Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko katika matayarisho ya mwisho ya kuandaa Sera mpya ya Ardhi itakayozingatia hali halisi ya mahitaji na matumizi bora ya Ardhi iliyopo Nchini kwa Maendeleo ya Kiuchumi.

Sera hiyo itakwenda sambamba na mageuzi makubwa ya kuendeleza sekta hiyo katika kupanga upya matumizi ya ardhi yote ya Zanzibar yanayoendana na matayarisho ya Mipango Miji yanayoendelea.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika sherehe za kuadhimisha mwaka mmoja wa usajili wa Ardhi zilizofanyika katika Hoteli ya Bwawani Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema usajili wa ardhi Nchini kwa muda mrefu ulikuwa ukikatishwa mara kwa mara kutokana na migogoro ya ardhi inayoleta kero kutokana na mizozo ya Kijamii na kuigharimu Serikali Kuu fedha nyingi.

Alisema migogoro mingi iliyojichomoza katika maeneo mbali mbali hapa Nchini imekuwa ikisababishwa na baadhi ya Wananchi kwa kuamua kutumia ardhi kinyume na utaratibu uliowekwa kisheria wa haki ya matumizi ya ardhi.

“ Usajili wa ardhi umekuwa ukihimizwa sana Duniani kutokana na kupelekea usimamizi mzuri wa matumizi ya ardhi. Usajili wa Ardhi unahitaji ardhi kutambuliwa, kupimwa na hatimae miji na vijiji vipangwe bila ya migogoro “. Alisisitiza Balozi Seif.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na watendaji wa Taasisi za Ardhi na Upimaji katika hatua za awali za utambuzi na upimaji hasa kwenye maeneo ambayo bado hayajafanyiwa usajili ili kufanikisha vizuri azma hiyo njema ya Serikali.

Alisisitiza kwamba kwa vile ardhi ni msingi mkuu wa maendeleo kwa nchi yoyote Duniani, Wananchi hawana budi kujenga katika maeneo yaliyopimwa kwa kufuata taratibu zilizowekwa na sheria za mipango miji na vijiji.

“ Katika usajili wa ardhi malengo yaliyokusudiwa ni kuona kuwa watumiaji halali wa eneo husika wanatambuliwa na maeneo yanapimwa, vyenginevyo uvamizi wa ardhi na ujengaji holela usiofuata taratibu kamwe hautovumiliwa “. Alionya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Katika kufanikisha nia njema ya Taifa ya matumizi mazuri ya ardhi Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inapanga upya matumizi ya ardhi katika ukanda wa pwani, Vijijini na tayari zoezi hilo limeshakamilika katika Kijiji cha Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alieleza kuwa jitihada kubwa zimechukuliwa na Serikali juu ya suala zima la upimaji na usajili wa ardhi ambapo jaribio la kwanza la usajili kwa utaratibu wa utambuzi unaoambatana na upimaji wa ardhi lilifanyika mwaka 1994 kwa ufadhili wa Serikali ya Finland kupitia mradi wa ZILEM.

Balozi Seif alifahamisha kwamba mipangilio ya upimaji wa mashamba kwa lengo la usajili ilianza kufikiriwa tokea mwaka 1920 lakini ilishindikana kutekelezwa kutokana na ukosefu wa fedha.

Hata hivyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema mnamo mwaka 1981 Serikali ilifanikiwa kufanya upimaji wa ardhi kwa msaada wa Serikali ya Sweden lakini usajili wake haukufanyika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliishukuru Serikali ya Finland kupitia Balozi wake aliyopo Nchini Tanzania pamoja na kuipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye zoezi hilo la usajili wa ardhi kupitia mradi wa MKURABITA. Akitoa Taarifa ya usajili wa ardhi MRAJIS WA Ardhi Zanzibar Bibi Mwanamkaa Abdullrahman Mohd alisema Nyumba zipatazo elfu 1,300 zimeshasajiliwa katika mshehia 16 zilizomo ndani ya Wilaya ya Mjini.

Bibi Mwanamkaa alisema wataalamu na watendaji wa Ofisi ya msajili wa ardhi wanaendelea kuyatambua mashamba yapatayo 22,746 Unguja na Pemba.

Alieleza kwamba katika kwenda sambamba na zoezi hilo la usajili wa ardhi hatua zinaendelea kuchukuliwa katika usajili wa ardhi kupitia mfumo wa kisasa wa mtandao wa Kompyuta.

Hata hivyo Mrajisi huyo wa Ardhi alielezea changamoto zilizojitokeza katika zoezi hilo la usajili wa ardhi katika maeneo yaliyokatwa eka tatu tatu ambayo mengi kati yao yamevamiwa kwa ujenzi wa nyumba za kudumu .

Aliipongeza Serikali Kuu kwa kusaidia utatuzi wa migogoro ya ardhi katika baadhi ya maeneo hapa nchini ambao umeleta utulivu baina ya pande zinazojichomoza kuzozana katika matumizi ya ardhi hizo.

Mapema Waziri wa Ardhi, Makazi, Maji na Nishati Mh. Ramadhan Abdulla Shaaban alisema migogoro inayofanywa na wajanja katika matumizi ya ardhi inaweza kuondoka iwapo wananchi wataamua kusajili ardhi wanazozitumia kila siku.

Waziri Shaaban alisema lengo lililowekwa na Ofisi ya Usajili wa Ardhi ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2015 usajili wa ardhi ufikie asilimia 50% ya ardhi yote ya Unguja na Pemba.

Alisema eneo lililosajiliwa hadi sasa bado ni dogo ikilinganishwa na ardhi yote iliyopo katika Visiwa vya Zanzibar. Hivyo juhudi za Wananchi katika kushirikiana na Serikali Kuu zinahitajika zaidi ili kufanikisha mpango huo muhimu kwa maendeleo ya Taifa.

Katika Maadhimisho hayo ya kusherehekea mwaka Mmoja wa usajili wa Ardhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alizindua kadi ya usajili wa ardhi sambamba na kuzindua jarida la Ardhi.

Kadi hiyo yenye nambari maalum ya utambulisho na kumbu kumbu za usaliji wa ardhi itampa fursa muhusika kuitumia wakati wowote badala ya kuranda na waraka.

Ujumbe wa mwaka huu wa usajili wa ardhi Zanzibar ni Nyumba yangu imesajiliwa yako jee?

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top