Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa ambae pia ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Jakaya Mrisho Kikwete amesema siri kubwa kwa Wabunge kuendelea kuungwa mkono Majimboni ni kuwa karibu na Wananchi pamoja na kutekeleza ipasavyo Ilani na ahadi walizozitoa wakati wa kampeni za uchaguzi.

Dr. Kikwete amesema hayo wakati akiifungua Semina ya Wabunge wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Tawala cha Mapinduzi iliyofanyika katika Ukumbi wa Makao Makuu ya Chama hicho { White House } uliopo Mkoani Dodoma.

Alisema yapo matatizo kadhaa yanayowasumbua wananchi katika maeneo yao ambayo baadhi yake yaliahidiwa na baadhi ya Wabunge wakati wakiomba ridhaa ya kuwaongoza lakini matokeo yake huleta balaa ndani ya chama kwa kukosa kutekelezwa na wabunge hao.

Dr. Kikwete alifahamisha kwamba wabunge hao wakiamua kutekeleza vyema ilani na ahadi hizo wanajengea uwezo zaidi wa kuendelea kuungwa mkono na wananchi wao kitendo ambacho hata idadi ya watu wanaoamua au kutaka kuomba nafasi hiyo wakati wa uchaguzi inakuwa ndogo.

“ Hakuna kitu kinachomuangusha vibaya Mbunge katika wadhifa wake isipokuwa ile tabia ya kutowatembelea Wananchi wa jimbo lake hali inayosababisha wananchi hao kuwa na maswali mengi ya kumuuliza hasa ule wakati anapokwenda tena kuomba kura “. Alisisitiza Dr. Kikwete.

“ Kama Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi haijatekelezwa vyema Majimboni inaweza kuleta balaa katika maeneo hayo hata ndani ya Chama chenyewe. Hivyo tunapaswa kuwa na hadhari na suala hilo “ Alieleza Dr. Kikwete.

Aliwataka Wabunge hao kuhakikisha wanaziorodhesha ahadi zote zilizotolewa na Wagombea Urais, Ubunge, Uwakilishi na hata Udiwani wakati wa kampeni ndani ya Majimbo yao ili kujenga mikakati ya pamoja na kuzikamilisha ahadi hizo.

“ Tuko kati kati ya safari yetu tuliyoianza Oktoba Mwaka 2010 hadi mwaka 2015 tukiwa na lengo moja tuu la kukijengea mazingira ya ushindi wa chaguzi zote Chama cha Mapinduzi “. Dr. Kikwete aliwakumbusha Wabunge hao.

Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa alisisitiza kwamba masuala mapya yanayowakereketa wananachi ndani ya majimbo yao pia yanapaswa kuainishwa na hatimae kuangalia mbinu za kuyatekeleza kadri hali itakavyoruhusu.

Dr. Kikwete aliwataka Wabunge hao wa CCM kuendelea kuwashawishi wananachi katika majimbo yao kuwaunga mkono ili kupata nguvu za kutekeleza vyema majukumu yao.

Aliiwaasa baadhi ya Wabunge wenye tabia ya kuwazuia wanachama wengine wasigombee nafasi hiyo kuacha mfumo huo ambao unawanyima haki wanachama hao pamoja na wananachi kumchagua Yule wanayeridhika naye.

“ Hakuna namna ya kuwazuia watu wasigombee uongozi wala wanachama kuchaguwa Viongozi wawapendao tena kwa uhuru na uwazi “. Alifafanua Dr. Jakaya Mrisho Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa Taifa wa CCM aliwapongeza Wabunge hao wa Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza vyema wajibu wao ndani ya Vikao vya Bunge licha ya baadhi ya Wabunge wa upande mwengine kufanya vioja vinavyoleta maswali mengi miongoni mwa wananchi.

Aliwataka wabunge hao kuendelea kuikosoa Serikali katika utaratibu na mazingira bora ya kujenga kwa lengo la kuwapa matumaini wananachi waliowachagua.

Mapema akitoa Taarifa fupi ya Kamati ya Wabunge hao wa CCM Katibu wa Kamati hiyo Mh. Jenister Muhagama alisema utendaji wa kazi za Wabunge wa CCM ndani ya Vikao vya bunge imekuwa mfano kwa Viongozi wengine wa Kisiasa hapa Nchini.

Mh. Jenister alisema nidhamu ya Wabunge wa CCM ndani ya Bunge itaendelea kuimarika siku hadi siku licha ya baadhi ya wenzao hivi sasa kuihamishia siasa kutoka majimboni hadi ndani ya Vikao hivyo.

Mh. Jenister Muhagama kwa niaba ya Wabunge wenzao wamelaani vitendo vinavyoashiria sura ya ugaidi ambavyo vinaonekana kuinyemelea amani iliyopo Nchini ambayo inaweza kutoweka mara moja iwapo hakutakuwa na juhudi za pamoja za kudhibiti matendo hayo.

Katibu huyo wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi Mh. Muhagama aliiomba Serikali kuu kujizatiti katika kukabiliana na vitendo hivyo kwa kuwadhibiti wahusika wa matendo hayo sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria.

Othman Khamis Ame 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top