Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeupongeza Uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } kwa hatua zake kubwa ilizoonyesha katika kusaidia maendeleo ya Kiuchumi na kijamii hapa Zanzibar.

Pongezi hizo zimetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika hafla fupi ya uzinduzi wa ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } awamu ya kwanza uliopata ufadhili mkubwa kutoka kwa Benki hiyo ya Badea hapo Tunguu Mkoa wa Kusini Unguja.

Baloz Seif ambae alimuwakilisha Rais wa Zanzibar kwenye uzinduzi huo alisema Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } imekuwa mshirika mkubwa wamaendeleo wa Zanzibar hasa katika sekta ya Elimu hatua ambayo inaijengea mazingira ya mfumo mzuri wa miundo mbinu ya Kielimu hapa Zanzibar.

Alisema sekta ya Elimu ni moja kati ya mambo yaliyopewa msukumo mkubwa ndani ya dira ya maendeleo ya Zanzibar ya 2020 katika muelekeo wa kuwajengea uwezo wa Kielimu vijana wanapomaliza masomo yao wakubalike kuingia moja kwa moja katika soko la ajira.

“ Chuo chetu Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } tunakusudia kukijengea uwezo mkubwa zaidi utakaowapa fursa pana wanafunzi wetu kuingia katika soko la ajira sio Tanzania na Afrika Mashariki bali popote pale Duniani “. Alifafanua BaloziSeif.

Balozi Seif alisisitiza kwamba licha ya ongezeko kubwa la idadi ya watu liliopo hivi sasa Nchini lakini bado Serikali imejikita kuongeza Skuli zaidi nyengine za Sekondari Unguja na Pemba kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuwajengea mazingira bora wanafunzi yatakayowawezesha kupata fursa ya uhakika ya kujiunga na vyuo vya Elimu ya juu.

Akitoa salamu za Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser Ibrahim Albassam alisema ujenzI wa vyuo Vikuu ni moja ya hatua nzuri kwa Taifa lolote katika kuelekea kwenye maendeleo ya uhakika.

Mhandisi Albassam ambe pia ni Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Saudi Arabia alisema Benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo za Zanzibar.

Alisema kupitia Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Hiyo Mhandisi Albassam alieleza kwamba Uongozi wa Benki hiyo umeahidi kusaidia tena Dola za Kimarekani Milioni kumi { U$ Dolla 10,000,000 } kwa ajili ya kuendeleza awamu ya pili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar { SUZA } katika Kampasi yaTunguu.

“ Tumefarajika na ukarimu wa watu wa Zanzibar na mazingira yake mazuri yaliyopelekea kuushawishi Uongozi wa Benki yetu ya Badea kusaidia Sekta ya Elimu, Bara bara na Nyanja nyengine za maendeleo “. Alisisitiza Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi ya Badea Mhandisi Albassam.

Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUSA } Profesa Idriss Rai alisema ujenzi huo umeongeza program nyengine na kufikia nane kutoka Nne kutokana na mabadiliko ya mahitaji Kiuchumi sambamba na Kijamii hapa Nchini.

Profesa Rai alizitaja baadhi ya program hizo kuwa ni pamoja na masomo ya Sayansi ya mazingira ,Biashara, Utalii na Kilimo pamoja na kuanzishwa kwa vituo viwili vya utafiti vya mazingira na Kiswahili.

Makamu Mkuu huyo wa Suza alifahamisha kwamba muelekeo wabadae wa chuo hicho kikuu cha Taifa cha Zanzibar ni kukiwezesha kuhudumia wanafunzi kutoka kanda ya Afrika Mashariki na maeneo mengine ya mbali.

Alieleza kuwa hatua hiyo imekuja kufuatia Zanzibar kubarikiwa kuwa na bahati ya kupokea wanafunzi wengi kutoka sehemu mbali mbali nje ya Tanzania kwa ajili ya kujakujifunza hasa masuala ya lugha.

“ Tutalazimika kujikita pia katika kuwajengea mazingira bora ya makazi wanafunzi wetu hasa wale wa kigeni na hili linahitaji pia kuungwa mkono na wadau wetu wa elimu “. Alieleza Profesa Rai.

Akimkaribisha mgeni rasmi katika uzinduzi huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mh. Ali Juma Shamhuna alisema msaada wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } umechangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha awamu ya kwanza ya mradi huo.

Katika ujenzi huo wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar { SUZA } awamu ya kwanza Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { Badea } imechangia Dolla za Kimarekani Milioni 5.6 wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetoa Shilingi za Kitanzania Bilioni 5.5.

Wakati huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alikutana kwa mazungumzo na Ujumbe wa Benki ya Maendeleo ya Kiislamu { BADEA } hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo hayo Balozi Seif aliueleza Ujumbe huo unaoongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser Ibrahim Albassam kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itahakikisha awamu ya pili ya Ujenzi wa Chuo Kikuu cha Suza unaanza mara moja.

Alisema uungaji mkono wa Uongozi wa Benki hiyo kwenye ahadi iliyotolewa katika uzinduzi wa kwanza umekuwa chachu ya maandalizi ya awamu inayofuatia .

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki hiyo Mhandisi Youser Ibrahim Albassam alisema Badea daima itaendelea kusaidia Mataifa machanga katika kujinasua kiuchumi ikilenga zaidi Mataifa ya Bara la Afrika.

Othman KhamisAme

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top