Baraza la Taifa la Watu Wenye ulemavu Zanzibar limetakiwa kuweka utaratibu mzuri ili kuhakikisha upatikanaji wa fursa sawa kwa wenye ulemavu walioko mijini na vijijini. 

Akifungua warsha ya Baraza hilo iliyofanyika hoteli ya Ocean View kilimani, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Fatma Abdulhabib Ferej amesema mara nyingi jamii imejengeka kuwapatia fursa watu walioko mijini na kuwasahau walioko vijijini, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita, ili fursa ziweze kutolewa kwa wote. 

Amesema wakati umefika sasa kuwajengea mazingira bora watu wenye ulemavu, ili kuhakikisha kuwa wanakuwa salama dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi, matumizi ya dawa za kulevya na elimu kuhusu mazingira. 

Kwa upande mwengine amesema baraza hilo ambalo hukutana kila baada ya miezi mitatu, lina jukumu la kuishauri serikali ili iweze kutekeleza mahitaji ya watu wenye ulemavu kulingana na rasilimali zilizopo, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa fursa za ajira na elimu katika taasisi za umma na zile za binafsi. 

Aidha amesema baraza pia lina wajibu wa kuhakikisha kuwa maslahi ya watu wenye ulemavu yanapewa kipaumbele katika mipango yao. 

Amewakikishia wajumbe wa baraza hilo kuwa Ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa karibu na baraza hilo ili kurahisisha utekelezaji wa majukumu iliyojipangia. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Watu wenye Ulemavu Zanzibar Bi. Abeida Rashid amesema lengo la warsha hiyo ni kuwajengea uwezo wajumbe wa baraza hilo ili waweze kutekeleza majukumu yao vizuri.

Raya Hamad, OMKR.

0 comments:

 
Top