Kikao cha kawaida cha kamati ya pamoja kati ya Viongozi na wataalamu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kimekutana kujadili changamoto mbali mbali zinazoleta kero katika masuala ya Muungano.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Mohd Gharib Bilal alikiongoza kikao hicho akiambatana na Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo katika Ukumbi wa Dodoma Hoteli Mjini Dodoma.
Akiwasilisha masuala yaliyofanyiwa kazi kufuatia agizo la kikao kilichopita Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamuhuri anayeshughulikia masuala ya Mauungano Mh. Samia Suluhu Hassan alisema ipo hatua kiasi iliyofikiwa katika kushughulikia masuala hayo zikiwemo zile kero zinazoleta changamoto ndani ya Muungano.
Waziri Samia aliyataja masuala hayo kuwa ni pamoja na Ushirikia wa MIRADI YA Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, suala la mafuta na Gesi kutolewa katika mamabo ya Muungano, Ushirikiano wa Zanzibar na Taasisi za nje katika mfumo wa uhusiano wa Kimataifa, Uvuvi wa Bahari kuu pamoja na Ajira za utumishi wa wafanyakazi wa Zanzibar katika Taasisi za Muungano.
Alisema majadiliano ya wataalamu na viongozi teule wa pande zote mbili katika masuala ya Mafuta na Gesi pamoja na lile la Uvuvi wa Bahari kuu yemechelewa kutokana na ufinyu wa bajeti za vikao hivyo.
Hata hivyo alifahamisha kwamba hatua za majadiliano hayo zitaendelea ndani ya kipindi cha miezi miwili inayofuata kwa vile mfuko wa kuratibu vikao hivyo tayari umeshapatikana.
Naye Naibu Waziri wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mh. Abdulla Juma Abdulla akizungumzia suala la ushiriki wa Miradi ya Zanzibar ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki alisema Jumuiya ya Afrika Mashariki inasubiri uchambuzi yakinifu katika miradi ya Bandari ya mpiga Duri Unguja, Uwanja wa ndege wa Pemba pamoja na Chelezo cha Malindi Unguja.
Mh. Abdulla alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika { ADB } kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki imekusudia kusaidia mradi wa Bandari ambao tayari makampuni matatu ya kimataifa yalijitokeza kufanya uchambuzi huo.
Kwa upande wake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amewapongeza Viongozi na watendaji wa pande zote kwa juhudi wanazoendelea kuchukuwa za kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya Kamati hiyo.
Balozi Seif alisema akiwa kama mtendaji mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amekuwa na mawasiliano ya kirafiki zaidi kati yake na Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Mizengo Peter Pinda wakati inapotokea hitilafu ya utendaji baina ya pande hizo mbili.
“ Tumekuwa tukiwasiliana na kushirikiana kwa karibu zaidi kama ndugu mimi na Waziri Mkuu Mh. Pinda wakati yanapojitokeza matatizo ya utekelezaji wa majukumu katika pande zetu mbili. Na hili wakati mwengine tunalazimika kuwasiliana kwa simu wakati wowote hata kama usiku “. Alisisitiza Balozi Seif.
Akikiahirisha kimao hicho cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanziabr Makamu wa Rais wa Muungano Dr. Mohd Gharib Bilal amewaasa Watendaji wa pande zote mbili kuhakikisha kwamba wanakuwa makini wakati wote katika kukabiliana na changamoto zinazojichomoza katika masuala ya Muungano.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment