Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amelaani vikali kitendo kwa kupigwa risasi na kuuliwa kwa Padre Evarist Mushi wa kanisa katoliki Zanzibar.

Amesema kitendo hicho kimevuruga sifa njema ya Zanzibar ya kuwa kisiwa cha amani.

Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF ametoa kauli hiyo kisiwani Pemba wakati akifungua semina ya madiwani wa CUF inayofanyika ukumbi wa kiwanda cha mafuta ya makonyo Wawi.

Amesema kwa niaba yake binafsi, chama chake na Serikali analaani vikali kitendo hicho cha kinyama ambacho kimeitia doa kubwa Zanzibar.

Amesema kitendo hicho ambacho hakikubaliki ni cha kusikitisha kwa vile Wazanzibari wamekuwa wakiishi kwa kuvuliana kwa kipindi kirefu bila ya kutoa vitendo hivyo.

Amesema ni wajibu wa Wazanzibari kuendeleza sifa njema ya Zanzibar kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuishi kwa kuvuliana na kuwapa matumaini wageni wanaokuja kuitembelea Zanzibar kwa shughuli mbali mbali ikiwemo ya utalii.

Ameviomba vyombo vya dola kufanya kazi ya ziada kuwatafuta waliohusika na tukio hilo na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hata hivyo amesema wakati uchunguzi huo ukiendelea kufanyika, ni vyema kwa vyombo vya dola kufanya kazi kwa umakini mkubwa ili kuepuka kuwahusisha watu wasiohusika na tukio hilo.

Katika hatua nyengine Maalim Seif ameelezea kusikitishwa kwake na kauli iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa kitendo hicho ni cha kigaidi.

Amekiri kuwa kitendo hicho ni kikubwa na kibaya, lakini hakijafikia hatua ya kuitangaza Zanzibar kuwa nchi ya kigaidi, na kwamba kufanya hivyo ni kuijengea sifa mbaya Zanzibar.

“Kauli kama hizi ukweli hazisaidii zaidi ya kutuvuruga, ni kweli ni kitendo kibaya na kikubwa, lakini ugaidi ni mkubwa zaidi na sisi hatujafikia na wala hatutofikia hatua hiyo”, alionya Maalim Seif.

Amesema ni vyema kwa viongozi wanaotokea upande wa pili wa Muungano kufanya mashauriano na viongozi wa Zanzibar kabla ya kutoa kauli ambazo zinaijengea sifa mbaya na kuitia doa Zanzibar.


Hassan Hamad, OMKR

0 comments:

 
Top