Kamati ya kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa imeelezea kusikitishwa kwake na tabia ya baadhi ya watendaji wa Serikali kuendelea kudharau Maagizo yanayokuwa yakitolewa na Viongozi Wakuu wa Serikali katika Taasisi na maeneo tofauti Nchini.

Wajumbe wa Kamati hiyo waliokuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wake Mh. Saleh Nassor Juma Mwakilishi wa Jimbo la Wawi walieleza hayo wakati wakizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi mara baada ya kukutana na Uongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupokea Taarifa ya utendaji ya Ofisi hiyo.

Walisema wamekuwa wakishuhudia uzorotaji mkubwa wa kusimamia maagizo hayo hasa katika masuala ya migogoro ya ardhi jambo ambalo huendelea kuleta malalamiko kwa wananchi wanaokumbwa na matatizo ya migogoro hiyo.

Walieleza kwamba baadhi ya watendaji hao wa Serikali wamekuwa wakionyesha chuki za wazi dhidi ya Waheshimiwa wakati wanapofuatilia au kulalamikia utendaji mbovu.

Walifahamisha kwamba wao sio polisi bali wanachokifanya ni kutekeleza majukumu waliyopangiwa ndani ya Kamati zao ambazo zimeteuliwa kwa mujibu wa taratibu na Kanuni za Baraza la Wawakilishi lililoundwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar kusimamia utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Wajumbe hao wameipongeza Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake ambayo yameleta faraja kwa Kamati hiyo na kusisitiza kuendelezwa kwa ushirikiano wa sehemu zote mbili ili lile lengo la kuwahudumia Wananchi lifanikiwe vyema.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa ndiye Mtendaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar aliwakumbusha Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa wakali wanapotekeleza wajibu wao wa kila siku.

Balozi Seif alisema Kamati za Baraza la Wawakilishi zimeundwa kwa lengo la kufuatilia mwenendo wa shughuli za Serikali katika Taasisi zake ili zishauri, zikosoe na hata kuelekeza njia ya kuleta ufanisi utakaostawisha na kunufaisha Jamii Nchini.

“ Hili suala la kufuatilia maagizo yanayotolewa na Viongozi wakuu wa Serikali limo ndani ya mamlaka yenu na kamwe hakutakuwa na kiongozi mwengine atakayekuwa na mamlaka ya kujipangia utekelezaji huu “. Alisisitiza Balozi Seif.

Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alifanya ziara fupi ya kukagua matengenezo ya majengo ya Kiwanda cha Idara ya Mpiga chapa Mkuu wa Serikali kinachotarajiwa kuhamia hapo Maruhubi Nje kidogo ya Mji Zanzibar.

Uamuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wa kukihamisha Kiwanda hicho hapo Mtaa wa Mkele na kuhamia Maruhubi umekuja kufuatia kiwanda hicho baadhi ya wakati kufungwa kutokana na mashine zake kuharibika kwa sababu ya mafuriko ya maji wakati wa msimu wa mvua za masika.

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Ndugu Mohd Mzee alimueleza Balozi Seif kwamba matengenezo ya majengo hayo chini ya Kampuni ya Kimataifa ya CRJ ya Nchini China yalipangwa kukamilika mwezi huu lakini yatachelewa kidogo kutokana na ufinyu wa bajeti yake.

Hata hivyo Ndugu Mzee alifahamisha kwamba Kampuni ya CRJ imethibitisha kwamba upatikanaji wa fedha za kukamilishia matengenezo yaliyobaki zikipatikana kwa wakati harakati hizo zinaweza kuchukuwa muda miezi miwili au mitatu kuanzia sasa.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohammed Aboud Mohammed alisema matengenezo ya majengo hayo ya Kiwanda cha Idara ya Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali yanatarajiwa kugharimu jumla ya Shilingi Bilioni mbili kutoka Mfuko Mkuu wa Serikali.

Wakati huo huo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikutana na Uongozi wa Kampuni ya Mafuta Tanzania { State Oil Tanzania } ukiongozwa na Bwana Bjorn Rasmussen hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Katika mazungumzo yao Uongozi huo wa mafuta ambao umekuwa ukiendesha mafunzo mbali mbali ya uhifadhi wa mazingira kwa kushirikisha wadau wa mafuta na wana taaluma wa vyuo vikuu Nchini umekuwa ukisisitiza umuhimu wa suala hilo.

Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Mafuta Tanzania Bwana Bjorn alifahamisha kwamba harakati za miradi ya mafuta na gesi hufanikiwa vyema na kuleta faida kubwa pale wahusika na wadau wakuu wa sekta hiyo wanapozingatia vyema msingi mkuu wa mazingira.

Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliitahadharisha jamii nchini kufahamu kwamba rasilmali yoyote inayopatikana popote pale huwa ni ya taifa na wala si ya wakaazi wa eneo husika pekee.

Balozi Seif alieleza kwamba upo ufinyu wa mawazo kwa baadhi ya wananchi kuhisi kuwa rasilmali inayopatikana katika maeneo yao haiwahusu wananchi wengine jambo ambalo ni kosa.

Othman Khamis Ame. 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top