Sheha wa Shehia ya Tomondo Wilaya ya Magharibi Bwana Mohd Omar Said { Maarufu Kidevu } anaendelea kupatiwa huduma za matibabu katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa Tindi kali { Acid } na mtu asiyejuilikana.

Mkasa huo umempata jana usiku mara baada ya kurejea ibada ya sala ya Isha wakati akiendelea na harakati za kutafuta huduma za maji na kumwagiwa tindi kali hiyo iliyoathiri eneo la kifua chek, Bega pamoja na sehemu za jicho la kulia.

Hili ni tukio la tatu kutokea ndani ya mkoa wa mjini Magharibi likiwahusisha aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa Ndugu Rashid Ali Juma pamoja na Katibu wa Fufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Fadhil Suleiman Soraga.

Sheha huyo wa Tomondo Bwana Mohd Omar Kidevu akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliyefika Hospitali hapo kumfariji pamoja na kumpa pole alisema alijikuta akimwagiwa tindi kali majira ya saa 2.00 za usiku na mtu asiyemfahamu.

Bwana Mohd Kidevu alisema Mtu huyo alianza kutimua mbio baada ya kufanikiwa kufanya dhambi hiyo kitendo ambacho akalazimika kuomba msaada kwa wasamaria wema lakini hatimae ilishindikana kutokana na kuzidiwa kwa maumivu makali yenye kuchoma kama moto.

Sheha huyo wa Shehia ya Tomondo aliendelea kumfahamisha Balozi Seif kwamba hali yake hivi sasa inaendelea vyema na ameshaanza kupata matumaini kufuatia jicho lake kuanza kuona ingawa bado anakabiliwa na maumivu katika sehemu yake ya usoni.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alimuomba Sheha huyo wa Tomondo kuwa na moyo wa subra wakati wa kipindi hichi kigumu cha huduma za matibabu.

Balozi Seif alimuhakikishia Bwana Mohd Kidevu kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kufuatilia ushauri utakaotolewa na Madaktari kuhusu tiba ya afya yake na kutoa msaada wowote utakaohitajika ili kuendeleza nguvu za huduma ya tiba yake.

“ Tutafuatilia ushauri watakaotupa Madaktari kuhusu afya yao. Na kama kuna wazo la kukusafirisha iwe Hospitali ya Rufaa Muhimbili au Nje ya Nchi basi sisi kama Serikali tuko tayari kulitekeleza hilo “. Balozi Seif alimuhakikishia Sheha Mohd Kidevu.

Akizungumza na vyombo vya Habari nje ya Wodi ya Mapinduzi Kongwe katika Hospitali Kuu ya Mmnazi Mmoja Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali Kuu imesikitishwa na vitendo hivi viovu vinavyoleta athari kwa Binaadamu.

Balozi Seif alisema tabia hii mbaya inayoonekana kuanza kuchipua hapa Nchini ikibeba ufinyu wa imani inaanza kuleta hofu miongoni mwa wananchi katika kuendelea na harakati zao za kimaisha za kila siku.

Alisema Serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi itaendelea na uchunguzi wa kufuatilia matukio hayo na haitasita kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuwafikisha katika mkondo wa sheria.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top