Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wakulima kisiwani Pemba kuyatumia mafunzo wanayopewa katika kujiongezea ufanisi wa shughuli zao.

Akizungumza wakati akitoa majumuisho ya ziara yake ya siku mbili katika Wizara ya Kilimo na Maliasili kwenye ukumbi wa kituo cha mazunzo ya Amali Fidel Castro, Maalim Seif amesema mafunzo hayo yanayotolewa kwa wakulima pamoja na utafiti shirikishi ni miongoni mwa juhudi za serikali katika kuwakomboa wakulima.

Amesema iwapo mafunzo hayo yatatumika vizuri, yatawasaidia wakulima kuweza kulima kilimo cha kisasa, kutumia mbegu bora na pembejeo kama inavyotakiwa.

Amepongeza juhudi za Wizara ya kilimo katika kuwashirikisha wakulima na wafugaji katika utafiti wa mazao mbali mbali, hatua ambayo inakuza uelewa kwa wakulima na kuweza kuongeza kipato chao.

Hata hivyo amesema Wizara ya Kilimo bado inakabiliwa na upungufu mkubwa wa wafanyakazi hasa mabwana na mabibi shamba, hali inayopelekea mtendaji mmoja kuhudumia hadi shehia tatu.

Katika majumuisho hayo Maalim Seif ameigiza Wizara hiyo kufanya utafiti wa pembejeo na mahitaji ya wakulima kwa kila shehia ili kuwawezesha wakulima kupata mahitaji kamili, sambamba na kusambaza matokeo ya tafiti za kilimo kwa wakulima wote.

Kwa upande mwengine Maalim Seif ameitaka Wizara ya kilimo kufikiria namna ya kuirejesha miti ya asili ikiwemo mifuu na mizambarau, ili kuirejeshea Zanzibar hadhi yake ya kuwa nchi ya kijani.

Kuhusu misumeno ya moto, amewataka wananchi kushirikiana kuifichua misumeno hiyo ambayo ni adui wa mazingira na binadamu.

Akiwa katika ziara ya kutembelea shughuli za kilimo Mkoa wa Kusini Pemba, wakulima waliomba kupatiwa mikopo ili waweze kuendeleza shughuli zao kwa uhakika.

Katika Mkoa wa Kusini Pemba ambako pia aliambatana na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mtumwa Kheri Mbarak na Katibu Mkuu Affan Othman Maalim, alitembelea maendeleo ya shmaba darasa la wakulima wa migomba Kuukuu Kangani, vitalu vya mikarafuu Mjimbini na Chanjaani pamoja na uzalishaji wa mbegu za muhogo Mfikiwa Chake chake.



Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top