Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, amewahimiza wazazi, walezi na walimu kushirikiana kutika kurejesha maadili na malezi bora kwa watoto.

Maalim Seif ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya maulid ya Mtume Muhammad (SAW), yaliyoandaliwa na Madrasat Ghulam Islamia ya Muembe Makumbi mjini Zanzibar.

Amesema maadili ya kiislamu na malezi bora kwa watoto yanaweza kurejeshwa iwapo jamii itakubali kushirikiana katika malezi, sambamba na kushajiisha elimu ya madrasa kwa vijana.

“Sisi wakati wetu mtoto alikuwa akilelewa na jamii nzima, yaani kama mtoto akikosea au kuondosha nidhamu na heshima kwa mzee mwengine basi alikuwa na uwezo wa kumrudi mtoto yule, na akienda kushtaki kwao basi mzazi wake atamuongeza kutokana na kosa hilo, lakini leo wapi, mambo yamebadilika”, alieleza Maalim Seif huku akitoa historia ya malezi ya zamani.

Aidha amesifu juhudi za walimu wa madrasa katika kuwaendeleza watoto kitaaluma, licha ya kukabiliwa na mazingira magumu, na kuwataka walimu hao kujipanga katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa mishahara.

Amewataka wazazi na walezi wa wanafunzi kuthamini mchango wa walimu wa madrasa kwa maendeleo ya watoto wao, na kushajiika kuchangia ili kuwawezesha walimu hao kufanya kazi zao vizuri.

Akizungumzia kuhusu Umoja wa Wazanzibari Maalim Seif ametoa wito kwa wananchi kushikamana na mafunzo ya dini katika kuendeleza umoja na mshikamano ili kulinda umoja uliopo.

Amefahamisha kuwa umoja huo umeijengea heshima kubwa Zanzibar kitaifa na kimataifa, sambamba na kurejesha umoja wa Wazanzibari uliokuwa hatarini kwa kipindi kirefu.

Maalim Seif pia alitumia fursa hiyo kuwatanabahisha wananchi juu ya athari za uchafuzi wa mazingira na utumiaji wa dawa za kulevya.

“Serikali haijazuia uchimbaji wa mchanga lakini imeweka utaratibu maalum na kuruhusu baadhi ya maeneo. Lengo letu ni kulinda mazingira yetu yasiathirike kwa faida zetu wenyewe ikizingatiwa kuwa nchi yetu ni kisiwa na ardhi inapungua kila siku huku idadi ya watu ikiongezeka kila mwaka”, alitanabahisha Maalim Seif.

Katika risala yao iliyosomwa na ustadh Amour Mgeni, madrasa hiyo yenye wanafunzi wapata 150 imesema imepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2009, ikiwa ni pamoja na kuweza kujenga jengo la madrasa hiyo.

Hata hivyo wamesema jengo hilo kwa sasa limekuwa dogo kulingana na idadi ya wanafunzi, na kuwaomba watu wenye uwezo kusaidia upanuzi wa madrasa hiyo, sambamba na kuipatia vikalio na vitendea kazi vya kisasa.

Hassan Hamad (OMKR).

0 comments:

 
Top