Na Abdi Suleiman, Pemba.

MKE wa makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mama Awena Sinani Massoud, amewataka walimu wa Madrasa za Qurani kisiwani Pemba, kuwapatia watoto elimu bora kama ilivyo katika kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu.


Alisema kuwa walimu wa madarsa hawana budi kutambua kuwa hakuna atakae weza kuwalipa ispokuwa Mwenyezi Mungu, hivyo hawana budi kuwasomesha watoto hao kwa moyo mkunjufu.


Mama Awena aliyaeleza hayo jana, huko katika skuli ya Fidel Castro Vitongoji, Wilaya ya Chake Chake, Mkoa wa Kusini Pemba, wakati alipokuwa akifungua mashindano ya Tahfidhi Qurani, kwa wanawake Pemba.


“Mtoto ni amana iliyowekwa kwa wazazi, hivyo kila mmoja ni mchunga na atakwenda kuulizwa kwa jinsi alivyochunga, au kuongoza mtoto wake”alisema Mama Awena.


Alifahamisha kuwa, watoto ni hazina kubwa waliyojaaliwa wazazi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, hapana budi watoto kuandaliwa katika misingi imara ya dini ya kiislamu.


Alisema kuwa, wanawake wananafasi kubwa katika jamii na wajibu wa kuwalea watoto, ili waweze kufuata maamrisho ya Mwenyezi Mungu, kwa kushikamana na dini na kutafuta elimu.


“Wanawake ndio wachunga wakubwa wa Familia, kwa kuwa karibu na watoto wao, kuliko mwanamme, hivyo ni wajibu wenu kuwalea katika misingi imara ya dini”alifahamisha Mama Awena.


Akizungumzia madhara ya madawa ya kulevya na ngono, alisema kuwa, Ugonjwa wa ukimwi hauna dawa, hayo yote yanatokana na kuchangiwa kwa uasharati, kwa kusahau mila, tamaduni na maamrisho ya Mwenyezi Mungu.


Hivyo aliwataka wazazi kurudisha malezi ya pamoja katika kuwalea watoto wao, ili kuweza kuwa na kizazi bora, kitakacho fuata Maamrisho ya Mwenyezi Mungu, sambamba na kuvilinda vipaji vya watoto wakike, kwani watoto wa kike hukumbwa na matatizo mengi na kushindwa kumaliza elimu zao.


“Sasa wakati umefika wa kupiga vita tabia za kuwakatisha masomo watoto wakike, kwa kuwaozesha waume mapema, ili kuweza kuwa na kukiendeleza kizazi kilicho kuwa ni bora”alisema Mama Awena.


Kwa upande wake Mlezi wa Jumuiya ya Tahfidhi Qurani Pemba, Dr Suleiman Ali Yussuf, alisema kuwa kipindi cha nyuma wanawake walikuwa wako nyuma kutokana na ukandamizaji uliokuwa ukifanya na wanaume, jambo ambalo sasa limebadilika.


Alisema kuwa, kutokana na mabadiliko hayo, sasa watoto wakike wamekuwa ni wengi sana katika kuhifadhi Qurani, kuliko hata watoto wa kiume jambao ambalo lemewapa faraja kubwa sana.


“Mgeni Rasmi, Mama yetu Mama Awena, hapa leo tuna vijana 36 wanawake waliohifadhi juzuu mbali mbali, na wawili tu wanaume tena ambao hawaoni, sasa ona maajabu hayo na mabadiliko tuliyoyapata kutoka kwa vijana wetu wakike”alisema.


Hata hivyo aliwataka wazanzi kutowadharau watoto wenye ulemavu katika jamii, na badala yake kuwaona kama ni watoto wao wa kawaida kama ilivyo kwa watoto wasio na ulemavu.


Akisoma risala ya wanajumuiya hiyo, mwanafunzi Mariyam Saleh Mohammed, aliwataka waislamu kuunganisha nguvu zao za pamoja kwa lengo la kupata vijana waliobora nchini.


Akizungumzia changamoto zinazowakabili wanajumuiya hiyo, ni uchakavu wa madara, hali duni kwa walimu wa madrasa waliyonayo, pamoja na fursa finyu ya kuwaendeleza vijana wao.


Alizitaja changamoto nyengine kuwa, ni ukosefu wa vifaa vya ofisi ya jumuiya hiyo, pamoja na udhamini wa wafadhili katika mashindano ya wanawake, kwani wafadhili wengi wamekuwa wakielekeza nguvu zao katika masuala ya mpira jambo ambalo ni gumu kwao
 

0 comments:

 
Top