Uchumi wa Mataifa machanga yanayolenga kuelekea kwenye maendeleo ya haraka utazidi kuimarika iwapo Mataifa hayo yatajikita zaidi katika matumizi ya Mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano ya moja kwa moja kati yao au hata kushirikiana pamoja na yale Mataifa yaliyoendela.
Hayo yaliibuka wakati wa mazungumzo kati ya Ujumbe wa Kampuni ya Vifaa vya Teknolojia ya Mawasiliano { Zhong Xing Telecommunication Equipment } {ZTE } yenye Makao Makuu yake Nchini China ulioongozwa na Makamu wa Rais wa Kampuni hiyo Bwana Chen Jinsong pamoja na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Bwana Chen Jinsong ambae Kampuni yake ya ZTE ndiyo inayojenga na kusimamia mradi wa Mkongo wa Taifa hapa Zanzibar alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuwa mfumo huu wa mawasiliano hutoa fursa kwa wataalamu wa pande mbili walio Nchi tofauti kufanya kazi pamoja kwa kutumia mtandao wa kisasa wa mawasiliano ya Teknolojia.
Alifahamisha kwamba hatua za Kiuchumi , Biashara, Afya pamoja na harakati za maisha ya Jamii za kila siku zina nafasi na fursa nzuri ya kutumia Mtandao wa Serikali { E. Government } wakati utakapokamilika matengenezo yake Mfumo huo.
“ Uwezo wa Wataalamu mfano wa sekta ya Afya unaweza kukua mara dufu kwa kushirikiana katika masuala ya mikutano { Group Discution } na hata baadhi ya operesheni za wagonjwa wakiwa nchi tofauti kwa kutumia mitandano ya Kisasaya Teknolojia “. Alifafanua Makamu wa Rais huyo wa Kampuni ya ZTE.
Bwana Chen alieleza kwamba katika kuunga mkono Mataifa ya Bara la Afrika kuingia katika mfumo huu wa mawasiliano ya Kisasa ya Teknolojia Uongozi wa Kampuni yake umeshaanza kusambaza huduma zake katika Baadhi ya Mataifa hayo ya Bara la Afrika.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Zhong Xing Telecommunicationa Equipement tayari imeshafungua Ofisi yake Nchini Tanzania likiwemo pia tawi lake moja hapa Zanzibar.
Alisisitiza kwamba miradi inayoanzishwa na Kampuni hiyo mbali ya kuongeza ushirikiano na Mataifa hayo lakini pia umelenga kusaidia kutoa ajira kwa wazalendo walio wengi kwenye Mataifa hayo rafiki.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema mradi mkubwa ulioanzishwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa Mtandao wa Serikali { E. Government } chini ya Kampuni hiyo ya ZTE utaisaidia kuirusha Zanzibar kuingia katika mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano Duniani.
Balozi Seif aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo ya ZTE kwa kusimamia kukamilisha awamu ya kwanza ya mradi huu wa Mtandao wa Serikali hapa Zanzibar hatua ambayo itazidi kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Jamuhuri ya Watu wa China.
“ Tunashukuru na kufarajika kuona kwamba Nchi zetu mbili Zanzibar na China bado zinaendelea kushirikiana kwa karibu miaka 50 sasa mara tuu baada ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 “. Alisisitiza Balozi Seif.
Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Mwenyekiti wa Kampuni inayoendesha Miradi ya Hoteli za Kimataifa Afrika Mashariki iitwayo Mada Hotels yenye Makao Makuu yake Mjini Nairobi Nchini Kenya Bwana Tinu Mhajan.
Bwana Tinu Mhajan ambae amefika Zanzibar kuangalia uwezekano wa Kampuni yake kutaka kuwekeza Vitega uchumi vyake hapa Zanzibar katika maeneo ya Hoteli alisema Utalii utaendelea kukua na kuimarika kwa kupitia mfumo wa kubadilisha vivutio vitakavyowapa ushawishi zaidi watalii kupenda kutembelea eneo hili.
Mwenyekiti huyo wa Kampuni ya Mada Hotels alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kwamba Taasisi yao imelenga kutoa huduma zake ndani ya Ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar bado ina fursa nzuri za uwekezaji katika maeneo ya Utalii ambayo Mada Hotels inaweza kuzitumia ipasavyo fursa hizo.
Balozi Seif alimfahamisha Mwenyekiti huyo wa Mada Hotels kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeipa kipaumbele sekta ya Utalii ili isaidie uchumi wa Taifa ambao hadi sasa unategemea zaidi zao la Karafuu.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
0 comments:
Post a Comment