Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema haki ya Taasisi au Jumuiya zinazotoa huduma katika maeneo mbali mbali inaweza kupotea kama hakukuwa na mikataba inayolinda pande hizo mbili.

Alisema makubaliano lazima yahemishiwe kwa maandishi vyenginevyo mtoaji au mpokeaji huduma hizo atambue kwamba kinyume cha ukosefu wa mkataba baina yao ni wizi.

Balozi Seif alieleza hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Jumuiya mpya ya Wajasiriamali na usambazaji bidhaa katika Hoteli za Kitalii pamoja na baadhi ya Osifi za umma na hata Binafsi aliokutana nao hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema wakati umefika kwa Taasisi na Jumuiya hizo kuondokana na tabia ya kuaminiana ambayo tayari imeshaonyesha muelekeo mbovu na kuwasababishia usumbufu katika harakati zao za Kibiashara.

“ Kama kuna Taasisi inafanya makubaliano na Jumuiya nyengine ni lazima yawepo maelewano yatakayofuatwa na mkataba wa kimaandishi utaolinda haki ya kila upande”. Alihadharisha Balozi Seif.

Aliueleza Uongozi wa Wajasiriamali hao kwamba Serikali Kuu italitafakari kwa kina tatizo linalowasumbua Wajasiriamali hao la kucheleweshewa malipo yao kunakofanywa na baadhi wanaowapatia huduma hasa Mahoteli ya Kitalii.

Alisema juhudi za dharura zitachukuliwa katika kipindi kifupi kijacho cha kutafuta suluhu ya tatizo hilo kwa kukutana na Watendaji wa Taasisi ya Utalii inayosimamia Sekta hiyo.

Alifahamisha kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilikuwa na nia nzuri ya kukaribisha wawekezaji Vitega uchumi kuwekeza Nchini kwa lengo la kuongeza mapato yao pamoja na ajira zitakazo nyanyua hali za maisha ya wananachi.

Balozi Seif aliwapongeza Wajasiriamali hao kwa uamuzi wao wa kuanzisha Jumuiya yao ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kukabiliana na changamoto zilizowazunguuka.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika kuunga mkono juhudi za Wajasiriamali hao amehidi kuchangia Shilingi Laki 500,000/- kusaidia harakati za ukamilishaji wa mahitaji muhimu ya Ofisi yao iliyopo Jengo la Umoja wa Vijana wa CCM Darajani.

Mapema Katibu wa Jumuiya ya Wajasiriamali na Usambazaji Bidhaa Bwana Ali Abdulla Mohd alisema lengo la kuanzishwa kwa Jumuiya yao limekuja kutokana na Wajasiriamali hao kukumbwa na changamoto kadhaa ikiwemo ile ya ugumu wa kulipwa fedha zao kutoka kwa wadau wao.

Bwana Ali alifahamisha kwamba baadhi ya uongozi wa Hoteli hizo umekuwa ukiwapa wakati mgumu wakati wanapofuata malipo yao na kupelekea wale wanaotoa vitu vya kwa mkopo kufikia hatua ya kutowaamini tena.

Wakichangia baadhi ya Viongozi hao wa Jumuiya ya Wajasiriamali na Usambazaji Bidhaa wameiomba Serikali kuhakikisha inafuatilia changamoto hizo ambazo kama hazikupatia ufumbuzi zinaweza kupunguza ari ya wajasiri amali hao ya kujitafutia ajira na hatime kuibebesha mzigo Serikali Kuu.

Jumuiya hiyo ya wajasiriamali na Usambazaji bidhaa yenye wanachama 150 inajihusisha zaidi ya usambazaji wa bidhaa za Matunda, Mboga Mboga, vyakula vya Baharini pamoja na vifaa vya Ofisini.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar

0 comments:

 
Top