Benki ya kuhudumia Wananchi wa Kawaida Nchini { NMB } imekabidhi mchango wa Vikalio 100 kwa ajili ya kusaidia sekta ya Elimu katika Skuli za Sekondari za Donge na Kitope zilizomo ndani ya Wilaya ya Kasakazini “ B “ Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Msaada huo wa Vikalio wenye gharama ya shilingi za Kitanzania Milioni Kumi utasaidia kupunguza uhaba wa madeski kwa Skuli hizo za Donge na Kitope ambapo kila Skuli imefanikiwa kupata madeski 50.

Meneja wa Tawi la NBC Zanzibar Bwana Bakari Khamis Moh’d alikabidhi msaada huo kwa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif Ali Iddi pamoja na Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis hafla iliyofanyika hapo katika skuli ya Sekondari Kitope.

Meneja huyo wa Tawi la Benki ya NMB Bwana Bakari aliiomba Jamii kuendelea kuiunga mkono Benki hiyo ili kusaidia kuipa nguvu za kiutendaji itakaoongeza kasi ya kusaidia harakati za Kijamii Nchini.

Alisema Benki hiyo tokea kuasisiwa kwake mnamo mwaka 1997 imekuwa ikijitahidi kuunga mkono maendeleo ya Wananchi hasa katika miradi iliyomo ndani ya Sekta ya Elimu.

Akitoa shukrani zake mara baada ya kupokea msaada huo wa vikalio Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameziomba Benki nyengine Nchini kuiga mfano wa Benki ya NMB katika kusaidia maendeleo ya Wananchi.

Balozi Seif alisema taasisi za Kifedha ndani na nje ya nchi zimekuwa na mfumo maalum unaosaidia kuunga mkono juhudi za jamii katika maeneo tofauti ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Alisema Wananchi hawanabudi kushirikiana na kuzipa nguvu taasisi hiyo ili ziweze kutekeleza malengo zilizojipangia.



“ Ukweli halisi NMB ni Benki ya wanyonge. Ni Benki yetu inayolenga kuhudumia wananachi wa kipato cha chini. Huyu ndie rafiki yetu na tunapaswa kumuunga mkono “. Alisema Balozi Seif.

Naye Mbunge wa Jimbo la Donge Mh. Sadifa Juma Khamis alisema Benki ya NMB imeonyesha umahiri mkubwa katika kutekeleza ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 ambayo imejipangia kuimarisha Sekta ya Elimu iliyo muhimili pekee wa maendeleo ya kiuchumi kwa Taifa lolote Duniani.

Akisoma risala ya Walimu na wazazi wa Skuli za Donge na Kitope Mwalimu Mkuu wa Skuli ya Sekondari ya Kitope Mwalimu Suleiman Juma Makame ameupongeza Uongozi wa Benki hiyo pamoja na ule wa Jimbo la Kitope kwa juhudi zao zilizojikita zaidi katika kuimarisha Sekta ya Elimu.

Hata Hivyo Mwalimu Suleiman alisema zipo changa moto zinazoendelea kuzikabili skuli hiyo akatolea mfano wa Skuli yake ya Kitope inayokabiliwa na uhaba wa Vifaa vya Maabara pamoja na uwezekwaji wa jengo moja la Skuli hiyo.

Akitoa salamu za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Afisa Elimu wa Wilaya ya Kaskazini “B “ Mwalimu Ussi Machano alieleza kwamba mchango wa Mbunge wa Jimbo la Kitope Balozi Seif katika Sekta ya Elimu umekuwa mfano wa kuigwa na Viongozi wengine hapa Nchini.

Mwalimu Ussi Machano alisema kwamba mchango huo kwa kiasi kikubwa umeipunguzia mzigo mkubwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali katika ukamilishaji wa Majengo mbali mbali ya Skuli yanayoanzishwa na wananchi wenyewe kwa mpango wa kujitolea.

Huu ni mkupuo wa Pili kwa Benki hiyo ya NMB kusaidia vikalio kwa Skuli za Donge na Kitope.



Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top