Wanachama wa CCM na Wananchi wameaswa kujiepusha na tabia ya baadhi ya watu wenye tabia ya kuendeleza matusi na kejeli kwa viongozi wao ambayo hujenga chuki na uhasama na hatimae kuashiria kuvunjika kwa amani na utulivu hapa Nchini. 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapionduzi Balozi Seif Ali Iddi alitoa nasaha hizo wakati akikabidhi msaada wa seti za Televisheni, Mashine ya DVD na fedha za kuunganishia TV kwa maskani ya CCM ya Tupendane na ile ya Mama Asha Balozi Maskani zilizomo ndani ya Jimbo la Kitope Wilaya ya Kaskazini “ B”. 

Balozi Seif ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Kitope aliyekuwa akitekeleza ahadi alizozitoa kwenye maskani hizo alisema tabia hizo zinapaswa kutoungwa mkono na Wananchi walioelekeza nguvu zao zaidi katika kujiletea maendeleo yao. 

Alifahamisha kwamba Jamii imekuwa shahidi katika matukio kadhaa yaliyowahi kutokea ndani ya vipindi tofauti hapa Nchini na kuleta uvunjifu wa amani ambayo yameacha makovu baada ya kusababishwa na baadhi ya watu wanaoichezea amani kwa maslahi yao binafsi. 

“ Jamii itaendelea kukumbwa na matatizo na kukosa utulivu wa kimaisha endapo Taifa hili halitaongozwa na Chama tawala cha Mapinduzi chenye sera zinazotekelezeka na kukubalika na Wananchi walio wengi “. Alisisitiza Balozi Seif Ali Iddi. 

Mbunge huyo wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha wana CCM na wananchi wa Jimbo hilo waelekeze nguvu zao katika kujiletea maendeleo na Viongozi wao watakuwa tayari kuunga mkono juhudi hizo. 

Aliwashauri wananchi hao na wana ccm kuanzisha vikundi vya ushirika vitakavyosaidia kuongeza nguvu za pamoja katika kuelekea kwenye uzalishaji wa miradi tofauti ya kiuchumi na kupunguza ukali wa maisha. 

“ Ni vyema mkaanzisha vikundi vya ushirika vya uzalishaji mali na mimi wakati wote nitakuwa tayari kuvipa nguvu vikundi hivyo ili muweze kutekeleza vyema malengo mliyojipangia ndani ya vikundi hivyo “ . Alifafanua Balozi Seif. 

Katika utekelezaji wa ahadi hizo Balozi Seif pia alikabidhi mchango wa shilingi laki tano kwa ajili ya ununuzi wa matofali na saruji ya kuendeleza ujenzi wa Maskani ya Tupendane. 

Halkadhalika Balozi Seif akakabidhi seti za jezi na mipira kwa maskani zote mbili za Tupendane na ile ya Mama Asha Balozi Maskani vifaa na vitu vyote hivyo vikiwa na thamani ya shilingi Milioni 2 na Laki Saba {2,700,000/- }.

Othaman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top