Mtaalamu wa masuala ya filam kutoka Uingereza Nick Broonfield amesema Visiwa vya Zanzibar ina mazingira mazuri kutokana na maumbile yake ya asili yanayotoa ushawishi kwa watengenezaji wa filam wa kimataifa kuitumia fursa hiyo.

Nick alieleza hayo wakati uongozi wa Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar { ZIFF } ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Nick Broonfield alisema Uongozi wa Tamasha la Kimataifa Zanzibar haukukosea kuichagua Zanzibar kuwa kituo cha kuendeleza maonyesho ya Tamasha la filam linalofanyika kila mwaka.

Alifahamisha kwamba filam ni mfumo mzuri na muhimu unaotoa fursa kwa jamii yoyote ile kuwa na mafungamano ya mawasiliano na hatimae husaidia mapato ya jamii kutokana na safari za wageni walioshajiika kupitia filam wanazoziona.

Naye Mwakilishi wa Taasisi inayosimamia kukuza vipaji vya wasanii wa filam na michezo ya kuigiza { ZUKU } ambayo ni mfadhili mkuu wa Tamasha la Filam Zanzibar Richard Alder alisema taasisi yake itaendelea kuunga mkono Tamasha hilo ili kusaidia vijana kujiendeleza.

Richard alieleza kwamba Maonyesho ya Tamasha ni njia pekee inayotoa nafasi ya kuibua vipaji vya vijana katika masuala ya michezo ya kuigiza pamoja na uandaaji wa filam.

Akizungumza na Uongozi huo wa Tamasha la Kimataifa Zanzibar { ZIFF } Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema filam mbali ya kuburudisha lakini pia hutoa taaluma kwa watazamaji.

Alisema maonyesho ya sinema kwa kutumia filam mbali mbali ambayo yalikuwa maarufu hapa Zanzibar katika miaka ya nyuma yanaonekana kufifia au kufa kabisa kutokana na mabadiliko ya teknolojia ya filam iliyopo hivi sasa.

“ Tulikuwa na majengo zaidi ya matatu ya michezo ya sinema hapa Zanzibar, Unguja na Pemba, lakini yote yamekufa na kufanywa maduka na Ofisi baada ya kukosa wateja kutokana na mabadiliko ya filam ambayo mtu hihi sasa anaweza kuangalia akiwa nyumbani peke yake “. Alisema Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuhakikishia Uongozi huo wa Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar kwamba Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi zao katika kuona majukumu yao yanazidi kuimarika kila mwaka.

Mapema Mwenyekiti wa Tamasha la Kimataifa la Filam Zanzibar Mahmoud Thabit Kombo alisema Zanzibar bado ina vyakula vya asili ambavyo vinaweza kutumiwa kupitia matamasha tofauti.

Alisema vipo baadhi ya yakula ambavyo vinaweza kutumiwa kama ishara ya kuutangaza utamaduni wa Zanzibar katika Nyanja za kimataifa.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top