Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema bado Makampuni na Taasisi mbali mbali za Ndani na nje ya Nchi zina fursa ya kuwekeza katika sekta za Maji na nishati ili Zanzibar iwe na uhakika kamili wa kujitosheleza kwenye mahitaji ya sekta hizo muhimu.

Alisema licha ya baadhi ya makampuni na taasisi tofauti kujitokeza kuonyesha nia hiyo lakini mlango uko wazi kwa washirika wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono hatua hiyo.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji salama yenye makao yake makuu Nchini Qatar mazungumzo yaliyofanyika hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Aliueleza Ujumbe huo unaoongozwa na Meneja Mkuu wake Bwana Adnan Harb kwamba Zanzibar inahitaji kuwa na vianzio vingi vya nishati ya umeme kwa vile imelenga kujiimarisha zaidi katika sekta ya viwanda pamoja na miji mipya.

Balozi Seif alifahamisha kwamba Zanzibar hivi sasa ina kianzio kimoja tuu cha umeme wakati mahitaji ya huduma hiyo yanabadilika kila mara kutokana na ongezeko la miradi ya kiuchumi kama Hoteli na Biashara ambayo yote hiyo inakwenda sambamba katika matumizi ya nishati hiyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Kampuni hiyo ya EMEQ kwa kuonyesha shauku ya kutaka kuwekeza miradi yake hapa Zanzibar jambao ambalo litasaidia ushawishi wa uwekezaji katika Visiwa vya Unguja na Pemba.

“ Kwa vile tayari mmeshapata fursa ya kutembelea na kukutana na watendaji wa Wizara zinazohusika na Nishati pamoja na Maji kuelezea fursa mlizonazo katika miradi yenu, nitajitahidi kuhakikisha wahusika hao wanawasiliana na nyinyi ili kufanikisha lengo hilo”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji salama Bwana Adnan Harb alisema Kampuni yao imefanikiwa kuendesha miradi ya umeme wenye uwezo wa kufikia Kilowati 100 ambao hutumia Gesi.

Bwana Adnan alimfahamisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Gesi inayotumika kuzalishia Umeme huo unaouwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka 20 haina sumu katika matumizi yake baada ya kufanyiwa utafiti wa kitaalamu.

Naye Mkuu wa Idara ya uhandisi wa Kampuni hiyo Bwana Ibrahim Raymond Nassar alieleza kwamba Kampuni hiyo imelenga kutoa huduma za kutibu maji ili kuondoa vijidudu vinavyosababisha maradhi mbali mbali.

Bwana Ibrahim alisema dawa maalum za vidonge zimetengenezwa ili kutumika katika miradi hiyo ambayo imekusudiwa kwa jamii iliyokubwa zaidi hasa vijijini ambayo umezo wao ni hafifu kwa kutumia mamlaka zinazohusika na huduma hiyo.

Ujumbe huo wa Kampuni ya Kimataifa inayojishughulisha na masuala ya umeme { emeq } pamoja na huduma za maji salama yenye makao yake makuu Nchini Qatar umekuja Nchini kupitia uratibu wa Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Ras Al- Khaimah Bwana Kamal Ahaya.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top