Viongozi mbali mbali wa vyma vya siasa na serikali wakiongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, wameungana na wananchi Kisiwani Pemba katika mazishi ya Mbunge wa Jimbo la Chambani (CUF), marehemu Salim Hemed Khamis.

Mbunge huyo alifariki dunia jana katika hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla juzi Jumatano wakati akiwa katika kikao cha Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Marehemu Salim Hemed ambaye aliwahi kuwa mwalimu wa skuli, alizaliwa mwaka 1951 katika kijiji cha Chambani na kuhitimu masomo yake ya shahada ya pili katika Chuo Kikuu cha Whales nchini Uingereza, na amezikwa kijijini kwake Mizingani katika jimbo la Chambani.

Akitoa salamu katika msiba huo Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Edward Lowassa, amesema Kamati yake pamoja na Bunge wamepoteza mtu muhimu katika utendaji wa vyombo hivyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF Taifa Prof. Ibrahim Lipumba amesema Chama chake kimepata pigo kubwa kwani marehemu alikuwa mjenga hoja makini na kiungo muhimu baina ya Bunge na Chama chake.

Viongozi kadhaa wa Serikali na vyama vya siasa wakiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge Mhe. Willium Lukuvi na Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Ushirika Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman wamesema marehemu Salim alikuwa mchapa kazi hodari na mtu mwenye busara katika shughuli zake za kiutendaji.

Viongozi wengine walioshiriki mazishi hayo ni pamoja na Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda, Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe. Ali Abdallah Ali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai na Mbunge wa Musoma Mjini (CHADEMA) Mhe. Vicent Nyerere.

Marehemu ameacha vizuka wawili na watoto wanane.
Hassan Hamad (OKMR)

0 comments:

 
Top