Uchaguzi wa wajumbe watatu watakaounda mabaraza ya katiba ya wilaya kutoka katika kila shehia za Zanzibar ambao watashiriki kwenye mchakato wa kujadili rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania katika Wilaya zao umeendelea tena.

Wananchi wa baadhi ya shehia hizo hapa Zanzibar walionekana kujitokeza katika uchaguzi huo ambapo ratiba zake kwa hapa Zanzibar zilianza mapema Jumamosi ya tarehe 30 mwezi uliopita.

Mbunge wa Jimbo la Kitope ambae pia ni Makamu Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Mkewe Mama Ash Suleiman Iddi walikuwa ni miongoni mwa Wananchi walioshiriki kwenye uchaguzi huo uliokuwa ukiendelea katika shehia za Wilaya ya Kaskazini B katika Kituo chao cha Shehia ya Kitope.

Wagombea waliojitokeza katika Kituo hicho kilichokuwa katika Skuli ya Msingi na Sekondari ya Kitope wakiomba kuchaguliwa kwa nafasi ya Wanawake alikuwa Bibi Abeida Khamis Mohd pekee akiwa hana mpinzani.

Nafasi ya Watu Wazima waliojitokeza ni Mzee Juma Issa Mwangira pamoja na Mzee Abeid Haji Abdulla wakati nafasi ya Vijana inawaniwa na Nd. Rashid Fadhil Makame na Suleiman Fadhil Juma.

Uchaguzi kama huo pia ulishuhudiwa kwa shehia ya Kwa Gube ndani ya Jimbo la Kitope uliopangwa kufanyika katika Skuli hiyo hiyo ya Msingi na Sekondari ya Kitope.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ikiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Joseph Sinde Warioba inatengeneza rasimu itakayowasilishwa katika Mabaraza hayo ya Katiba ya Wilaya.

Utaratibu huo utaozingatia upanuzi zaidi wa Demokrasia hapa Nchini umelenga kutoa fursa zaidi kwa ushiriki wa wananchi katika kujadili rasimu hiyo itakayotoa uwakilishi wa kina wa Wananchi kutoka kila Shehia Nchini.

Othman Khamis Ame

Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
            

0 comments:

 
Top