Wazanzibari wote walioko ndani na nje ya Zanzibar wana fursa, haki na Uhuru wakati wowote kusaidia kwa njia mbali mbali maandalizi na hatimae kufanikisha sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kutimia robo Karne ambayo ni sawa na miaka 50 iliyopita.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibarf Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akizungumza na Wajumbe wa Kamati ya Wafanyabiashara ya kushajiisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika maadhimisho ya Sherehe za kutimia miaka 50 ya Zanzibar aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar. 

Balozi Seif alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga kuwaungalisha Wazanzibari wote popote pale walipo ili kuona wanashiriki kikamilifu kwenye maadhimisho hayo yanayotarajiwa kuwa ya aina yake na Kihistoria hapo mwakani. 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliieleza Kamati hiyo baadhi ya mambo yaliyopangwa kufanya ndani ya vugu vugu la maadhimisho hayo ambayo yatasaidia kutoa taaluma kwa Jamii hasa kile kizazi kilichozaliwa baada ya mapinduzi ya mwaka 1964 ambacho bado hakijaelewa dhamira hasa ya kufanyika kwa Mapinduzi ya Zanzibar. 

Balozi Seif ambae pia ni Mwenyekiti wa Sherehe na Maadhimisho ya Taifa aliyataja baadhi ya mambo yaliyolengwa kufanya katika kipindi hicho cha sherehe kuwa ni pamoja na warsha, makongamano kwa kushirikisha vyama vya Siasa, matembezi ya kuashiria sherehe hizo pamoja na usiku maalum wa burdani na ngoma za asili. 

Alifahamisha kwamba Mnara Maalum wa kumbu kumbu ya Mapinduzi utajengwa ili kupamba sherehe hizo za aina yake zitakazotoa pia fursa ya kualikwa kwa Viongozi wa nchi rafiki za mwanzo zilizojitokeza kuunga mkono mapinduzi ya mwaka 1964.

“ Katika kupamba sherehe zetu tumeandaa kutoa nishani maalum kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa Taifa tokea Mapinduzi ya Mwaka 64 wakiwemo askari wa Vikosi vya ulinzi na usalama, wana sanaa na Utamaduni “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Kamati ya sherehe na maadhimisho ya Taifa. 

Balozi Seif aliwaomba wajumbe wa Kamati hiyo ya Wafanyabiashara ya kushajiisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika maadhimisho ya Sherehe za kutimia miaka 50 ya Zanzibar kuhakikisha wanajitolea kwa nguvu zao zote katika kufanikisha vyema kazi waliyopewa na Taifa. 

Naye mjumbe wa Kamati hiyo Mbunge wa Jimbo la Mpendae Salum Turky aliahidi akujitolea kugharamia ujenzi wa mnara huo wa kumbu kumbu ya Mapinduzi unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Mzunguuko wa Bara bara za makutano ya Nyumba za Maendeleo Michezani. 

Aliiomba Kamati ya Sekriterieti ya Sherehe na Maadhimisho ya Taifa Zanzibar kumpatia michoro ya ujenzi wa Mnara huo ili apate wasaa wakujiandaa kuitekeleza kazi hiyo ambayo anaamini kwamba atakuwa ametoa mchango na kuweka historia ndani ya maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar. 

“ Tunashukuru kuona kwamba Zanzibar inaingia kutimiza miaka hamsini ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 ikiwa katika hali ya amani na utulivu hali ambayo ni nadra kupatikana katika baadhi ya Nchi Duniani “. Alifafanua Mjumbe huyo wa Kamati hiyo Salum Turky. 

Kwa upande wao wajumbe wengine Simai Mohd, Ahmada Abdullwakil, Sharifa Khamis na Meneja wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zantel Zanzibar Mkweche wameipongeza Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi wake wa kuanza kujiandaa mapema ya sherehe hizo kubwa. 

Hata hivyo waliishauri Serikali kufikiria kutenga maeneo ambayo wafanyabiashara wanaweza kuyatumia kutangaza biashara zao katika njia maalum itakayotoa fursa ya kuchangia maadhimisho hayo. 

“ Sio mbaya kwa Serikali kutafuta njia ya kuwashirikisha pia Wafanyabiashara wa Tanzania Bara hasa wale waliowekeza vitega uchumi vyao hapa Zanzibar na pia wenye imani ya muelekeo wa kuunga mkono maadhimisho hayo “. Alisisitiza Simai Mohd. 

“ Wakati tumejikubalisha na sisi kuingia katika ulimwengu wa sayansi na tenolojia na kwa vile wenzetu wamejiimarisha vyema katika masuala ya utambulisho wao itapendeza nasisi kuelekea huko kwa kuwa na utambulisho wetu maalum ambao utawapa fursa wageni na watalii kuielewa vyema Zanzibar“. Alishauri pia Mjumbe mwengine wa kamati hiyo Ahmada Abdull wakil. 

Katika kuanza rasmi jukumu zima walilopewa wana kamati hao walifikia uwamuzi wa kuanza kikao cha dharura mara baada ya mkutano huo kupanga mikakati ya kufanikisha jukumu lao. 

Ujumbe wa mwaka huu wa Maadhimisho ya sherehe za Mapinduzi ya Zanzibar kutimia robo Karne { sawa na miaka 50 } ni Amani, Umoja na Maendeleo yetu ni Matunda ya Mapinduzi ya 1964. “ Mapinduzi Daima “.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top