Viongozi wa Jamii popote pale walipo wataendelea kuwa wahimili wa kusimamia malezi na elimu kwa kizazi chao kilichowazunguuka ili kujenga Taifa lenye heshima, Utii, Maadili na nguvu ya uwajibikaji kwa mfumo wa kitaaluma.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati akizungumza na Ujumbe wa Viongozi sita wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Nchini Tanzania { Tamta } uliofika Ofisini kwake Mtaa wa Vuga Mjini Zanzibar.

Balozi Seif alisema suala la kumfinyanga mtoto halihitaji mjadala na litaendelea kuwa jukumu la wazazi kwa kufuata sheria, taratibu sambamba na maamrisho yaliyoelekezwa katika vitabu vya dini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliipongeza Jumuiya hiyo ya Walimu wa Kiislamu Tanzania kwa jitihada zake za kuendeleza elimu ya Dini kwa watoto wa rika tofauti ambazo zinahitaji kuungwa mkono na waumini wengine ndani na nje ya Nchi.

Aliufahamisha Uongozi wa jumuiya hiyo kwamba katika kuunga mkono jitihada zao atajitahidi kuangalia uwezekano wa kuunga mkono hatua yao hiyo kwa kuwashawishi wahisani na washirika wa masuala ya dini kusaidia Jumuiya hiyo muhimu kwa hatma ya Umma wa Kiislamu.

“ Sisi Viongozi ndio wahimili wakubwa wa kusimamia elimu iwe ya dunia au akhera kwa watoto wetu waliotuzunguuka na tukielewa kuwa hii ni dhima inayotukabili wazazi sote”. Alisisitiza Balozi Seif.

Mapema Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { Tamta } Sheikh Mohammed Abdull Dhikri alisema utaratibu wao wa kuendesha sherehe za Madrasa ya Jumuiya hiyo unalenga kuamsha ari na hamasa kwa wanafunzi kuelekea katika kudumu vyema mafunzo yao.

Hata hivyo sheikh Mohammed Abdul Dhikri alisema zipo changamoto kadhaa zinazochangia uendeshaji wa madrasa ya Jumuiya hiyo akazitaja kuwa ni pamoja na uwezeshaji wa walimu wanaojitolea, uchakavu wa majengo pamoja na huduma za Umeme.

Alieleza kuwa katika kukabiliana na changamoto hizo Uongozi wa Jumuiya hiyo pamoja na kujiendesha kwa baadhi ya misaada ya wahisani lakini umelenga kujiendesha wenyewe kwa kuamua kuwekeza katika Kilimo cha alizeti.

Katibu Mkuu huyo wa Tamta amewakumbusha waislamu popote walipo kuandaa mazingira ya kuunga mkono jumuiya hiyo ili lile lengo la kuujenga kitaaluma Umma wa Kiiislamu lipatikane.

Jumuiya hiyo ya Walimu wa Kiislamu Tanzania { Tamta } ifikapo Juni 27 mwaka huu inatarajiwa kuadhimisha miaka 51 tokea kuanzishwa kwake mnamo mwaka 1962.

Othman Khamis Ame
 
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanziba

0 comments:

 
Top