Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema ni lazima maamuzi ya madiwani yaheshimiwe na watendaji wengine katika kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema madiwani ndio wafanya maamuzi katika Serikali ya mitaa,hivyo maamuzi yao yaheshimiwe na watendaji ili kujenga mustakbali mwema katika kuwatumikia wananchi.

Akifungua semina ya madiwani wa CUF katika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi kisiwani Pemba, Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF amesema tatizo lililopo ni kuwa mfumo uliopo sasa unatoa mamlaka makubwa kwa watendaji, hasa makatibu wa Halmashauri na Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa.

Amesema wakati Serikali imo katika mchakato wa kuleta mageuzi katika Serikali za Mitaa Zanzibar, ni vyema mageuzi hayo yakarekebisha hali isiyoridhisha iliyopo sasa.

Ametoa wito kwa Madiwani kuchapa kazi kwa bidii, na kuhakikisha wanayafahamu, kuyasimamia na kuyatekeleza ipasavyo majukumu waliyokabidhiwa.

Aidha Maalim Seif amewasihi Madiwani wa CUF kutokubali kuburuzwa na watendaji, na kuhakikisha kuwa maamuzi yao katika Mabaraza na Halmashauri yanaheshimiwa na kutekelezwa kwa ukamilifu.

“Lazima mujue matumizi ya kila senti moja. Lazima muhakikishe kuwa hakuna upendeleo katika ugawaji wa rasilimali kwa Shehia zilizomo katika Halmashauri au Baraza”, alisema Maalim Seif na kuongeza,

“Endapo Katibu au Mtendaji hafuati maagizo ya Madiwani na anafanya atakavyo, lazima mumuarifu Waziri anayehusika, na kama Waziri atapuuza wasilisheni ripoti kwa Makamu wa Pili wa Rais”,

Amefahamisha kuwa ili malengo ya utekelezaji yaweze kufikiwa ni vyema kwa madiwani kufanya kazi bega kwa bega na watendaji wengine wakiwemo wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Wabunge na Masheha, kwa vile kazi na maeneo yao ya kazi yanalingana.

Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top