Wanawake nchini wamehimizwa kuvuliana na kuaminiana katika kuendeleza shughuli zao za ushirika.

Wito huo umetolewa na Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mama Awena Sinani Massoud kwa nyakati tofauti, wakati akiangalia mandeleo ya vikundi vya akinamama katika Mkoa wa Kaskazini Pemba. 
 
Amesema hali ya kuvuliana na kuaminiana ni nyenzo muhimu ya kuendeleza vikundi vya ushirika, na kuwataka waliopewa dhamana ya kuongoza katika vikundi hivyo kuwa waadilifu.

Pia Mama Awena amekemea tabia ya ubaguzi katika kuendeleza vikundi hivyo, na kuwasisitiza kuwa kitu kimoja na kushirikiana bila ya kujali itaikadi za vyama, dini au eneo.

Ameelezea kufurahishwa kwake na hatua zilizochukuliwa na akinamama hao katika kujikwamua kiuchumi, na kuwashajiisha kuongeza juhudi katika kujiletea maendeleo.

Katika ziara hiyo Mama Awena ametembelea vikundi vya maendeleo ya wanawake kikiwemo kikundi cha Fahari kinachojishughulisha na kazi za mikono na utengenezaji wa sabuni, na kikundi cha “Gando Livestock and Snacks Producers” kinachojishuhulisha na mapishi ya vyakula.

Amewahimiza akinamama hao kuzihifadhi vizuri bidhaa wanazozizalisha, ili kuvutia wateja na kuweza kukabiliana na ushindani wa soko.

“packing au uhifadhi ni muhimu sana katika kuuza bidhaa zenu, bila ya kuwa na uhifadhi mzuri bidhaa zinaweza kudoda hata kama zina ubora kiasi gani, kwa hiyo hizo packing zinazidisha ubora wa bidhaa zinapoingia sokoni”, alisisitiza Mama Awena.

Amefahamisha kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kuleta maendeleo ili wataamua kufuta ile dhana ya kuwa mwanamke ni mtu wa kukaa nyumbani tu na kusubiri kuletewa kila kitu.

Katika risala ya kikundi cha Fahari iliyosomwa na katibu wake Bi. Maryam Mbarouk, akinamama hao wamesema malengo yao ni kuzalisha bidhaa tofauti na kuongeza ubora wa bidhaa hizo.

Amesema pia wamekusudia kuongeza ajira binafsi ili kuipunguzia mzigo serikali dhidi ya wazururaji na kuwawezesha wanakikundi hao kujiongezea kipato .

Hata hivyo amesema wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa masoko, upatikanaji wa mali ghafi na vifaa vya kisasa vya kufanyia kazi.

Hivyo wameiomba Wizara ya Kazi, Uwezeshaji wananchi kiuchumi na Ushirika kuwapatia wataalamu ili kuweza kujifunza zaidi na kufanya kazi zao kwa uhakika na zenye ubora zitakazoweza kuendana na soko la kibishara.

Na. Mauwa Mohd-Pemba.

0 comments:

 
Top