuendeleza umoja na mshikamano uliopo, ili kuweza kufikia malengo waliyojiwekea ya kukamata hatamu za dola katika uchaguzi mkuu ujao.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba ambaye anakabiliwa na upinzani katika uchaguzi huo, ameahidi kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo, na iwapo atashindwa ataendelea kukiunga mkono chama hicho kwa kutoa kila msaada unaostahiki kwa maendeleo ya chama.

“Mimi nikiangushwa katika uchaguzi nitaendelea kuwa mwanachama na kutoa mchango wangu wote kwani suala hili la kugombea nafasi ni haki ya kikatiba kwa wanachama wote” alieleza Prof. Lipumba na kuongeza.

“Nilikuwa mwanachama wa kawaida kwa kipindi kiferu ndipo ikafika wakati chama kikaniteua kugombea na kuchaguliwa Mwenyekiti hadi leo, kwa hivyo haki hii anaweza kuwa nayo mwanachama yeyote”, aliweka bayana Prof. Lipumba.

Jumla ya wagombea watatu wamejitokeza kugombea nafasi ya Uenyekiti Taifa akiwemo Mwenyekiti wa sasa Prof. Ibrahim Haruna Lipumba.

Wagombea wengine wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti Taifa ni M’bezi Adam Bakar kutoka Temeke Dar es Salaam na Chifu Lutalosa Yemba kutoka Shinyanga.

Nafasi ya Makamu Mwenyekiti ina mgombea mmoja ambaye ni Mhe. Juma Duni Haji na Ukatibu Mkuu ni Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

Aidha Prof. Lipumba ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe kuwa bado chama hicho kinaendelea na juhudi zake ili kuweza kupata katiba ya wananchi, katika mchakato wa katiba mpya unaotarajiwa kuendelea tena mwezi Ogasti, 2014.

Katika hatua nyengine Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Mhe. Machano Khamis Ali, amesema ameamua kwa hiari yake kutogombea tena nafasi hiyo kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo sababu za kiafya.

“Mimi nimeamua kuwa mfano ndani ya chama chetu, sitaki kuwa king’ang’anizi wa nafasi hii, nimeona nisigombee tena nafasi hii kutokana na sababu nilizozieleza, lakini nakuahidini kwamba sitokwenda chama chengine na nitaendelea kutoa mchango wangu wote katika kukijenga na kukiendeleza Chama chetu”, aliweka wazi Mhe. Machano.

Mapema akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wajumbe wa Baraza Kuu na watendaji wengine wa Chama hicho, Bibi Najma Khalfan amewatanabahisha viongozi na wanachama kuungana ili waweze kupata ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

0 comments:

 
Top