Waheshimiwa Mawaziri,
Waheshimiwa Wabunge na Wawakilishi,
Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi,
Makatibu Wakuu wa Wizara mbali mbali za Serikali za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
Meya wa Mji wa Zanzibar,
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini ya ZSSF,
Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZSSF,
Viongozi wa Vyama vya Siasa Zanzibar,

Wawakilishi wa Kampuni ya Ujenzi ya CRJE na Mshauri wa Ujenzi Covell Mathews and Partnership,

Ndugu Waalikwa Mabibi na Mabwana.
Assalam Aleykum,

Nachukua fursa hii adhimu kumshukuru Muumba wa yote kwa kutuwezesha kukutana leo hii hapa tukiwa ni wazima wa afya njema katika sherehe adhimu ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanja kipya cha kufurahishia watoto cha ZSSF-UHURU ambacho kipo hapa Kariakoo, Zanzibar.

Vile vile, sina budi kuwashukuru wahusika kwa maandalizi mazuri ya sherehe zetu hizi ikiwa ni miongoni mwa shamra shamra za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mapinduzi ambayo yametufanya tuwe huru na furaha na bashasha kila hatua aya kimaendeleo tunayopiga.

Pia naushukuru Uongozi wa Wizara ya Fedha na ZSSF kwa kunialika kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii muhimu.

Kumbukumbu za kiwanja hiki sambamba na kile cha Pemba kinaonesha kuwa awali kilifunguliwa mwaka 1975, naamini mnakubaliana nami kuwa kwa wakati ule kilikuwa ni kiwanja cha kipekee kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki kwa ajili ya kuwakutanisha watoto wetu bila kujali kabila zao rangi, dini na mambo mengine kama ambavyo lengo la Mapinduzi ya mwaka 1964 lilivyojiwekea.

Hivyo basi, kiwanja hiki kikapewa jina la ‘UHURU’ lenye mnasaba wa moja kwa moja na Mapinduzi ya mwaka 1964.

Na naomba kwa ZSSF ambao ndio wasimamizi wakuu wa kiwanja hiki kuendeleza lile lengo la kuwapatia huduma watoto wetu ambao wanatokana na wakulima, wafanyakazi na hata wafanyabiashara linaendelezwa na bila kujali kipato chao.

Baada ya kuona kuwa Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, nguvu zake kupungua na kiwanja hiki kuchakaa sana, Baraza la Mapinduzi chini ya Mwenyekiti wake kwa wakati ule Mhe. Dk. Amani Abeid Karume alitumia busara zake kwa kukihamishia kwa Taasisi yake ya ZSSF ili kukiimarisha na kuwa katika hali bora zaidi.

Uamuzi ule wa busara sasa ndiyo tunaiona faida yake kuwa Serikali haikukosea kukipeleka katika Taasisi hii makini na tunaamini hamtoiangusha Serikali. Tunaishukuru sana ZSSF kukubali maamuzi ya Serikali na kutekeleza maagizo mliyopewa, hongereni sana.

Ndugu Wananchi,

Kama inavyoeleweka kuwa tunatimiza miaka 50 ya Mapinduzi yetu Matukufu ya Zanzibar yaliyoikomboa nchi hii kutoka katika minyororo ya kikoloni. Wakati wazee wetu wanafanya Mapinduzi yale, wasioipendelea mema nchi hii walisema hatutaweza kujitawala na kujiletea maendeleo sisi wenyewe pasi na kusimamiwa kama vile zamani.

Napenda nikariri maneno ya wazee wetu waliokuwa wakiwajibu wenye kauli za kukatisha tamaa kuwa “waliosema hatuwezi na waje kututizama”. Nami nawaambia watakapokuja pia wafike na hapa Kariakoo waje kuangalia hatua ambazo tunaendelea kuzipiga kuzidi kuendelea.
 
Hivyo basi, kitakapokamilika kiwanja hiki kitazidi kuonyesha matunda ya Mapinduzi ambayo yametokana na nguvu na usimamizi wa Wazanzibari wenyewe na kielelezo chengine cha kuonesha kukua kwa uchumi wa nchi kwani hakuna fedha za msaada zilizotumika katika ujenzi wa kiwanja hiki.

Ndugu Wananchi,

Madhumuni ya ujenzi wa kiwanja hiki kama ilivyoelezwa kuwa umezingatia sifa nne za miradi ya uwekezaji ya ZSSF ambapo moja kati ya sifa hizo ni kuzingatia maslahi ya kiuchumi na kijamii (Social and economic utility).

Kwa upande wa maslahi ya kiuchumi nia ya ZSSF bila shaka ni kuweza kuzalisha zaidi kile ambacho kinachokusanywa kutoka kwa wanachama waajiri na waajiriwa, ili kuweza kulipa mafao wakati ukifika wa kufanya hivyo. Na imani kubwa kile ambacho kinachokusanywa kutoka kwa mwanachama kinalipwa kikubwa kulinganisha na alichochangia, faida hiyo ndiyo hutokana na miradi kama hii na mingineyo inayofanywa na ZSSF.

Lakini pia ni imani yangu kuwa juu ya suala la kiuchumi kiwanja hiki kitatoa ajira kama ilivyoelezwa kwa wasimamizi na waendeshaji wa kiwanja lakini kutakuwa na maeneo ya biashara zenye mnasaba wa kiwanja hiki. Hivyo basi, kwa watakaobahatika kukodishwa sehemu hizo wataendeleza kipato chao kwa biashara au huduma watakazokuwa wakiziendesha.

Tumepata taarifa kuwa mara baada ya kukamilika kwa kiwanja hiki na kuanza kazi rasmi, ZSSF inatarajia kurudisha fedha baada ya miaka kumi. Kwa upande wetu Serikali tunawaombea dua mradi huu uweze kulipa kwa muda huo na pia kuanzishwe miradi mengine yenye tija kwa pande zote husika.

Ama kwa maslahi ya kijamii, kilichosababisha ZSSF kuendeleza mradi huu, ni kuweka mazingira mazuri baina ya wazee na watoto wao kama ilivyozoeleka katika hekima zetu huwa tunasema furaha ya watoto neema kwa wazee bila shaka kupitia kiwanja hiki yote mawili yatapatikana furaha kwa watoto lakini pia faraja kwa wazee

Kama nilivyosema awali, kukamilika kwa mradi huu ni miongoni mwa matunda ya Mapinduzi. Napenda niongezee kwamba pia inatokana na sera madhubuti za Serikali katika kupunguza umasikini kwa kuwapatia ajira wananchi. Naishukuru sana ZSSF kwa kuchukua hatua hii.

Ndugu Wananchi,

Katika suala zima la uwekezaji, naipongeza ZSSF kwa hatua iliofikia lakini isibweteke na miradi iliyoanzisha, ni vyema ikatafuta maeneo mengine zaidi hususan katika vitega uchumi visivyohamishika na vyenye usalama zaidi ili kuwa na rasilimali zaidi ambazo zitasaidia kuufanya Mfuko huu tegemeo kwa jamii na Serikali kuwa imara zaidi.
 
Kwa kuwekeza katika miradi ya aina hii ambayo ni salama itaufanya Mfuko uwe endelevu na kuweza kuwapatia wanachama mafao yaliyo bora zaidi. Aidha, ni hatua ya kuuepushia Mfuko huu na janga la kufilisika. Na hapa naipongeza ZSSF kwa uamuzi wake wa kugharamia ujenzi wa mnara wa kumbu kumbu ya miaka 50 ya Mapinduzi Matukufu, ambao utawekewa jiwe la msingi na Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi hivi karibuni ikiwa ni kitega uchumi kingine.

Napenda ZSSF ielewe kwamba wanachama wake wote wanauangalia Mfuko huu kwa matumaini makubwa, matarajio yao ni kwamba pale watakapostaafu hawataambiwa njoo kesho au rudi mwezi ujao.

Vile vile, wananchi na wanachama wa Mfuko huu ni vyema wakaelewa kwamba Mifuko kama hii ina jukumu la kuendeleza uchumi wa nchi katika nyanja mbali mbali, kujenga majengo imara na yenye kuleta haiba katika nchi. Hivyo ZSSF imeanza kulitekeleza jukumu hilo. Napenda ieleweke wazi kuwa ujenzi huu haukuwa utashi wao bali kuna miongozo imara ambayo imefuatwa hadi kufikia hatua hii kwa nia ya kuwekeza, kupata faida na kulipa mafao yaliyo bora kwa wanachama bila kupoteza rasilimali kubwa ambayo ni michango ya wanachama.

Napenda kutoa wito kwa ZSSF kuweka mikakati imara na usimamizi madhubuti ambayo itaharakisha kurejesha fedha zilizotumika kujenga kiwanja hiki ili pia kuweza kuendeleza vitega uchumi vyengine.

Ndugu Wananchi,

Pia natoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla ambao watafika hapa kupata huduma mbali mbali, kuzithamini juhudi za Serikali yenu ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mfuko huu, kuutekeleza kwa vitendo ule msemo maarufu usemao ‘kitunze kidumu’.

Kutunza pembea na suala la usafi hususan katika sehemu kama hii itakayokusanya watu wengi linahitaji kupewa kipaumbele cha aina yake ili kuepusha madhara kwa watoa huduma na pia watumiaji lakini pia kupoteza haiba yake kwa muda mfupi.

Aidha, katika ujenzi huu muhakikishe kuwa kunazingatiwa watu wenye mahitaji muhimu na wao waweze kufika na kupatiwa huduma kama wenzao vyenginevyo tutakuwa hatuwatendei haki kama ambavyo wanavyostahiki.

Pia, wakati ujenzi ukiendelea sio vizuri kwa wafanyakazi wa ujenzi au wakaazi waliozunguka kiwanja hiki kufanya vitendo ambavyo vitarejesha nyuma harakati za ujenzi au kumkatisha tamaa mkandarasi wetu CRJE. Hatua kama hiyo inaleta sura mbaya kwa wageni wetu lakini pia itaongeza gharama kwa ZSSF jambo ambalo linaweza kuepukwa.

Ndugu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya ZSSF,

Kiwango cha wananchi wanaopatiwa Hifadhi ya Jamii kupitia Mifuko kama yenu bado ni tatizo sio kwa Tanzania tu bali pia kwa nchi nyingi Barani Afrika. Takwimu zinaonyesha si zaidi ya asilimia 20 tu ndio wanaojiunga na Mifuko hii na hatimae kufaidika na huduma na mafao yanayotolewa. Kiwango hiki ni kwa waajiriwa Serikalini na Taasisi Binafsi. Hali hiii ni tafauti kwa nchi zilizoendelea kwani zaidi ya asilimia 80 ni wanachama au wanafaidika na mifuko kama hii.

Ipo haja sasa kuihusisha kikamilifu sekta isiyokuwa rasmi ambayo ina idadi kubwa ya wananchi lakini pia wanahitaji huduma kama zile wanazofaidi wanachama wenu. Kwa kuwa kutakuwepo wajasiariamali mbali mbali, naona ni eneo zuri la kuanzia kwa kuwawekea mazingira mazuri ili nao wajiunge waweze kufaidika na Mfuko huu hususan wakati wa uzee au watapofikwa na majanga mengine.

Mwisho, ninatoa shukurani zangu za dhati kwa Waziri anaehusika na Fedha na Uchumi ambae ZSSF iko chini ya Wizara yake kwa usimamizi wake mahiri, Bodi ya Wadhamini ya ZSSF na watendaji kwa ujumla kwa ubunifu wenu wa mradi huu ambao matarajio yetu sote utakuwa na tija kwa pande zote husika.

Aidha, nawapongeza wajenzi wetu CRJE ya China na mshauri wa ujenzi huu Covell Mathews and Partnership kwa umahiri wao na ushirikiano wao ili kuona kwamba kiwanja hiki kinakamilika tena kiwango kinachohitajika.

Pia nami naungana na waliotangulia kwa kuwashukuru Afisi ya Mkoa wa Mjini Magharibi kwa msaada wao mkubwa kwenu, Shirika la Bandari Zanzibar kwa nguvu zao kuhakikisha pembea zinasimama pamoja na Taasisi nyengine zinazosaidia kwa njia moja ama nyengine.

Nawatakieni afya njema itakayopelekea kuendeleza majukumu yenu na ya Taifa kwa ujumla na pia ninawaomba kushiriki katika kilele cha sherehe zetu za miaka 50 pale Uwanja wa Amani tarehe 12 Januari 2014.

Mwisho kabisa, nawashukuru kwanza msoma Quraan, msoma utenzi na wasanii wetu wa ngoma ya kibati.

Kwa hayo machache sina budi kuwashukuru nyote kwa kuhudhuria hapa na kuweza kunisikiliza.

                        MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
                        MUNGU IBARIKI TANZANIA
                        MAPINDUZI DAIMA!
                        Ahsanteni kwa kunisikiliza.

0 comments:

 
Top