Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa shilingi Milioni Nne ikiwa ni nusu malipo ya gharama ya shilingi milioni Nane ilizoahidi kutoa kwa ununuzi wa Mashua kwa ajili ya kufidia chombo cha Wavuvi wa Kijiji cha Kivunge kilichochomwa moto mwezi Januri mwaka huu wa 2014 katika Kisiwa cha Tumbatu.

Ikasisitiza tena na kuonya kwamba hilo litakuwa ni tukio la mwisho kubebwa na Serikali la kulipa fidia kwa migogoro yoyote itakayosababishwa na wana jamii katika maeneo mbali mbali kutokana na hitilafu wanazoweza kuzikabili wana jamii wenyewe.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akikabidhi fedha hizo kwa mdhamini wa ujenzi wa Mashua hiyo Bwana Ali Makame Madaha { Cheupe } hafla iliyofanyika pembezoni mwa bahari ya Nungwi ilipochongwa mashua hiyo Mkoa wa Kaskazini Ungua.

Balozi Seif alisema fedha hizo ni hatua ya kwanza na Serikali itajitahidi kukamilisha nusu iliyobakia katika kipindi kifupi kijacho itakayokwenda sambamba na wavuvi wanaohusika na suala hilo kupatiwa vifaa vyengine kama nyavu ili waendeleze uvuvi unaokubalika Kiserikali.

Akipokea fedha hizo mdhamini wa ujenzi wa chombo hicho cha uvuvi ambae pia ni Katibu wa Kamati Tendaji ya hifadhi ya Mnemba na Chwaka Bwana Ali Makame Madaha { Cheupe } aliishukuru Serikali kwa hatua iliyochukuwa ya kununua chomba hicho kwa wakati muwafaka.

Hata hivyo Bwana Madaha Cheupe alitahadharisha kwamba ongezeko la wavuvi katika baadhi ya sehemu hapa nchini ndio sababu kuu inayoleta migogoro ya uvuvi kwenye maeneo mbali mbali ya bahari.

Aliiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuiongezea nguvu ya uwezeshaji Idara ya Uvuvi na mazao ya Baharini katika kubuni miradi mbadala itakayosaidia kukabiliana na msongamano huo wa wavuvi.

Akikabidhi rasmi chocho hicho kwa wavuvi wa Kijiji cha Kivunge na kushuhudia pia na Uongozi wa Serikali na Vyama vya Siasa wa Mkoa wa kaskazini Unguja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliendelea kuwaasa Wananchi kwamba Serikali kamwe haitakuwa tayari kubeba dhamana ya kulipa fidia ya mali au vyombo watakavyoharibiana kwenye migogoro wanayoweza kuiepuka.

Balozi Seif aliwahimiza Wananchi na hasa wavuvi katika maeneo mbali mbali nchini kuepuka ugomvi na pale yanapojitokeza mambo yenye kuleta hitilafu njia nzuri ni kukaa pamoja kwa pande husika katika mbinu za kuyapatia ufumbuzi muwafaka.

Tarehe 6 juni mwaka huu akizungumza na Wananchi wa Kivunge Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema tabia ya migogoro ya wavuvi ambayo inaonekana kuchochewa na baadhi ya wana siasa imekuwa ikiipa mzigo mkubwa Serikali kuu katika kugharamia fidia zisizo na msingi.

Balozi Seif alifahamisha kwamba masuala ya maendeleo na kiuchumi kuingizwa mambo ya kisiasa kamwe hayatekelezeki na daima yataendelea kuwaharibia wananchi kimaisha.

Chombo hicho cha uvuvi walichokabidhiwa wavuvi wa kijiji cha kivunge kina uwezo wa kuchukuwa watu kwenda katika shughuli zao za uvuvi kati ya ishirini na ishirini na tano kwa wakati mmoja.

Fundi wa chombo hicho Kilichopewa jina Riziki zina Mungu Rajab Haji Juma alitoa baraka na aliashiria kitendo cha kukishua baharini chombo hicho tayari kuanza safari ya kuelekea nyumbani katika kijiji cha kivunge.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top