Mheshimiwa Ali Juma Shamuhuna, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali,
Mheshimiwa Abdullah Mwinyi Khamis, Mkuu wa Mkoa wa Mjini na Magharibi,
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri,
Waheshimiwa – Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Mpendae,
Waheshimiwa Viongozi mbali mbali mliopo hapa,
Ndugu Waalikwa,
Mabibi na Mabwana.

Asaalam Aleykum,

Napenda kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na uzima na kutuwezesha kukutana hapa leo katika shughuli hii muhimu ya ufunguzi wa Skuli ya Sekondari ya Mpendae tukiwa katika hali ya afya njema. Shughuli ambayo inafanyika ikiwa ni sehemu ya shamra shamra za maadhimisho ya miaka 50 ya Mapinduzi yetu Matukufu ya mwaka 1964.

Aidha, napenda kuushukuru uongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa heshima hii kubwa ulionipa ya kuwa Mgeni Rasmi katika shughuli hii.

Ndugu Wananchi, napenda kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Mpendae na wa Wilaya ya Magharibi kwa kupata Skuli mpya na nzuri na ya kisasa ambayo itawawezesha vijana wao kusoma vizuri, bila ya usumbufu wala bughdha ya kuyafuata masomo ya Sekondari kwa masafa marefu. Skuli sasa ipo nyumbani, kilichobaki ni juhudi yao tu ya kufanya vizuri katika masomo ya msingi ili waweze kuingia katika Skuli hii. Ningewasihi sana wanafunzi wataopata bahati ya kuingia katika skuli hii waitunze vizuri ili iendelee kuwa na haiba nzuri kama inavyoonekana sasa.

Ndugu Wananchi, leo tuna furaha kubwa kuwa tunasherehekea miaka 50 ya Mapinduzi yetu na kuona hatua kubwa tulioipiga katika sekta ye Elimu. Naipongeza sana Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kwa kazi nzuri walioifanya katika kipindi cha miaka 50 tangu kufanyika kwa Mapinduzi Matukufu. 
 
 Miongoni mwa kazi hizo ni kuendelea kuimarisha miundombinu ya elimu, na kuipandisha hadhi sekta ya elimu kwa jumla, hasa katika ujenzi wa shule za msingi, sekondari pamoja na vyuo vya amali nchini.


Miaka 50 ya Mapinduzi imeshuhudia kufunguliwa kwa fursa mbali mbali za elimu hapa nchini ambazo huko nyuma, mimi mwenyewe na wenzangu wengi wa umri wangu, tukiwa mashahidi kuwa hazikuwepo. Huko nyuma kabla ya Mapinduzi tulikuwa na skuli chache sana za sekondari na hata za msingi, wachilia mbali vyuo vya elimu ya juu. 
 
 Na hata hizo skuli chache za sekondari zilizokuwepo wakati huo, wakati wa kikoloni ni watu wachache tu waliokuwa na fedha ndiyo waliokuwa wanafaidika. Skuli nyingine zikiwa za binafsi ama za kikabila au za kidini kama vile, Skuli ya Agakhan, Kiungani na nyinginezo za aina hiyo. Na ndiyo maana baada ya Mapinduzi, Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mzee Abeid Amani Karume akaamuru elimu bila ya malipo ili hata watoto wa kimaskini waweze kupata fursa za kusoma.

Tangu wakati huo harakati za kuongeza skuli za msingi na sekondari ziliongezeka kwa kasi kubwa. Mfano, kabla ya Mapinduzi skuli za msingi zilikuwepo 62 tu ambazo zilikuwa na jumla ya wanafunzi 24,334. 
 
Mpaka mwaka huu tukisherehekea miaka 50 ya Mapinduzi zipo Skuli za Msingi 234 zenye jumla ya wanafunzi 247,353. Kabla ya Mapinduzi zilikuwepo Skuli za Sekondari 4 tu zilizochukua jumla ya wanafunzi 1,011. Leo tunaposherehekea miaka 50 ya Mapinduzi tunazo Skuli za Sekondari 144 zenye jumla ya wanafunzi 76,706. Kabla ya Mapinduzi hatukua na chuo chochote cha elimu ya juu, ukiacha Chuo cha Ualimu cha Beit-el-Ras, ambacho kilichukua idadi ndogo sana ya wanafunzi wa kusomea ualimu. Leo tuna Vyuo vya Elimu ya Juu 3, pamoja na Vyuo vya Elimu ya Juu vya Kisekta 8. 

Hii inatuonyesha dhahiri ni kiasi gani miaka 50 ya Mapinduzi imetufanya tupige hatua kubwa sana katika sekta ya elimu nchini kwa juhudi za Serikali na wananchi wenyewe. Hivyo, kufunguliwa kwa Sekondari ya kisasa ya Mpendae ni fursa nyengine kwa watoto wetu kupata elimu ya Sekondari katika mazingira ya kisasa, na hivyo basi ni juu ya sisi wazazi na walezi kuwahimiza vijana wetu kuzitumia ipasavyo fursa hizo kwa faida yao na Taifa kwa jumla.

Ndugu Wananchi, ningependa kutoa wito kwa uongozi wa Wizara ya Elimu kuifanya mitaala ya masomo yanayofundishwa kuwa bora zaidi kila inapobidi ili kwenda na wakati. Ili haya yafanikiwe, walimu nao wapatiwe mafunzo (refresher courses) ya mara kwa mara ili waweze kutumia mitaala hiyo. 
 
 Ni dhamira ya Serikali kupata vijana wengi zaidi waliomaliza Vyuo Vikuu, kwa hivyo skuli za sekondari zilizojengwa na zinazoendelea kujengwa na Serikali yenu ya Mapinduzi ya Zanzibar, Unguja na Pemba zikiwa kama mazalisho yenye lengo la kuzalisha vijana wengi wa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu. Naendelea tena kusema kwamba ni jukumu la vijana wenyewe kuzitumia vizuri fursa hizi zinazotolewa na Serikali yao.

Ndugu Wananchi, ningependa kuwasihi vijana kutozichezea chezea nafasi zilizopo za kusoma kwa sababu wakizichezea nafasi hizo, vijana wengi hawatoweza kushindana na vijana wenzao wa nchi za Afrika Mashariki. 
 
Dawa ya tatizo hili ni vijana wetu kupania kutafuta elimu ya juu kwa nguvu zao zote, na wajitahidi kuyapenda masomo ya Sayansi kwani ndiyo ulimwengu wenyewe tunaoishi nao – ulimwengu wa Sayansi na Teknolojia. 
 
 Uchumi wa Afrika Mashariki unaonyesha utazalisha ajira nyingi kwa wananchi wake. Kuvumbuliwa kwa mafuta Uganda na hivi karibuni Kenya, kuvumbuliwa kwa gesi Tanzania ni viashiria tosha kuwa kutakuwepo na ajira nyingi kwa vijana waliosoma. Vijana waliomaliza Vyuo Vikuu watakuwa na nafasi nzuri ya kupata ajira hizo.

Ningependa pia kuwasihi wanafunzi pamoja na walimu kuwa tayari na mabadiliko ya teknolojia ya habari. Walimu lazima wajifunze namna ya kutumia kompyuta na kuwa tayari kutumia chombo hicho kwa kufundishia wanafunzi. Kwa upande wa wanafunzi na wao lazima kujua kuitumia kompyuta kwani itawarahisishia kujifunza kwa urahisi zaidi. 
 
 Serikali ina mpango wa kutoa kompyuta za kutosha kwa kila skuli ili wanafunzi waweze kutumia mitandao kwa ajili ya masomo yao. Hivi karibuni nilipofanya ziara Marekani tulipata bahati ya kupata msaada wa kompyuta zipatazo 3500 kwa ajili ya kusambazwa katika skuli mbali mbali za Unguja na Pemba kwa ajili ya kusomeshea vijana wetu. Sehemu ya kwanza ya kompyuta 250 zitaweza kufika nchini wakati wowote kuanzia sasa.

Ndugu Wananchi, pamoja na juhudi hizo za Serikali, lakini na walimu pia wanao wajibu wa kuwasomesha vijana wetu vizuri ili waweze kupasi wengi zaidi, tena kupasi kihalali siyo kwa kukopia. Vijana wetu waache kuangalia TV, Video na Internet usiku kucha, kwani wakifanya hivyo, darasani kutakuwa hakuna kusoma ila kusinzia tu.

Pamoja na masomo ya kawaida, ni muhimu pia kuwa na mafunzo ya ziada ambayo yatasaidia wanafunzi kuchemsha bongo ili kuondokana na kuwa na mambo yale yale (routine) kila siku darasani, ili waongeze motisha wa kusoma. Mathalan, skuli za sekondari zinaweza kuanzisha “debating societies”, michezo ya kuigiza kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili. Mambo haya ambayo zamani yalikuwepo sasa hayapo tena. Ni vema kurudishwa katika skuli zetu za sekondari.

Wanafunzi nao, wajitahidi kuyatunza majengo ya skuli yao ili yaendelee kuwa mazuri na ya kungꞌara kama yalivyo sasa, pamoja na kuvitunza vifaa vilivyomo ndani yake, na pale panapotokea uharibifu, uongozi wa Skuli uchukue hatua za haraka kurekebisha.

Mwisho, napenda kuwashukuru kwanza, msoma Quraan, pili msoma utenzi na tatu wasanii wetu.

Mwisho kabisa, nawashukuru tena kwa kunialika kuja kujumuika nanyi katika shughuli hii ambayo imefana sana.

Ahsanteni sana.

0 comments:

 
Top